Na MWANDISHI WETU
SHABIKI na mwanachama maarufu wa Klabu ya Yanga, Haji Omary ‘Mzee Mpili’, ameibuka na kukanusha kuzushiwa kifo na baadhi ya watu.
Asubuhi, katika baadhi ya mitandao ya kijamii zilizuka tetesi kwamba Mzee Mpili amefariki kitu ambacho siyo kweli.
Akizungumza kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, Mzee Mpili amesema amesikitishwa na taarifa za kuzushiwa kifo.
Amesema hilo tukio lilitokea jana kwa mara ya pili na hivyo kuna baadhi ya watu wenye chuki ambao wamekuwa wakisambaza habari za uongo.
Amesema waliomzushia kufariki wao siyo Mungu, hivyo wanaendelea kumwongezea muda mrefu zaidi wa kuishi.
“Nilisikia kwamba nimezushiwa kifo katika mitandao ya kijamii, mimi nipo na sina tatizo na mtu.
“Wale wanaonizushia kifo ni mara ya pili hivi sasa na wao siyo Mungu, hivyo wananiongezea muda mrefu zaidi wa kuishi.
“Niwatoe hofu watu wote na tayari nimeshazungumza na baadhi ya viongozi wa Yanga kwamba mimi nipo salama,” amesema Mzee Mpili.




