Na MWANDISHI WETU
HIVI karibuni Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi katika Baraza la Eid EL Fitri lililofanyika jijini Dar es Salaam, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ambapo alisisitiza umuhimu wa kulinda maadili, kujenga jamii bora yenye uzalendo hususan kwa watoto na vijana.
Alisema hilo litawezekana endapo viongozi wa dini wataendelea kutekeleza wajibu wao ipasavyo, hasa kuijenga jamii katika elimu ya dini ambayo itawajengea maadili na kuwaepusha na vitendo vya uvunjifu wa maadili.
Pia, Rais Dk. Samia alitumia jukwaa hilo, kusisitiza matumizi sahihi ya teknolojia hususan ya Akili Mnemba (AI), katika matumizi yenye tija ya kuchochea maendeleo na kuepuka vitendo vya uchochezi na upotoshaji ambao unaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Kauli hiyo ya Rais Dk. Samia, kuhusu maadili, ilipokelewa vyema na wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo wanasiasa na wasomi, huku wakisema maadili ndiyo hujenga taifa imara lenye mshikamano na mafanikio.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, alipongeza kauli hiyo ya Rais Dk. Samia, huku akitoa wito kwa jamii kutumia teknolojia kujiletea maendeleo, badala ya kuigeuza daraja la kukashfiana na kuvunjia heshima viongozi nchini.
Chatanda alisema teknolojia hiyo isitumike kukashfu viongozi wa nchi, bali iwe nguzo ya maendeleo na mafanikio.
Alisema teknolojia imeletwa kwa madhumuni ya kujifunza na kuleta maendeleo nchini na kwingineko duniani.
Chatanda alisema baadhi ya watu ndiyo wanaosababisha matumizi ya AI, kuonekana mabaya kutokana na kutumia teknolojia hiyo kupotosha jamii.
“Wazazi tuzungumze na watoto wetu kwa lengo la kuwa na maadili ya Kitanzania, maadili yetu yapo kwa makusudi huku yakiwa na nia ya kulinda utu wa Mtanzania,” alisema Chatanda.
Pia, mwanasiasa mkongwe, Anna Abdallah, alisema sayansi na teknolojia imekuja nchini kuelimisha jamii na kutafuta fursa kupitia mitandao ya kijamii.
Anna Abdallah, alisema baadhi ya watu wasiyo na maadili mema wamekuwa wakiwadhalilisha viongozi wa serikali kwa kuwatolea lugha zisizofaa, kuwachora vibaya mitandaoni, badala ya kutumia teknolojia kujinufaisha kiuchumi.
Alisema zipo nchi zinazotumia vyema mitandao ya kijamii katika kutafuta maendeleo ya kweli na kukuza uchumi wao.
“Tunaona mitandao ya kijamii na Akili Mnemba (AI) ipo kutusaidia kutafuta elimu kwa njia hizo, sasa tunavyotumia vibaya inakuwa haina maana,” alisema.
Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa waziri katika awamu mbalimbali za uongozi, alisema utumiaji usiofaa wa mitandao ya kijamii unaleta mkanganyiko kwa taifa, jamii na hata ndani ya familia.
“Tuacheni kutumia vibaya mitandano ya kijamii, tuitumie kwa lengo la kujijenga na kupata maarifa mazuri kutoka katika nchi nyingine,”alisema.
Mama Anna aliiomba serikali isimamie sheria dhidi ya watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii.
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Nuhu Mruma, alisema maendeleo ya teknolojia ni muhimu kwa taifa.
Alisema hivi sasa imekuwa ni kawaida teknolojia hiyo kutumiwa vibaya kwa kuwatukana viongozi wa serikali, viongozi wa dini au kada nyingine.
Mruma aliwaomba wazazi na walezi kuwasisitiza watoto wao umuhimu wa kushiriki katika mafunzo ya dini.
“Mtoto ashiriki mafunzo ya dini yatamsaidia kuwa na hofu ya Mungu na hata kufuata maadili mazuri,” alisema Mruma.
UMUHIMU WA MAADILI
Naye, Profesa Wineaster Anderson anayefundisha katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), alisema taifa lisilo na maadili ni mfu, kwani nidhamu inatakiwa kuanzia ngazi ya familia.
“Maadili ni kila kitu katika jamii, inagusa maeneo tofauti katika kuchochea maendeleo na mafanikio,” alisema.
Kuhusu Akili Mnemba, Profesa Wineaster alieleza teknolojia ni dhana kubwa ya maendeleo japokuwa matumizi yake ndiyo yanaweza kutoa athari mbaya katika jamii.
Alihimiza kuitumia teknolojia kwa matokeo chanya na kuepuka matumizi yasiyo na tija ambayo yatachochea vurugu na uvunjifu wa amani.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk. Philip Daninga, alisema lengo la kuanzishwa AI ni kurahisisha mtindo wa maisha kupitia teknolojia ambayo inatatua changamoto, mabadiliko na kuacha matokeo yasiyokusudiwa.
“Tuzingatie ushauri na maelekezo ya Rais Dk. Samia ya kuchukua tahadhari ya matumizi ya teknolojia, kufahamu matumizi yake ipasavyo, inavyosaidia na kuepuka kusababisha changamoto, taharuki katika jamii na kuhakikisha jamii haipotoshwi,” alisema.
MSISITIZO WA RAIS DK. SAMIA
Akizungumza katika Baraza la Eid El Fitri jijini Dar es Salaam, Rais Dk. Samia, aliwasisitiza viongozi wa dini kuendelea kuikumbusha jamii umuhimu wa kuzingatia maadili mema.
“Bila kuwepo maadili, tukiendelea kuyaacha ya kutukanana katika mitandao ya kijamii, yanayotengenezwa kwa AI, ya kuwakashfu viongozi wa serikali, watoto wetu wakiyaona wanajifunza,” alitahadharisha Rais Dk. Samia.
RAIS Dk. Samia alisema ni muhimu kutambua kuwa siyo kila mtu anafurahi kuona Tanzania ikiwa katika hali ya amani, umoja na utulivu, hivyo ni vyema kuzidisha mshikamano na upendo katika taifa kuendelea na sifa ya Tanzania ya amani.
Aliwaeleza viongozi wa dini kuwajenga waumini kiimani na kimaadili kama vitabu vya dini vinavyoelekeza, hatua hiyo itaendelea kujenga taifa lenye amani, mshikamano, utulivu na ustahimilivu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Alisema serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuhakikisha uhuru wa kuabudu unaendelea kuwepo.
Aliwataka waumini kufahamu mipaka ya uhuru huo kwa kuheshimu sheria za nchi na haki za wengine.
Rais Dk. Samia alisema uhuru huo usigeuke chanzo cha chuki, mgawanyiko au kuvuruga amani na mshikamano wa taifa. Aliwashukuru viongozi wa dini kwa mchango wanaoutoa katika kuimarisha maadili.
“Ni ukweli usiofichika dini inapojenga maadili mema katika jamii, taifa hujenga jamii bora na maendeleo yake.
Bila kuwepo maadili, tukiendelea kuyaacha ya kutukanana katika mitandao ya kijamii, yanayotengenezwa kwa AI (akili mnemba), ya kuwakashifu viongozi wa serikali, watoto wetu wakiyaona wanajifunza,” alieleza Rais Samia.
Alionya hayo yakiachwa yaendelee, nchi haitakuwa salama wala kutulia na maendeleo yatakosekana kutokana na vurugu.
Rais Samia alisema viongozi wa dini wamekuwa sauti ya matumaini na mwongozo kwa waumini katika nyakati za changamoto za kijamii na kimaadili.
Alisema wamekuwa wafariji kwa waliokata tamaa na kuwatia moyo walio katika dhiki.
Alieleza katika nyakati hizi inaposhuhudiwa mivutano na migogoro duniani, nchi imeendelea kubaki salama na amani.
“Ni muhimu tukatambua siyo kila mtu anafurahi kutuona katika hali ya amani, umoja na utulivu, hivyo ni vyema tukazidisha mshikamano na upendo, katika taifa letu, tuendelee na sifa yetu ya Tanzania ya amani,” alisema Rais Samia.
Alieleza Waislamu na Wakristo wana wajibu wa kutekeleza kwa vitendo maamrisho mema ya vitabu vitakatifu, siyo tu katika vipindi vya mfungo wa Ramadhani na Kwaresma, bali siku zote.
“Mwezi Mtukufu wa Ramadhani haikuwa tu kipindi cha toba na ibada, ni wakati ambao mioyo yetu ilikumbushwa kuwaonea huruma wenye uhitaji,” alisema.
Aliongeza: “Kusaidiana na kuimarisha mshikamano katika jamii kama kitabu cha Quran kinavyosema ‘wema siyo kuelekeza nyuso mashariki na magharibi, bali ni imani ya kweli, kuamini Mungu yupo, kuamini siku ya kiama, kuamini kitabu chake kitukufu na kuamini mitume wake.”
“Ni kutoa mali uipendayo kwa jamaa, yatima na masikini na wenye uhitaji, katika mifumo tofauti ikiwemo sadaka au zaka na wema na kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu,” alisema.
Alisema Biblia inaeleza dini safi ni kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda na dunia pasipo mawaa.
Alimshukuru Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, kwa kumwalika katika baraza hilo na kuwapongeza Waislamu kwa kutimiza funga.
Aliwapongeza viongozi wa BAKWATA wakiongozwa kwa kuimarisha huduma za afya nchini, kwa ujenzi wa vituo vya afya kila mkoa na baadhi ya wilaya, pamoja na mkakati wa kujenga hospitali ya rufaa, Dar es Salaam.
Alisema uamuzi huo, unaunga mkono jitihada za serikali za kuimarisha huduma za afya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati na kuwaahidi ushirikiano wa vitendo.
WITO WA HESHIMA
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, aliwasihi Watanzania kuheshimu viongozi na kuwaombea kwa Mungu wafanikishe utekelezaji wa majukumu yao.
“Pamoja na kupiga makelele wanaombewa kwa nini, tunachozungumza ni mistari, tunazungumza vitabu, hatuzungumzi vitu juu juu tu,” alifafanua.
Mufti Zuberi aliwataka Waislamu kutokubali kuchokozeka na jambo la uongo halijifichi, hubainika mara moja.
“Jambo lingine ni kuwa na heshima kwa viongozi, siku hizi kila mtu anaweza kumsema mtu yeyote, haogopi Mungu wala sheria, wala uislamu, mtu anatukana anavyotakana,” alisema.
KATIBU WA BAKWATA
Akitoa salamu za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Alhaji Nuhu Mruma, alisema amani na utulivu katika nchi ni kigezo cha maendeleo kwa jamii.
“Pamoja na masikitiko makubwa tuliyopata mwisho wa mwaka uliopita, tunamshukuru Mungu kwa kutuvusha salama kama taifa na kusonga mbele,” alisema.
Alisema kuna mihimili ya kimaadili yenye kuchangia kujenga usalama na amani ndani ya jamii; moyo wa kupendana, kuhurumiana, upole na maadili mema.
“…usalama na amani ni jukumu letu sote na si la serikali pekee yake, bali ni kila mtu,” alisema.
Alitoa wito kwa Waislamu kulinda amani, kwani ndiyo mtaji muhimu kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla, huku wakiepuka hila za kuivuruga.
Alisema BAKWATA inampongeza Rais Dk. Samia kwa kuendelea kulinda amani baada vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu.
“Tumeshuhudia yaliyotokea kipindi cha uchaguzi ambayo hayakuwa na taswira nzuri kwenye nchi yetu, pongezi ziende vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha amani na usalama kurejea kwa kipindi kifupi,” aliongeza.
Alisema baraza hilo linaamini tume iliyoundwa na Rais Dk. Samia ya kuchunguza vurugu za Oktoba 29, mwaka jana, itabainisha wazi nini chanzo cha matukio hayo na kutoa njia sahihi ya namna ya kupatikana suluhisho.
“Tume itafanyia kazi matokeo yake kwa haki na baadaye kutupeleka kwenye maridhiano yatakayoleta mustakabali wa taifa letu tuendelee kuishi kama jamii moja katika nchi yetu,” alisema Alhaji Mruma.
Alisema kila mmoja anapaswa kujifunza kwa kile kilichotokea Oktoba 29 na kuhakikisha anaepuka migogoro inayosababisha mifarakano na kuathiri usalama na amani.
Katika baraza hilo viongozi mbalimbali walihudhuria wakiwemo, Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu na Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete.




