Na WAANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemwagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Denis Simba, kuzitaja taasisi zinazofanya vizuri na vibaya kwa ununuzi wa umma katika ripoti ya mwakani ya mamlaka hiyo.
Alitoa agizo hilo jana, katika hafla ya kupokea ripoti tatu za ofisi ya Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na PPRA.
“Nikuelekeze Mkurugenzi Mkuu PPRA, ili tuweze kusimamia vizuri taasisi zetu kuna kitu kinaitwa ‘name’ and ‘shame’, kwa hiyo katika ripoti yako ya mwakani ukitutajia nani wanafanya vibaya zaidi na nani wanafanya vizuri zaidi itakuwa vizuri, itawatia ari wanaofanya vibaya zaidi.
“Ili wajitahidi kufanya vizuri zaidi, badala ya kusema tu mashirika haya, sema TANESCO hawajafanya vizuri, nani wamefanya vizuri tutajie waone aibu wajitahidi wafanye vizuri, lakini niseme pia tuwataje kubainisha watendaji au taasisi zitakazobainika kukiuka sheria za manunuzi, hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao,”alisema.
Rais Dk. Samia alisema lengo la kuwaanika watendaji na taasisi zinazofanya vibaya katika ununuzi wa umma ni kulinda fedha za wananchi na kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.
MIFUMO ISOMANE
Akizungumzia mifumo ya serikali kusomana, aliziagiza Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kushirikiana kusimamia na kuimarisha mifumo hiyo kuondoa ubadhirifu wa fedha za serikali na mianya ya rushwa.
Alitoa agizo hilo, baada ya kuonekana mfumo wa ‘Nest’ kuwa na changamoto katika utekelezaji wake, hivyo kuzitaka wizara hizo kutatua tatizo lililopo.
Rais Dk. Samia aliwataka viongozi wa umma na Watanzania kwa ujumla, kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao.
“Uwajibikaji siyo chaguo bali ni wajibu, nataka kuwajibika au sitaki hapana, wajibu huo hauishii katika taasisi hizi tatu pekee, bali unatuhusu viongozi wote wa umma na Watanzania kwa ujumla.
“Kwa upande wetu serikali, tutaendelea kuimarisha mifumo ya uwajibikaji na pale ambapo kutabainika kushindwa kuwajibika au kutimiza majukumu ipasavyo kutokana na uzembe au ubadhirifu, hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zetu,”alisema.
Alieleza serikali inaendelea kusimamia rasilimali za taifa kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi.
Rais Samia alimwelekeza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, kusimamia kwa ukaribu tathmini ya mapendekezo yote yaliyotolewa na taasisi hizo tatu.
Aliahidi serikali kuzipitia kwa kina taarifa hizo na baadaye kuiwasilisha ripoti ya CAG bungeni, kwa mujibu wa Ibara ya 143 ya Kifungu cha 4 ya Katiba ya Tanzania.
MAAGIZO TAKUKURU
Aidha, Rais Dk. Samia alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, kuchukua hatua bila ya upendeleo wala muhali katika kutekeleza majukumu yake.
“Nikueleze Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, chombo chetu kiendelee kuchukua hatua bila ya upendeleo wala muhali kukabili vitendo vya rushwa na ufisadi,”alisema.
Aliwataka viongozi wa umma na binafsi kuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa na ufisadi katika maeneo yao ya uwajibikaji kulinda rasilimali za taifa.
Kwa mujibu wa Rais Dk. Samia, hali ya mapambano dhidi ya rushwa inaendelea kuimarika ikilinganishwa na miaka ya nyuma pamoja na kuwepo dosari zinazojirudia kila mwaka.
Aliipongeza taasisi hiyo kwa jitihada za kufuatilia vitendo vya rushwa katika miradi ya maendeleo kwa kuwa rushwa ni adui wa maendeleo ya taifa.
Pia, aliipongeza taasisi hiyo kuwa kutoa mchango wa kijamii katika sekta ya afya.
KUHUSU CAG
Akiizungumzia taarifa ya CAG, Rais Dk. Samia aliipongeza ripoti ya taasisi hiyo kwa kuonesha ongezeko la hati safi katika taasisi za umma mwaka 2024/25 ikilinganishwa na mwaka 2023/24.
Alisema hayo ni maendeleo makubwa yaliyofikiwa, hali inayoonesha namna serikali inavyoendelea kuboresha mikakati ya usimamizi wa rasilimali za umma.
Aliahidi serikali kuchukua hatua za mapendekezo yaliyotolewa na CAG kuhusu mapungufu yaliyojitokeza katika ripoti hiyo.
“Kwenye ripoti hii, kwa bahati nzuri CAG ametuandikia vizuri sana amebainisha mapungufu, lakini ameweka na mapendekezo yake nini kifanyike kuondokana na hali hiyo, sasa niseme tu serikali itachukua hatua kama ilivyoelekezwa na sheria zetu na kama ilivyopendekezwa na CAG,” alisema Rais Dk. Samia.
TAARIFA YA CAG
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Dk. Charles Kichere, alisema hadi kufikia Juni 30, 2025, deni la serikali lilikuwa sh. trilioni 110.05.
Dk. Kichere alisema fedha hizo zinajumuisha deni la ndani la sh. trilioni 35.5 na deni la nje sh. trilioni 74.55.
Alisema mwenendo huo unaonesha ndani ya mwaka mmoja deni limeongezeka sh. trilioni 12.7 sawa na asilimia 13.04.
Dk. Kichere alisema deni hilo ni himilivu na lipo ndani ya viwango salama vinavyokubalika kimataifa.
Vilevile, alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 amefanya kaguzi 1,553 zikihusisha 1,339 za hesabu za fedha, 18 za ufanisi, mifumo ya Tekonolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) 137 na kaguzi maalumu na za kiuchunguzi 47.
Alisema katika kaguzi hizo maalumu na kiuchunguzi, zilizokamilika ni 18 na tisa zipo katika hatua mbalimbali za kukamilika.
Dk. Kichere alisema katika kipindi hicho, ametoa hati 1,339 za kaguzi ikiwa ni ongezeko la hati 38 ikilinganishwa na hati 1,301 alizotoa mwaka 2023/2024.
Alisema hati 221 zinahusu tawala za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa, 225 za mashirika ya umma, 562 serikali kuu na 331 miradi ya maendeleo.
Mkaguzi mkuu huyo alisema kati ya hati hizo, zinazoridhisha ni 1,326 sawa na asilimia 99 na zenye shaka ni 10 ambazo sawa na asilimia 0.8 na mbaya ni moja sawa na asilimia 0.1, huku taasisi mbili akishindwa kutoa maoni ya ukaguzi.
Dk. Kichere alizitaja taasisi zenye hati zenye mashaka ni Bodi ya Korosho, Bodi ya Chai, Kiwanda cha Dawa cha Keko na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kyela-Kasurumu, ambapo ameshindwa kutoa maoni.
Alisema Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kondoa, Handeni zilipata hati zenye shaka, huku Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ikipata hati mbaya.
Dk. Kichere alisema katika utendaji wa benki za serikali ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), alibaini changamoto katika usimamizi wa mikopo, ambapo ilikopesha sh. bilioni 12.17 kwa mteja mmoja uliovuka ukomo wa sh. bilioni 7.17 na kutoa sh. bilioni 9.8 bila usajili na udhamini wa dhamana ipasavyo.
TRA YAPONGEZWA
Ripoti hiyo ya CAG imeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kuimarisha mifumo ya kodi na kuongeza ufanisi wa makusanyo, akisisitiza mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2025/26.
Dk. Kichere alisema TRA imevuka malengo ya makusanyo ya kodi, ikisaidiwa na matumizi ya mifumo ya kisasa ya kodi na Mashine za Kielektroniki (EFD).
TRA pia imepongezwa kutokana na ukaribu wake na wafanyabiashara, pamoja na utatuzi wa migogoro ya kodi kwa njia ya majadiliano, masuala ambayo yamechangia kuongezeka kodi, hasa katika maeneo kama soko la Kariakoo.
“Ufanisi huu unaiweka TRA katika nafasi nzuri ya kufikia lengo la kukusanya zaidi ya asilimia ya pato la taifa mwaka wa fedha 2025/2026,” aliongeza Dk. Kichere.
VYAMA VYA SIASA
Kwa upande wa vyama vya siasa, Dk. Kichere alisema Chama cha CUF na NRA zimepata hati zenye shaka. Alisema hakukagua hesabu za CHADEMA mwaka wa fedha 2024/2025, baada ya kupata taarifa kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu mashauri yanayoendelea mahakamani.
TAARIFA YA TAKUKURU
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Chalamila, alisema wamefuatilia matumizi ya rasilimali za umma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo 1,864 yenye thamani ya sh. trilioni 14.3.
Alisema idadi hiyo ni ongezeko ikilinganishwa na miradi 1,773 yenye thamani ya sh. trilioni 11.4, iliyofuatiliwa mwaka 2023/2024.
Chalamila alisema wamefuatilia matumizi ya rasilimali za umma katika utekelezaji wa miradi 1,864, ambapo miradi 913 ilibainika ina kasoro.
Alieleza kati ya miradi hiyo 913 yenye kasoro, 66 imeanzishiwa uchunguzi.
Alisema idadi hiyo ni pungufu ikilinganishwa na miradi 92 iliyoanzishiwa uchunguzi mwaka 2023/2024.
Alisema idadi hiyo inaonesha miradi inayoanzishiwa uchunguzi inapungua hatua inayotokana na ufuatiliaji wa TAKUKURU katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema walibaini kuwepo usimamizi dhaifu wa mikataba unaosababisha mambo sita, ambayo ni miradi kutekelezwa kwa kutozingatia matakwa ya mkataba husika, wakandarasi kulipwa fedha kwa kazi ambazo hazikutekelezwa, kutokatwa kodi ya zuio katika baadhi ya miradi, ubora wa kazi na vifaa usioridhisha.
Pamoja na kutozingatiwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na kufanyika malipo zaidi ya matakwa ya mkataba.
Alisema kupitia operesheni za uchunguzi, TAKUKURU iliokoa sh. bilioni 14.5.
Chalamila alisema kati ya fedha iliyookolewa, sh. bilioni 10.1 ni fedha taslimu iliyowekwa katika akaunti za taasisi na idara za serikali.
Alisema sh. bilioni 4.4 ilidhibitiwa na kurejesha vifaa na mali zilizoelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mkurugenzi huyo wa TAKUKURU alisema operesheni hiyo ilifanyika kuanzia Julai, 2024 hadi Juni 2025.
Alibainisha kati ya Julai, 2025 hadi Februari 2026, sh. bilioni 101.8 ziliokolewa kutokana na operesheni za uchunguzi zilizofanywa na taasisi hiyo.
TAARIFA YA PPRA
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Simba alisema mwaka wa fedha 2024/2025 walifanya tathimini ya uzingatiaji sheria, ambayo imeonesha mafanikio kutoka asilimia 76 mwaka wa fedha 2023/ 2024 hadi asilimia 79 mwaka wa fedha 2024/2025.
Alisema ongezeko hilo ni matokeo ya juhudi zilizofanywa na serikali, ikiwemo kuwepo matumizi mapya ya sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka wa fedha 2023 na mfumo wa taifa wa kielektroniki wa ununuzi wa umma NeST.
Akizungumzia matumizi ya teknolojia katika manunuzi ya umma, Simba alisema mwaka wa fedha 2024/2025 waliongeza moduli mbalimbali katika mfumo wa NeST.
Alisema taasisi za ununuzi 6,921 za ngazi za chini ambazo ni vituo vya afya, zahanati, ofisi za kata, shule za msingi na sekondari zilisajiliwa kutumia mfumo huo.
Alisema matumizi ya mfumo wa NeST yameongeza ufanisi kwa kupunguza muda wa kukamilisha mchakato wa zabuni.
Pia, umeongeza idadi ya zabuni zinazotangazwa kutoka 53,211 mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia 69,983 mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 82.
Aliongeza katika mwaka wa fedha 2024/2025, tuzo za zabuni 74,303 zilitolewa ikilinganishwa na tuzo za zabuni 44,089 zilitolewa mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 69.
Simba alitaja idadi ya wazabuni walioshiriki ni 11,564 mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia wazabuni 22,900 sawa na ongezeko la asilimia 98.
Imeandikwa na Simon Nyalobi, Ziana Bakari, Rehema Maigala na Emmanuel Mohammed.




