MUSSA YUSUPH, Dodoma Na ATHANAS KAZIGE ,Dar es Salaam
HAIJAPATA kutokea baada ya gwiji wa soka duniani, Didier Drogba kutinga bungeni jijini Dodoma akiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda.
Drogba aliwasili katika viwanja vya Bunge saa nne asubuhi akiambata na Makonda wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser 300, lenye rangi ya silva.
Akiwa amevalia suti ya rangi bluu mwanasoka huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Ivory Coast na Chelsea aliyejizolea umaarufu kimataifa, mkononi alikuwa amebeba mkoba mweusi wenye maandishi, ‘Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo’ ambapo akiwa na Waziri Makonda walikwenda karibu na lango la kuingilia bungeni kisha kuunyanyua mkoba huo kwa pamoja na kupiga picha.
Baada ya hatua hiyo, wawili hao waliingia moja kwa moja katika jengo la Bunge ambapo Drogba alikwenda kuketi eneo la wageni mashuhuri tayari kushuhudia bajeti hiyo.
Kabla ya bajeti hiyo kuanza kusomwa, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alimtambulisha mcheza kabumbu huyo ambapo shangwe zililipuka kutoka kwa wabunge ambao nao mchana baada ya kuahirishwa mjadala wa bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Cecilia Pareso, aliwatangazia fursa wabunge kupiga picha ya pamoja na Drogba.
Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Drogba alisema wakati michuano ya AFRCON iliyofanyika nchini Ivory Coast, kila mdau wa alishiriki kwani ni mashindano makubwa yenye mvuto Afrika.
Alisema anaamini Tanzania itafanya vizuri katika kufanikisha michuano hiyo.
Drogba yupo nchini kwa ziara ambayo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuitangaza zaidi Tanzania kimataifa ambayo ni nchi mwenyeji wa michuano ya Soka Afrika (AFCON 2027).
Staa huyo ambaye ni nahodha mstaafu wa timu ya soka ya Ivory Coast maarufu kama “Tembo”, amewahi kusakata kabumbu katika timu za Chelsea na Galatasaray za barani Ulaya huku sasa akimiliki timu ya Phoenix Rising ya Marekani.
KAULI YA MAKONDA
Makonda alisema uwepo wa Drobga ni uthibitisho tosha wa namna gani serikali imeamua kuitumia AFCON 2027 kuitangaza taswira ya Tanzania kimataifa.
Akizungumzia mkakati wa hamasa katika kipindi hiki cha maandalizi ya AFCON, Makonda alisema mashindano hao yanayotarajia kutimua vumbi kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, wizara imejipanga kushirikisha wadau kuhakikisha mashindano hayo siyo tu yanafanyika bali yanaweka historia na alama isiyofutika kwa taifa.
Alibainisha kuwa mkakati hamasa kuelekea AFCON 2027 umeandaliwa na utazinduliwa hivi karibuni na kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa sehemu ya mashindano kwa lengo la kunufaika na fursa za mashindano na kutangaza nchi.
“Tayari tunazo kamati mbalimbali za uratibu kitaifa na katika hili nimshukuru Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba ambaye ni mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kitaifa na mawaziri wote kwa ushiriki wao madhubuti.
Alisisitiza: “Pamoja na miundombinu iliyoelezewa hapo awali, tayari serikali imewaunganisha wadau katika sekta za utalii na ukarimu hususan mighahawa, hoteli na huduma za malazi, huduma za usafiri na ushafirishaji (magari, treni, ndege na meli) maeneo ya starehe na burudani kwa mashabiki.
Makonda alitaja hatua zingine ni maboresho ya muonekano wa miji, vivutio vya utalii (mbuga, fukwe, malikale) matibabu ya kibingwa, uhamiaji, ulinzi na usalama.
WADAU
Ally Mayay Tembele alisema ujio wa Drogba ni mafanikio makubwa kwa Watanzania wote kwani ni mchezaji aliyeitangaza Afrika kwa mambo makubwa.
“Nakumbuka mwaka 2004 Roman Arkadyevich Abramovich aliyekuwa mmiliki wa Chelsea alimsajili Drogba kwa fedha nyingi zaidi ya euro milioni 20 ni mchezaji wa mfano wa dunia.
“Drogba ana rekodi kubwa, ndio mchezaji wa kwanza kutoka Afrika kufunga mabao 100 katika Ligi Kuu ya England, kwa kweli hongera kwa Rais Samia Suluhu Hassan na waziri wetu, Makonda, Gerson Msigwa kwani kazi inafanyika kwa vitendo,”alisema Mayay.
Aliongeza kuwa serikali ipo makini kwani ujio wa Drogba dunia nzima inajua na hiyo ni sehemu ya kukuza utalii.
“Ujio wake umeongeza utalii wa Tanzania kuwa serikali ipo makini na inathamini michezo, Drogba amebeba mfano wa kuwapa hamasa wachezaji wetu kufanya mambo makubwa, kumbuka pia Drogba alikuwa anafundisha washambuliaji wengine, hii ni nafasi adimu imepatikana naomba apewe nafasi atoe darasa kwa nyota wetu,” alisema Mayay.
Hata hivyo, Mayay aliipongeza serikali kwa juhudi kubwa inayofanyika kuhakikisha mwakani michuano ya AFCON inafanyika kwa mafanikio makubwa.
Kwa upande wa Mtemi Ramadhan ambaye alizungumza na gazeti hili alisema ujio wa Drogba umeonesha jinsi ambavyo serikali ilivyojipanga kuelekea AFCON 2027.
Alisema kitendo cha ujio wa mchezaji huyo wa zamani wa Ivory Coast na Chelsea kimeleta mwamko kuwa jambo hilo lipo hapo mwakani.
“Ukweli ujio wa Drogba ni picha nzuri ya kuitangaza nchi nje ya mipaka yetu, hii haijawahi kutokea mchezaji kama huyo kuja na kwenda bungeni akiwa na mkoba wa bajeti huku amemsindikiza waziri wetu, ni kitu kikubwa sana,” alisema Mtemi ambaye aliwahi kuichezea timu ya Simba kwa mafanikio makubwa.
Gwiji wa zamani wa Taifa Stars na Yanga, Sekilojo Chambua alisema ujio wa Drogba unahamasisha michuano ijayo ya AFCON 2027, kukuza utalii wa nchi na kuongeza hamasa kuelekea mashindano hayo.
Alisema jambo hilo ni chachu kwa wachezaji watakaoitwa wajue wana jukumu kubwa la kuipambania nchi iweze kufanya vizuri.
“Maandalizi kuelekea AFCON 2027 ni mazuri, waziri nampongeza amefanya kazi kubwa kumleta Droga, hii ni hamasa kwa wachezaji wetu wafanye vizuri, kwani watatengeneza sifa kubwa kwa nchi na kwao kwa ujumla,”alisema.
Kwa upande wa Fredrick Mwakalebela alisema ujio wa Drogba umeonesha jinsi ambavyo serikali ilivyo makini na kukuza michezo kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana.
“ Drogba ni mtu mahiri katika soka kuanzia Ivory Coast na Chelsea na duniani kwa ujumla, hivyo kuja na kwenda bungeni akiwa na waziri wetu wa michezo ni kitu kikubwa na dunia yote imeona,” alisema Mwakalebela ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga.
Mwakalebela aliongeza kuwa jambo hilo ni ukweli kwamba ana imani kuwa mastaa wengi watakuja hapa nchini kabla ya kuanza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2027.
Aliwaomba wadau wa soka nchini kuendelea kuiunga mkono serikali ili lengo la kutengeneza ajira kwa vijana liweze kutimia.
HISTORIA YA DROGBA
Didier Yves Drogba Tébily alizaliwa Machi 11, mwaka 1978 ni mchezaji mstaafu wa mpira wa miguu kutoka Ivory Coast. Mara ya mwisho alichezea klabu ya Phoenix Rising F.C. kama mshambuliaji akiwa pia mmiliki wake.
104. Aliongoza Ivory Coast kwenye Kombe la Dunia ya FIFA 2006.
Baadaye aliiiongoza Ivory Coast katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2006 na 2012.




