Na MUSSA YUSUPH,
Dodoma
SERIKALI imetangaza kuwa miundombinu yote vikiwemo viwanja vya michezo vitakavyotumika katika michuano ya soka kwa Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), vitakamilika mwezi Agosti, mwaka huu.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa AFCON 2027 katika mashindano yatakayofanyika pia nchini Kenya na Uganda.
Hayo yalisemwa bungeni jijini Dodoma, jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo katika Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Makonda alisema wizara yake inaendelea na maandalizi ya mashindano hayo kwa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo katika miji ya Dar es Salaam na Arusha.
Alisema tayari Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa sh. bilioni 76.1 ambayo ni ada ya uandaaji mashindano hayo yenye mvuto zaidi Afrika.
UKARABATI VIWANJA
Makonda alisema hadi sasa ukarabati uwanja wa Benjamin Mkapa umefikia asilimia 95, ukarabati wa viwanja vitatu vya mazoezi vya Gymkhana, Meja Jenerali Isamuhyo na Shule ya Sheria umekamilika huku ujenzi wa viwanja vitatu vingine vya mazoezi vya Farasi, Leaders Club na Gymkhana II vipo katika hatua za awali.
“Ujenzi uwanja wa Arusha wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 32,000 umefikia asilimia 77.5 na ujenzi kiwanja kimoja cha mazoezi kinachojengwa katika eneo la uwanja wa Arusha umefikia asilimia 60. Ni matarajio yetu kuwa kufikia Agosti 2026, serikali itakuwa imekamilisha miundombinu yote kwa ajili ya AFCON 2027”.
Aliongeza: “Katika kudhihirisha dhamira ya dhati ya serikali kuhakikisha tunafanikisha mashindano ya AFCON 2027, tayari Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameridhia na kutoa dola 30,000,000 sawa na sh. bilioni 76.1 kama ada ya uandaaji mashindano husika. Hii ndiyo tafsiri halisi ya Dk. Samia kama mwanamichezo namba moja nchini.”
VITUO VYA MICHEZO
Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), alisema serikali imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu mingine ya michezo nchini kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati yenye lengo la kukuza vipaji, kuboresha huduma za michezo kwa wananchi.
Alisema miradi mingine ambayo inatekelezwa ni ujenzi wa vituo vya kukuza vipaji, kikiwemo cha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 49.
Alisema ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu jijini Dodoma wenye uwezo wa kuchukua watizamaji 32,500 umefikia asilimia tano.
“Ujenzi Kituo cha Mazoezi na Kupumzikia Wananchi jijini Dodoma ambao umefikia asilimia 73.5, ujenzi wa Kituo cha Mazoezi na Kupumzikia Wananchi jijini Dar es Salaam kilichofikia asilimia 49 na ukarabati uwanja wa Uhuru umefikia asilimia 70,” alisisitiza.




