• ePaper
Thursday, May 7, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

ZIARA YA RAIS KAGAME, RUTO KUIMARISHA DIPLOMASIA KIUCHUMI

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
May 5, 2026
in Habari, Kitaifa, Makala
0
ZIARA YA RAIS KAGAME, RUTO KUIMARISHA DIPLOMASIA KIUCHUMI
0
SHARES
3
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na SUPERIUS ERNEST

KUANZIA Mei 3 hadi 5 jana, Tanzania imeshuhudia ugeni wa kimataifa wa viongozi wa mataifa jirani wakifika nchini kwa ziara za kikazi zenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Mei 3, mwaka huu, Tanzania ilipokea ugeni wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame aliyewasili nchini na kukutana na Mwenyeji wake Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam kwa mazungumzo ya maendeleo baina ya mataifa hayo mawili.

Pia, Mei 4, juzi, Rais wa Kenya, Dk. William Ruto aliwasili nchini kwa ziara ya siku mbili ya kikazi akiambata na ujumbe wake ambapo alikutana na Rais Dk. Samia kwa mazungumzo ya kiuwekezaji baina ya mataifa hayo mawili.

Vilevile jana, Rais Ruto alihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, msisitizo ukiwa ni kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika maeneo mbalimbali kiuchumi na kisiasa.

Ugeni huo wote una tija kubwa kiuchumi, katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa mataifa hayo jirani ambayo yapo katika jumuiya ya Afrika Mashariki huku ushirikiano wake ukiwa ni wa enzi tangu harakati za kudai uhuru, ambapo Tanzania iliongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Wakizungumzia ziara za viongozi hao, wataalamu wa uchumi walipongeza  uimarishwaji wa ushirikiano huo wa kikanda kwa mataifa hayo jirani, ikiwa ni ishara ya kushirikiana kiuchumi hususan kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa migogoro ya kivita.

DK. DANINGA

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi Kuu ya Kivukoni, Dk. Philip Daninga, ambaye ni mbobezi wa masuala ya kiuchumi, alisema ziara hizo za kikazi za viongozi hao wakuu wa nchi, zina taswira nyingi hasa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kutokana changamoto mbali mbali zilizopo ulimwenguni za migogro ya kivita.

“Ziara hizi zimefanyika wakati muafaka kuimarisha diplomasia ya kiuchumi, kuangalia maeneo yaliyokuwa yamelega lega na kuangalia maeneo mapya ya kushirikiana kiuchumi, ambapo uchumi wa mataifa hayo katika uwekezaji unakua na kuimarika.

“Wanaangalia namna ya kushirikiana katika kufanya biashara kupitia rasilimali zilizopo kuakisi vita ya umasikini kwa wananchi wa mataifa hayo, ni ziara zenye tija, tunawapongeza sana viongozi wetu hao kwa kuona tija hiyo ya ushirikiano katika kipindi hiki kinachohitaji ushirikiano wa majirani na siyo utengano,”alisema.

Aidha, alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuwakaribisha viongozi hao nchini, kwa ziara za kikazi kuimarisha ushirikiano na kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikikwamisha maendeleo ya uwekezaji na biashara kwa wananchi wa Tanzania na mataifa hayo ya Kenya na Rwanda.

 KANYASU

Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Geita Mjini, Costantine Kanyasu, ambaye ni mtaalamu wa uchumi, alisema ziara ya Ruto na hotuba yake bungeni imefanyika wakati na inaweza kuwa imechelewa kidogo, kwani imeakisi maono yaliyo asisiwa wa viongozi wa mataifa hayo mawili ya kuimarisha diplomasia ya kisiasa na kiuchumi.

Alisema hotuba ya Rais Dk. Samia na viongozi hao, zimesisitiza kuwa adui wa mataifa hayo ni umaskini na siyo watu au wale wanaokosanisha na kuchonganisha mataifa yao, wakihimiza kuelewa kuwa jirani achaguliwi, isipokuwa adui.

“Ziara hizi ni muhimu kiuchumi, zimelenga na kusisitiza kuondoa vikwazo vyote vinavyosababisha wananchi na mataifa hayo kuwa masikini, tunawapongeza sana viongozi wetu hawa kwa maono haya katika kipindi hiki muafaka, kinachohitaji Afrika kutegemea rasilimali zake zaidi kuliko misaada kutoka nje,”alisema Kanyasu.

Aliongeza “Nampongeza sana Rais Dk. Samia kwa ukarimu wake wa jicho la kiuchumi, kupata ushauri mzuri wa kuondoa vikwazo vya kibiashara mipakani kushirikiana na mataifa hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanategemea Tanzania katika bandari, licha ya kwanza Tanzania ni taifa kubwa kuliko mengine linaweza kujiendesha, lakini Rais Dk. Samia ameonyesha unyenyekevu mkubwa kuwapokea na kuzungumza nao kwa dhamira njema ya kiuchumi,”alisisitiza 

PROFESA WANGWE

Mbobezi wa uchumi, Profesa Samuel Wangwe alisema ziara hizo zimekuwa na tija kwani kupitia makubaliano yaliyofanyika kuna faida kubwa kati ya Tanzania na nchi hizo mbili kuendeleza ushirikiano mzuri wa kiuchumi na kisiasa.

Alisema uhusiano huo, utasaidia kuimarisha uchumi wa nchi na kujenga ushirikiano mzuri uliotokana na msingi imara uliowekwa na watangulizi.

Profesa Wangwe alisema mahusiano na makubaliano yaliyopo kati ya nchi hizo yatasaidia kubadilishana uzoefu katika shughuli zao za uzalishaji mali wanazozifanya.

 “Katika makubaliano haya Watanzania wengi watapata fursa ya kuwekeza nchini Kenya na Rwanda, wao kuwekeza nchini, hiyo itasaidia uchumi wa nchi yetu kukua vizuri,”alisema.

PROFESA KINYONDO

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo alisema uhusiano wa bara moja unafaida kubwa katika uzalishaji mali.

Alisema nchi ya Kenya na Tanzania zina ushirikiano wa siku nyingi, hivyo makubaliano ya kimaendeleo waliojiwekea yatasaidia kuinua uchumi wa nchi zote mbili katika suala la uzalishaji mali.

Akizungumzia kilimo, Profesa Kinyondo alisema ni wakati sasa wakulima nchini kuzalisha mazao yenye tija kwa lengo la kwenda kuyauza nchi jirani ikiwemo Kenya.

“Tunayo mazao mengi ambayo yakipelekwa nchi zingine yatazalisha mali na uchumi wetu kukua hivyo kinachotakiwa ni kuyaongezea ubora yawe na thamani zaidi,”alisema.

Alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuwakaribisha viongozi hao nchini, huku akisema kupitia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi utakuwa na tija kwa nchi zote mbili.

TANZANIA NA RWANDA

Akieleza ushirikiano na Rwanda, katika mkutano uliofanyika hivi karibuni Ikulu, jijini Dar es Salaam, Rais Dk. Samia, alisema wamekubaliana kushirikiana maeneo sita kwa lengo la kuimarisha na kukuza uchumi wa nchi hizo.

Rais Dk. Samia alisema katika makubaliano hayo, jambo kubwa ambalo nchi hizo zimekubaliana ni eneo la biashara na uwekezaji.

“Nina furaha kuwaambia kuwa, biashara yetu kati ya Tanzania na Rwanda, imekuwa hadi kufikia sh. bilioni 644 mwaka jana.

“Pia, kuanzia mwaka 1997 hadi Machi mwaka huu, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA), imesajili miradi 42 kutoka Rwanda,”alisema.

Alisema miradi hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 325.5 ambayo imeajiri Watanzania 2,225 na kwamba, jambo hilo lina mchango mkubwa nchini.

“Takwimu hizo, zinatia moyo katika biashara yetu ambapo tumekubaliana kuendelea kushirikiana kukuza biashara na uwekezaji hususan katika kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi, vikwazo vyote vya kibiashara, tuzungumze tuviondoe tuweze kutumia vizuri Soko la Pamoja la Afrika Mashariki,”alisema.

Rais Dk. Samia, alisema eneo la pili ni uchukuzi na miundombinu ambapo serikali hizo mbili, zimekubaliana katika kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na uboreshaji wa usafiri.

“Kwa watu wasiofahamu, takwimu zinaonesha kuwa, takribani asilimia 70 ya shehena za mizigo kutoka Rwanda, inapitia katika bandari za Tanzania, wastani wa tani milioni 1.6 kila mwaka tunapitisha kwenda Rwanda,”alisema.

Rais Samia, alisema serikali hizo zimekubaliana ujenzi wa barabara zinazounganisha nchi hizo pamoja na reli, kwa lengo la kuharakisha shughuli za biashara.

“Tumekubaliana kujadili mradi wa ujenzi wa reli kipande cha reli cha Isaka hadi Kigali, ambayo itakwenda kuhamasisha na kuharakisha usafirishaji wa bidhaa,”alisema

Pia, alisema eneo la nishati, serikali hizo zina mradi wa pamoja kati ya Rwanda, Burundi na Tanzania katika mradi wa umeme wa maporomoka ya Rusumo ambao unazalisha umeme megawati 80.

“Mwaka 1976, nchi zetu mbili zilianzisha Tume ye Kudumu ya Ushirikiano wa Pamoja, ambapo mkutano wa 16 ulifanyika Julai, mwaka jana.

“Kule Kigali kupitia tume hiyo, nchi zetu mbili, zimeshirikiana katika nyanja ya biashara, kilimo, nishati, mafuta, miundombinu ya usafiri na usalama kwa ujumla,”alisema.

Kwa upande wake,  Rais wa Rwanda, Kagame alimshukuru Rais Dk. Samia kwa kudumisha ujirani mwema na udugu kati ya nchi hizo na kwamba, Tanzania ni kiungo muhimu, siyo kwa upande wa Rwanda tu, bali kwa majirani wengine katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema ushirika kati ya nchi hizo katika sekta mbalimbali hususan eneo la biashara na usafirishaji ni kiunganishi muhimu kwa Rwanda na soko la dunia.

TANZANIA NA KENYA

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano na Kenya, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Dk. Samia, alisema miongoni mwa mafanikio makubwa ni makubaliano ya kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi, vinavyokwamisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Alieleza vikwazo hivyo visivyo vya lazima, vimekuwa vikiongeza gharama na kupunguza kasi ya biashara, hivyo kuondolewa kwake, kutafungua fursa zaidi ya uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.

Rais Dk. Samia, alisema ziara ya Rais Ruto, ililenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania, Kenya na kujadili maendeleo na uwekezaji.

“Rais wa Kenya mara nyingi amekuwa akija Tanzania kwa shughuli mbalimbali, lakini leo (jana), amekuja kwa ziara rasmi ya kiserikali.

“Katika ziara hii, tumefanya mazungumzo muda mfupi uliopita kuangalia maendeleo ya nchi zetu, lakini pia tumezungumza masuala ya siasa na ulinzi na kukuza uwekezaji katika nchi zetu,” alisema.

Aidha, Rais Samia, alieleza kuwa, wamekubaliana pia katika miradi ya maendeleo ikiwemo bomba la gesi na sekta ya uchukuzi na miundombinu.

“Pia, tumekubaliana kuhusu bomba la gesi kutoka jijini Dar es Salaam, Tanzania kuelekea Mombasa, Kenya na kama mlivyoshuhudia tumesaini maelewano.

“Katika uchukuzi na miundombinu, tumekubaliana kwenye reli kutoka Bandari ya Tanga itapita Kilimanjaro hadi Kenya na usafiri wa ndani ya maji katika maziwa yetu hasa Ziwa Victoria, kuunganisha biashara ya Kenya na Tanzania,” alisema.

Aliongeza kuwa, wamejadili masuala ya usalama na biashara ya mazao ili kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo.

“Tumezungumza pia sekta ya ulinzi na changamoto za ugaidi na uhamiaji haramu kwa sababu, kuna mambo ya ugaidi na uhamiaji haramu kuongeza umakini wa watu waovu wasiwe wanapita mipakani.

RAIS RUTO

Kwa upande wake, Rais Ruto, alisema biashara kati ya Tanzania na Kenya, imeendelea kukua hadi kufikia Dola za Marekani milioni 860 mwaka jana.

“Hii inatoa tafsiri ya kukua kwa ushirikiano wa kibiashara katika nchi zetu hizi, Kenya inaihitaji Tanzania kama Tanzania inavyoihitaji Kenya, kipindi cha nyuma biashara kati ya nchi hizi, ilikuwa inainufaisha Kenya.

“Lakini kwa sasa, hali ipo na uzani sawa, miaka miwili ya nyuma, Tanzania ilikuwa inaingiza bidhaa nyingi zaidi ya Kenya, kwa sasa mwaka mmoja baadaye, hali ipo sawa,” alisema.

Aidha, Rais Dk. Ruto, alisema serikali za nchi hizo, zimekubaliana kuangalia uwezekano wa kutengeneza barabara ambayo inaunganisha Lunga Lunga, Pangani, Bagamoyo hadi Dar es Saalam.

“Sababu ya kutaka kujenga kiwanda cha kusindika mafuta pale Tanga, inatokana inatokana na fursa kubwa ya kukuza biashara, ujenzi wa viwanda vya nishati ya mafuta, mbolea na viwanda vya plastiki,”alisema.

Previous Post

RAIS RUTO AIPONGEZA NSSF TANZANIA KWA UWEKEZAJI WA DOLA ZAIDI YA MILIONI 51 NAIROBI

Next Post

DEMOKRASIA ISIZICHAFUE NCHI ZETU – RAIS DK. SAMIA

Next Post
DEMOKRASIA ISIZICHAFUE NCHI ZETU – RAIS DK. SAMIA

DEMOKRASIA ISIZICHAFUE NCHI ZETU – RAIS DK. SAMIA

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

MSAMAHA WA RAIS DK. SAMIA WAGUSA WAFUNGWA WAZEE, WENYE UJAUZITO

MSAMAHA WA RAIS DK. SAMIA WAGUSA WAFUNGWA WAZEE, WENYE UJAUZITO

5 months ago
UWEKEZAJI WA SHILINGI BILIONI 50 KITUO CHA MPOMVU WAIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME KANDA YA ZIWA

UWEKEZAJI WA SHILINGI BILIONI 50 KITUO CHA MPOMVU WAIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME KANDA YA ZIWA

2 months ago

Popular News

  • RAIS DK. SAMIA AKEMEA VIONGOZI ‘KUVIMBA’

    RAIS DK. SAMIA AKEMEA VIONGOZI ‘KUVIMBA’

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DEMOKRASIA ISIZICHAFUE NCHI ZETU – RAIS DK. SAMIA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • ZIARA YA RAIS KAGAME, RUTO KUIMARISHA DIPLOMASIA KIUCHUMI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS RUTO AIPONGEZA NSSF TANZANIA KWA UWEKEZAJI WA DOLA ZAIDI YA MILIONI 51 NAIROBI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TANZANIA KAMILI AFCON 2027

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?