Na NASRA KITANA
WAKATI leo ikishuka dimbani dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco, timu ya soka Yanga imesema ipo fiti kuhakikisha inapata ushindi katika mtanange huo wa kwanza wa kundi B wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Yanga itachuana na AS FAR saa 10:00 jioni katika mechi itakayopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza kutoka Zanzibar, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema hana presha na mchezo huo kwani wamejipanga kupata ushindi.
Pedro amesema pamoja ya kutofanya mazoezi ya kutosha na kikosi chake lakini ana imani watapata matokeo mazuri katika mchezo huo.
Kocha huyo amesema hana hofu na kikosi chake kwani anajua ubora wa wachezaji wake na jinsi wanavyojituma uwanjani.
“Tunaingia katika mchezo mgumu, hatuna presha na wala hakuna ambaye tunamhofia, tuna matumaini makubwa ya kupata ushindi kutokana na mbinu pamoja mifumo ambayo nimewafundisha wachezaji wangu,” amesema Pedro.
Kocha huyo amesema wamefanya marekebisho mapungufu yote yaliyojitokeza katika mechi zilizopita ili kufanya vizuri katika mchezo huo.
Amesema lengo lao kubwa ni kuhakikisha timu yake inashinda katika mchezo huo na inayofuata ili kumaliza kundi ikiwa nafasi ya kwanza.
Naye nyota wa timu hiyo, Dikson Job amesema wachezaji wanajua umuhimu wa mchezo huo na wamejipanga kupambana kwa jasho na damu kupata ushindi.
“Huu ni mchezo muhimu kwetu kupata ushindi hasa katika uwanja wetu wa nyumbani, hatuna hofu na wachezaji wote tumejipanga vyema kuhakikisha hatupotezi na kujizolea pointi tatu muhimu,” amesema Job.
Katika mashindano hayo, Yanga ipo kundi B na timu za Al Ahly ya Misri, AS FAR ya Morocco na JS Kabyile ya Algeria.




