Na AMINA KASHEBA
BAADA ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho FA, timu za Yanga na Simba zinaweza kukutana katika mchezo wa fainali.
Timu hizo, zimepangwa kucheza hatua ya nusu fainali katika michezo miwili tofauti ambapo Yanga itachuana na Azam FC.
Pambano hilo, limepangwa kufanyika Juni 21, mwaka huu katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza.
Huku Simba yenyewe imepangwa kucheza Juni 20, mwaka huu na Coastal Union katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Kama timu hizo zitatinga fainali, ndani ya msimu huu Yanga na Simba zitakuwa zinapambana mara ya tano.
Awali zilipambana Septemba 16, mwaka jana ambapo
Yanga iliichapa Simba 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii, bao la ushindi lilipachikwa wavuni na Pacome Zouzoua.
Timu hizo, zilipambana tena katika Uwanja wa New Amaan Complex, Machi Mosi, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo zilitoka suluhu.
Timu hizo zilipambana tena Aprili 29, mwaka huu katika mchezo wa Kombe la Muungano ambapo Simba ilishinda 1-0 katika Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Bao pekee la Simba liliwekwa kimiani kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 120 na mchezaji wake Selemani Mwalimu kufuatia Clatous Chama kufanyiwa madhambi na Edmund John katika eneo la hatari.
Mchezo huo ulilazimika kwenda dakika 120 baada ya kumalizika kwa suluhu muda wa kawaida ndani ya dakika 90.
Mei 3, mwaka huu, timu hizo zilipambana katika mchezo wa ligi hiyo, zilitoka sare ya 2-2.
Hata hivyo, mashabiki wengi wa timu hizo wanasubiri kuona kama timu hizo zitakutana tena.
Tayari taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeeleza kuwa maandalizi ya michezo hiyo yanaendelea vizuri.
Katika michuano hiyo, Yanga ilitinga nusu fainali baada ya kuichapa JKT Tanzania kwa mabao 2-0.
Azam imeingia hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa FC katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Kikosi cha Simba kilisonga mbele baada ya kuigagadua TRA mabao 4-0 wakati Coastal Union ilishinda kwa mikwaju ya penati 4-2 dhidi ya Singida Black Stars.




