NA MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kung’ara katika nyanja za kimataifa, ambapo safari hii, Umoja wa Afrika (AU), umempendekeza kuteuliwa kuwa kinara wa umoja huo katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto,
Kwa mujibu taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, kwa vyombo vya habari, Rais Dk. Samia anatarajiwa kuthibitishwa na Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), utakaofanyika kesho hadi Februari 15 mwaka huu.
Taarifa hiyo ilisema katika mkutano huo, Rais Dk. Samia ambaye aliwasili nchini humo jana, anatarajiwa kupitishwa rasmi kuwa kinara wa AU katika masuala ya afya ya mama na mtoto.
“Katika mkutano wa mwaka huu, Rais Dk. Samia amependekezwa kuteuliwa kuwa kinara wa Umoja wa Afrika katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, uteuzi ambao unatarajiwa kupitishwa rasmi na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo: “Uteuzi huo unaakisi dhamira ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, ustawi wa familia na maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika.
Tayari Rais Dk. Samia amewasili jijini Addis nchini Ethiopia, kushiriki Mkutano huo, ambapo leo anatarajiwa kushiriki mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC), utakaofanyika chini ya uenyeji wa Rais wa Kenya, William Ruto na baadaye kuhudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.
Pia Rais Samia katika mkutano huo, anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali, wakiwemo Waziri Mkuu wa Eswatini, Russell Dlamini, Rais wa Comoro, Azali Assoumani.
Wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Amina Mohammed na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Sidi Ould Tah, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na maendeleo.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika utafunguliwa rasmi Februari 14, ukiwa na kaulimbiu: “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Huduma Salama za Usafi wa Mazingira, Kufikia Malengo ya Ajenda 2063.”
Taarifa hiyo ilisema, kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza hatua za pamoja za bara la Afrika katika kuhakikisha usalama wa rasilimali maji, afya ya jamii na maendeleo endelevu.
Ilifafanua kuwa,Tanzania inakamilisha muda wake wa kuhudumu katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, baada ya kulitumikia kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2022 hadi 2026 na kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha amani, utulivu na usalama Afrika.
“Mkutano huo utatangaza rasmi uongozi wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2026, ambapo Jamhuri ya Burundi itachukua nafasi ya Uenyekiti wa Umoja huo, huku Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Mwenyekiti, ikiwakilisha Kanda ya Mashariki, nafasi inayoakisi imani ya nchi wanachama kwa mchango na uongozi wa Tanzania katika masuala ya Bara la Afrika.
“Katika mkutano wa mwaka huu, Rais Dk. Samia amependekezwa kuteuliwa kuwa kinara wa Umoja wa Afrika katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, uteuzi ambao unatarajiwa kupitishwa rasmi na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo: “Uteuzi huo unaakisi dhamira ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, ustawi wa familia na maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika.
“Kupitia ushiriki wake katika mkutano huu, Tanzania inalenga kuendelea kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kikanda, kimataifa, kutetea maslahi ya taifa na kuchangia kikamilifu ujenzi wa Afrika yenye amani, mshikamano, uthabiti wa kiuchumi na maendeleo endelevu.”
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ndiyo chombo cha juu zaidi cha uamuzi cha umoja huo, chenye mamlaka ya kupitisha maazimio, matamko na mwelekeo wa sera za Afrika.




