Na MWANDISHI WETU
STAA wa Yanga, Allan Okello, ameing’arisha timu yake baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Singida Black Stars.
Yanga iliibuka na ushindi huo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliofanyika Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Mchezo ulianza kwa kasi huku kila timu ikihitaji ushindi, dakika ya kwanza, Yanga nusura wapate bao ambapo Okello alipata nafasi na kufumua shuti lililopaa juu ya lango.
Yanga walipata bao la kuongoza dakika ya 13, lililowekwa kimiani na Okello kwa mpira wa faulu, kufuatia Mudathir Yahya kufanyiwa madhambi na mabeki wa Singida Black Stars na mpira kujaa wavuni.
Singida BS walijibu shambulizi dakika ya 19, Emmanuel Keyekeh alifumua shuti lililotoka nje ya lango.
Katika dakika ya 23, benchi la ufundi la Singida BS liliamua kumtoa kipa Metacha Mnata na kumwingiza Obasogie Amas baada ya kutoridhishwa na kiwango chake.
Nyota wa Yanga, Mudathir iliipatia timu yake bao la pili dakika ya 41, baada ya kufumua shuti kali kufuatia mabeki na kipa wa Singida, Amas kujichanganya kuokoa mpira uliotoka kwa Maxi Nzengeli na kujaa wavuni, hadi mapumziko ya kipindi cha kwanza, Yanga ilikuwa mbele kwa bao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Singida BS ikionekana kuhitaji bao, dakika ya 55, Keyekeh, alipiga shuti mpira ukatoka nje ya lango.
Wakitandaza kandanda safi huku wakigongeana pasi fupi fupi, Yanga walipata bao la tatu katika dakika ya 69 likiwekwa kimiani na Okello akiwa nje ya eneo la hatari na shuti lake kutinga wavuni moja kwa moja, hadi mchezo unamalizika, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Kufuatia ushindi huo, katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imerejea kileleni ikifikisha pointi 57 nyuma ya Simba yenye pointi 55 huku Singida BS ikishikilia nafasi ya nne kwa poinyi zake 38, timu zote zimeshacheza mechi 24 kila mmoja.
Yanga: Djigui Diarra, Frank Assink, Ibrahim Bacca, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua/ Mohamed Damaro, Chadrack Boka, Allan Okello, Mudathir Yahya, Prince Dube, Yao Kouassi na Duke Abuya.
Singida Black Stars: Metacha Mnata/ Obasogie Amas, Abdulmalik Zakaria, Ibrahim Imoro, Ande Koffi, Ahmed Pipino, Kennedy Juma, Emmanuel Keyekeh, Horso Muaku, Ndumumwe Mossi, Linda Mtange na Offen Chikola/ Lamin Jarjou.




