Na MUSSA YUSUPH, Dodoma
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeanika mikakati kabambe ya ujenzi wa viwanda ya sukari, mafuta ya kupikia na dawa za binadamu kwa lengo la kuliondolea taifa mzigo wa uagizaji bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Utekelezaji wa mikakati hiyo, umezingatia miongozo mbalimbali ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/2027 – 2030/2031), Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2025, sheria na sera mbalimbali.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini hapa jana, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema wizara imeendelea kuweka mazingira wezeshi kuchochea mageuzi ya uchumi fungamanishi, jumuishi na shindani unaojengwa katika msingi wa kuongeza thamani ya rasilimali zinazozalishwa nchini na kuimarisha viwanda vinavyozalisha bidhaa kwa wingi kutumia malighafi za ndani.
“Jitihada hizo ni utekelezaji wa malengo ya Dira ya 2025 ambayo imejielekeza kuhakikisha upatikanaji bidhaa muhimu, kuzalisha bidhaa bora, kutoa ajira kwa wingi na kuongeza mauzo nje ya nchi. Kupitia mwelekeo huo, viwanda vipya vimejengwa na vingine vimefanyiwa upanuzi,” alisisitiza.
UPANUZI WA VIWANDA VYA SUKARI
Waziri huyo, alisema Tanzania ina viwanda saba vya kuzalisha sukari ambavyo ni Kilombero Sugar, Tanganyika Planting Company Limited (TPC – Kilimanjaro), Kagera Sugar (Kagera), Mtibwa Sugar (Morogoro), Mkulazi Holding (Morogoro), Manyara Sugar (Manyara) na Bagamoyo Sugar (Pwani).
Alisema viwanda hivyo vina uwezo kuzalisha sukari tani 800,000 kwa mwaka ambapo hadi kufikia Aprili mwaka huu, vimezalisha tani 410,979 za sukari, mahitaji yakiwa tani 550,000.
Viwanda hivyo, vimetoa ajira za moja kwa moja 28,500 na zisizo za moja kwa moja 95,000.
“Katika kuhakikisha nchi inapunguza uagizaji sukari kutoka nje ya nchi, viwanda vya Mkulazi Holding na Kilombero Sugar, vimefanya upanuzi kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.
Aliongeza: “Kufuatia upanuzi huo, Kiwanda cha Kilombero kitakuwa na uwezo kuzalisha tani 226,000 kutoka tani 123,000 kwa mwaka ambapo majaribio ya uzalishaji, yamekamilika na uzalishaji utaanza Juni mwaka huu.”
Kwa mujibu wa Judith, Kiwanda cha Mkulazi, kimeongeza mtambo utakaozalisha sukari ya viwandani ambapo majaribio ya mitambo, yamefanyika na tayari kiwanda kimezalisha tani 256 za sukari ya kiwandani.
Alisema kukamilika kwa upanuzi huo, kunawezesha viwanda vyote viwili kuzalisha ajira za moja kwa moja 8,500 na zisizo za moja kwa moja 25,000.
UJENZI VIWANDA VYA DAWA
Judith alisema Tanzania ina viwanda 14 vya kuzalisha dawa za binadamu na vifaa tiba vyenye uwezo wa kuzalisha asilimia 20 ya dawa na vifaa tiba zinazohitajika nchini.
Katika kukabiliana na uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi, alisema serikali imeendelea kutekeleza mikakati mahsusi kuhakikisha sekta hiyo inaongeza uwekezaji wa viwanda vya dawa na vifaatiba kufikia asilimia 60 ya mahitaji ya dawa na vifaatiba ifikapo mwaka 2035.
Alitaja mafanikio ya jitihada hizo ni ujenzi wa viwanda 11 katika mwaka 2025/2026 na kuanza majaribio ya uzalishaji dawa za binadamu na vifaatiba.
Kati ya viwanda hivyo, alisema viwili vinazalisha maji tiba, vitatu vitendanishi vya maabara, vitatu vinazalisha dawa za vidonge na maji huku viwanda vitatu vinazalisha vifaa tiba.
“Viwanda hivyo vina uwezo wa kuzalisha vizio (units) bilioni 3.5 za dawa za binadamu na kutoa ajira za moja kwa moja 4,200 na zisizo za moja kwa moja 21,000.
“Hadi kufikia Aprili mwaka huu, viwanda hivyo vimezalisha vizio (units) bilioni 1.2 za dawa za binadamu.
“Aidha, kiwanda cha kuzalisha dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARV) cha Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI) kilichopo Arusha, kimeanza ukarabati zikiwa ni juhudi za kuzalisha dawa hizo nchini,” alisisitiza.
ONGEZEKO VIWANDA VYA MAFUTA YA KUPIKIA
Kwa upande wa viwanda vya mafuta ya kupikia, alisema Tanzania ina viwanda 1,604 vya kuzalisha bidhaa hiyo, kati ya hivyo, 1,038 ni vidogo sana, 543 vidogo, tisa vya kati na 14 vikubwa.
Alisema viwanda hivyo vina uwezo wa kuzalisha mafuta ya kupikia tani milioni 2.5 kwa mwaka, vikatoa ajira za moja kwa moja 10,755 na zisizo za moja kwa moja 36,416.
Pia, alisema kwamba, viwanda hivyo, vinazalisha tani 302,000 za mafuta huku mahitaji yakiwa tani 700,000 kwa mwaka.
“Hivyo, tani 430,000 huagizwa ili kutosheleza mahitaji ya ndani.
Serikali imeendelea na juhudi mbalimbali kujitosheleza na mahitaji ya mafuta ya kupikia.
“Katika mwaka 2025/2026, kiwanda cha Vion Win cha kukamua na kusafisha mafuta ya alizeti na kuzalisha mashudu kwa ajili ya chakula cha mifugo kilichopo Mkoa wa Singida, kimejengwa.
“Kiwanda hicho, kimewekeza mtaji wa sh. bilioni 5.5. Hadi kufikia Aprili mwaka huu, kiwanda kimetoa ajira za moja kwa moja 70 na zisizo za moja kwa moja 300. Kiwanda kina uwezo uliosimikwa kuchakata tani 100 za mbegu za alizeti kwa siku.”
Vilevile, alisema kiwanda cha Mainland Group Agro Process kilichopo Dodoma, kimefanya upanuzi utakaosindika mbegu za alizeti tani 150,000 kutoka tani 75,000 kwa mwaka.
Hadi kufikia Aprili mwaka huu, alisema kiwanda kimezalisha mafuta ya kupikia tani 48,000 huku kikitoa ajira za moja kwa moja 450 na zisizo za moja kwa moja 2,000.
MWENENDO WA BIASHARA
Judith, alisema biashara ya Tanzania nje ya nchi, imekuwa ikiongozeka mwaka hadi mwaka.
Alisema mauzo ya bidhaa nje ya nchi, yaliongezeka kufikia dola milioni 10,080.9 mwaka jana, ikilinganishwa na dola milioni 8,702.0 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 16.
Alisema ongezeko hilo, linatokana na kuimarika mikakati ya kuboresha mazingira ya biashara nchini, utafutaji masoko, kuzalisha bidhaa zinazokidhi ushindani nje ya nchi na kupunguza milolongo ya hatua za kusafirisha bidhaa nje ya nchi.
“Bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni ufuta, tumbaku, mbaazi, ngano, mchele, maharage, mahindi, kahawa, pamba na parachichi.
“Mazao ghafi ya mifugo ni samaki na bidhaa za viwandani ambazo ni dhahabu, kakao, makaa ya mawe, vigae na mabati.
“Mwaka 2025, bidhaa zilizoingizwa nchini zilikuwa na thamani ya dola milioni 16,031.3 ikilinganishwa na dola milioni 15,684.5 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 2.2.
“Ongezeko hilo linatokana na kuagiza kwa wingi bidhaa ambazo hazizalishwi nchini na zinazotumia teknolojia ya juu,” alieleza.
Alizitaja bidhaa zilizoagizwa kwa wingi ni magari, bidhaa za kutengeneza lami, bidhaa za chuma, mashine za hospitalini, dawa baridi, mafuta ya petroli, gesi na sukari ya viwandani.
MAOMBI YA FEDHA
Katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Viwanda na Biashara ililiomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. bilioni 137.8.
Waziri Judith, alisema kati ya fedha hizo, sh. bilioni 104.1 ni matumizi ya kawaida huku sh. bilioni 33.6 ni matumizi ya maendeleo.
Alieleza kuwa, katika sh. bilioni 104.1 za matumizi ya kawaida, sh. bilioni 78 ni mishahara na sh. bilioni 26 ni matumizi mengineyo huku fedha zote za maendeleo ni za ndani.
MAONI YA KAMATI
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mariam Ditopile, alisema kamati hiyo inashauri wizara kushirikiana na mamlaka nyingine za serikali, kufanya tathmini ya kina kuhusu tozo mbalimbali na athari zake katika biashara.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kuchochea ukuaji uchumi wa taifa.
Pia, alisema wepo wa bidhaa feki sokoni unasababishwa na ukosefu udhibiti wa kutosha wa mamlaka husika jambo linalosababisha serikali kukosa mapato, kuathiri uwekezaji na kuleta athari kwa watumiaji.
Hivyo, alisema kamati inaishauri serikali kuimarisha ukaguzi wa bidhaa mipakani, sokoni na kuziongezea nguvu mamlaka husika kwa kuwaongezea rasilimali watu na fedha ili kuimarisha ukaguzi nchi nzima.




