Na MWANDISHI WETU
TANZANIA imejipanga kudhibiti uendelezaji holela wa makazi pembezoni mwa miji kuepuka gharama kubwa za kurekebisha miundombinu hapo baadaye.
Akizungumza katika Jukwaa la 13 la Miji Duniani (WUF13) jijini Cairo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, alieleza kuwa Tanzania imeweka mkakati madhubuti wa kitaifa kusuka upya mustakabali wa miji kabla ya ujenzi holela kushamiri.
Profesa Shemdoe alisema serikali imeamua kuelekeza nguvu zake katika maeneo ya pembezoni mwa miji, akibainisha kuwa Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Arusha zinapanuka kwa kasi ya mlalo.
Alionya kuwa, ukuaji wa miji bila mpango wa mapema unasababisha makazi yasiyo rasmi, ukosefu wa ajira na changamoto za huduma muhimu kama maji safi, umeme na usafi wa mazingira.
“Ukuaji wa miji unapotokea bila mipango ya mapema unatengeneza makazi yaliyotawanyika na ukosefu wa ajira.
Kuweka miundombinu katika maeneo haya baada ya kuwa tayari yamejengwa ni gharama kubwa zaidi kuliko kuyapanga mapema kabla hayajajengwa,” alisema.
Alisema serikali imezindua miongozo mipya ya mipango ya miji na udhibiti wa uendelezaji, pamoja na miongozo ya kuhifadhi mazingira ya kijani.
Kupitia mifumo ya kidijitali na taarifa za kijiografia (GIS), serikali inarasimisha makazi ya pembezoni na kugawa viwanja vilivyopimwa kuhakikisha matumizi bora ya ardhi.
Profesa Shemdoe alisema Tanzania inatekeleza programu ya Kupandisha Kiwango cha Miundombinu na Ushindani wa Miji (TACTIC) inayotekelezwa katika miji 45, ikilenga barabara, masoko na udhibiti wa mafuriko.
Aidha, alieleza kuwa Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) Awamu ya Kwanza na ya Pili unalenga kuongeza miundombinu inayohimili mabadiliko ya tabianchi.
Pia, serikali inawekeza katika miji ya kati na pembezoni kwa kujenga masoko ya kisasa 28, vituo vya usindikaji wa mazao ya kilimo na kuanzisha Ukanda wa Kiuchumi wa Kwala.
Alisema pamoja na mambo mengine hatua hizo zinalenga kuchochea upatikanaji wa fursa za ajira karibu na wananchi.
Profesa Shemdoe alisisitiza kuwa ujenzi wa masoko makubwa zaidi ya 15 na uboreshaji wa sekta isiyo rasmi, hususan kwa vijana na wafanyabiashara wadogo ni sehemu ya ajenda kuu ya kitaifa ya kupunguza tatizo la ajira na kuimarisha uchumi wa miji.
Waziri huyo alisema kwa mkakati huo, Tanzania inalenga kujenga miji yenye usawa, miundombinu imara na inayoweza kukabiliana na changamoto za tabianchi huku ikiepuka gharama kubwa za kurekebisha makosa ya uendelezaji holela.




