MUSSA YUSUPH NA SELINA MATHEW
SERIKALI imetangaza hatua mpya na za kimkakati kupunguza matumizi ya fedha taslimu kuanzia Mwaka wa Fedha 2026/2027, ikiwa ni juhudi za kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuongeza uwazi katika miamala ya fedha.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Omar, alitangaza mkakati huo bungeni jana alipowasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Alisema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuboresha mfumo wa malipo ya papo kwa hapo (TIPS) ili kuongeza ufanisi, usalama na urahisi wa kufanya miamala.
“Mwaka jana mfumo huo ulirekodi miamala milioni 651 yenye thamani ya sh. trilioni 54.9, ikilinganishwa na miamala milioni 453 yenye thamani ya sh. trilioni 29.82 mwaka 2024, jambo linaloonyesha ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali.
“Kutokana na mafanikio hayo, serikali imeelekeza kuwa malipo kwa huduma mbalimbali yafanyike kwa njia za kidijitali, ikiwemo tozo, ushuru na nauli za usafiri wa umma kama mabasi ya mwendokasi, reli, usafiri wa anga pamoja na huduma za vivuko na madaraja,” alibainisha.
Alisema biashara katika maeneo makubwa kama majengo ya biashara, vituo vya mafuta, kumbi za mikutano, viwanja vya michezo na maonesho ya biashara kama Sabasaba na Nanenane, zitalazimika kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali.
“Sekta ya elimu pia imejumuishwa ambapo ada na michango yote kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu italipwa kwa njia za kielektroniki. Vilevile, huduma za hoteli, migahawa na sekta ya utalii zitapaswa kutumia malipo ya kidijitali,” alibainisha.
BIMA YA AFYA KWA WOTE
Katika hatua nyingine, serikali inatarajia kukusanya sh. bilioni 7.5 kupitia vyanzo vipya vya mapato vitakavyowezesha kugharamia utekelezaji wa bima ya afya kwa wote nchini.
Balozi Khamis alisema hatua hiyo inatokana na mapendekezo ya marekebisho ya sheria na kanuni yanayolenga kuongeza uwezo wa kifedha wa serikali katika sekta ya afya.
Alieleza kuwa miongoni mwa hatua hizo ni kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147 kwa kuongeza ushuru wa bidhaa kwa sh. 20 kwa kila sigara 1,000 zinazotambulika chini ya HS Heading 24.02 na 24.03.
Pia, alisema serikali inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Sukari, Sura ya 251 pamoja na kanuni zake kwa kuongeza tozo ya sh. 10 kwa kila kilo moja ya sukari inayozalishwa ndani ya nchi au kuagizwa kutoka nje.
Kwa mujibu wa waziri huyo, tozo ya sukari itakusanywa na Bodi ya Sukari Tanzania na kuwasilishwa katika Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote, kuhakikisha fedha hizo zinatumika moja kwa moja kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Balozi Omar alisema lengo la hatua hizo ni kuhakikisha mfumo wa bima ya afya kwa wote unakuwa endelevu na wenye uwezo wa kuwahudumia wananchi bila ubaguzi.
Aliongeza kuwa maboresho hayo yanalenga kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.
Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 ya sh. trilioni 62.3 ni ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/26.
Katika bajeti hiyo, mapato yanatarajiwa kuwa sh. trilioni 46.79 ambapo mapato ya kodi ni sh. trilioni 36.99, mapato mengine ni sh. trilioni 9.24 ikijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa sh. trilioni 1.97 na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo sh. bilioni 563.1.
“Ili kuendana na dhamira yetu ya kujitegemea katika uendeshaji wa serikali na maendeleo, takribani robo tatu ya bajeti yote ya mwaka 2026/27, sawa na asilimia 74.2 inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Balozi Khamis, bajeti hiyo ni ya kwanza katika utekelezaji Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/2027 – 2030/2031).




