Na IRENE MWASOMOLA
ZIARA ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, mkoani Mara, imeacha neema kwa wanawake mkoani humo.
Katika ziara hiyo, baadhi ya wanawake walitatuliwa changamoto zao zikiwemo ukosefu wa mitaji, utatuzi wa migogoro ya ardhi na kutopata huduma ya nishati ya umeme.
Hatua hiyo imeendelea kuwapa matumaini wanawake kuwa CCM, ndiyo Chama pekee kinachojali maisha ya wananchi kwa kumaliza changamoto zao.
Pia, ziara hiyo imetafsiri kwa vitendo falsafa ya ‘Kazi na Utu’ baada ya Kihongosi kutatua na kusikiliza changamoto hata za wanawake wenye mahitaji maalumu.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Jimbo la Bunda, Kihongosi, akisikiliza kero za wananchi, Shida Kashinde, alipatiwa mtaji sh. milioni moja kufanya biashara ya kuuza matunda.
Shida alimwomba Kihongosi amsaidie fedha hizo, baada ya kutelekezwa akiwa na watoto wake ambao hamudu gharama za kuwatunza.
“Mimi sina mume nilizalia nyumbani, nina changamoto ya jicho, tuna migogoro na ndugu zangu wameninyang’anya shamba naomba mtaji shilingi 500,000.
“Nimeteseka miaka 19 nahangaika na familia, naomba nisaidie mtaji niweze kuhudumia familia yangu ninahangaika,”alisema.
Aidha, Kihongosi alisikiliza changamoto ya Veronica Philip, aliyekuwa na changamoto ya mgogoro wa ardhi, baada ya kujenga eneo la wazi, ambapo alimwagiza ofisa ardhi wa Manispaa ya Musoma kutatua.
Arejesha tabasamu kwa mjane
Aidha, katika tukio jingine, Kihongosi, alitatua changamoto ya mkazi wa Manispaa ya Musoma mjane Lucia Mwita, aliyehitaji mchango sh. 600,000 kumlipia mtoto wake gharama za bweni.
Lucia alisema ana mtoto anayetarajia kuhitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Makoko, ambapo alitoa fedha hizo.
“Mimi nitatoa 600,000 ya kumpa huyu mama akamlipie mtoto wake, lakini manispaa ijitafakari kwanini shule hiyo inakwenda kinyume na sera ya serikali ya elimu bila malipo, mtoto asikae nyumbani,”aliongeza.
Pia, Kihongosi alitatua changamoto ya mkazi wa Busege wilayani Butiama, ambaye nyaya za umeme zimepitishwa juu ya nyumba yake zinazosababisha kutopata umeme wa uhakika, ambapo alitua kero hiyo kwa kutoa maagizo kwa TANESCO.
Wabunge wanawake wafunguka
Mbunge wa Jimbo la Musoma Mijini, Mgore Kigore, alisema ujio wa Kihongosi mkoani humo ni neema kwa kuwa ametatua kero mbalimbali.
Mgore alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kutoa sh. milioni 426 kupitia mikopo ya asilimia 10 ambapo wanawake wamenufaika.
Mbunge wa Jimbo la Bunda, Ester Bulaya, alimshukuru Rais Dk. Samia kuendelea kumtua mama ndoo kichwani baada ya kutoa zaidi ya sh. bilioni tisa kutatua changamoto ya maji.
Mei 17 mwaka huu, Kihongosi alihitimisha ziara ya siku nne mkoani Mara iliyoanza Mei 14, ambapo alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Majimbo ya Tarime Vijijini, Musoma Mjini na Bunda.




