Na SELINA MATHEW
SIASA za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Ismani mkoani Iringa, zimeendelea kushika kasi huku Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikielekeza nguvu zake kuomba ridhaa ya wananchi kupitia mgombea wake, Emmanuela Mtatifikolo.
Mgombea huyo, anatajwa kama kiongozi mwenye uzoefu, msimamo na uwezo wa kuendeleza kasi ya maendeleo iliyoachwa na hayati William Lukuvi.
Katika kipindi hiki cha kampeni, hoja kubwa inayotawala katika mikutano ya kisiasa ndani ya jimbo hilo ni nani anayefaa kuendeleza agenda ya maendeleo ambayo wananchi wa Ismani wameijenga kwa miaka mingi chini ya uongozi wa CCM.
Barabara, elimu, huduma za afya, maji na maendeleo ya vijijini ni miongoni mwa masuala yanayotajwa mara kwa mara katika mikutano ya kampeni.
Kwa CCM, uchaguzi huo unaonekana kuwa zaidi ya ushindani wa kisiasa, bali ni jukumu la kutafuta kiongozi mwenye uwezo wa kusimamia maendeleo yaliyopo na kuongeza kasi mpya ya utekelezaji wa miradi ya wananchi.
Ndiyo maana viongozi mbalimbali wa Chama, wanajitokeza kumtetea na kumnadi Emmanuela wakieleza kuwa, ana sifa zinazohitajika katika uongozi wa umma.
Miongoni mwa viongozi waliovuta hisia za wananchi katika kampeni hizo ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Fadhili Maganya, ambaye alisema Chama hakikufanya makosa kumteua Emmanuela kuwa, mgombea wake katika uchaguzi huo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Kising’a mkoani Iringa, Maganya alisema Emmanuela ni mmoja wa viongozi walioonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi tangu alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na baadaye Babati.
“Tulimwona anatosha, ana uzoefu mkubwa, akitumwa anakimbia wala hatembei,” alisema Maganya huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza katika mkutano huo wa kampeni.
Kauli hiyo imeendelea kutafsiriwa na wafuasi wa CCM kama ishara ya imani kubwa ambayo Chama kinayo kwa mgombea wake, hasa ikizingatiwa amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya serikali na kuthibitisha uwezo wake katika utendaji.
Maganya alisema CCM haiwateui viongozi kwa kubahatisha, bali hupitia historia ya utendaji, uwezo wa kusimamia wananchi na nidhamu ya mtu kabla ya kumpa ridhaa ya kupeperusha bendera ya Chama.
Kwa mujibu wa Maganya, moja ya mambo yaliyomjengea imani kwa Emmanuela ni msimamo wake katika kusimamia maamuzi ya serikali bila kuyumbishwa na shinikizo la watu mbalimbali.
Alisimulia tukio lililotokea katika msiba wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Zerothe Steven, baadhi ya watu walitaka kuvuruga utaratibu wa serikali ila Emmanuela akiwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru alisimama kidete kuhakikisha taratibu zinafuatwa.
“Alisema wazi mimi ndiye Mkuu wa Wilaya na mwakilishi wa Rais katika wilaya hii, utaratibu utakuwa huu. Akafunga mjadala kabisa. Huyo ndiye Emmanuela mnayetakiwa kumchagua,” alisema Maganya.
Kauli hiyo ilizua shangwe kubwa kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo huku baadhi yao wakisema wanahitaji kiongozi mwenye uthubutu wa kusimamia sheria, taratibu na maslahi ya wananchi bila kuyumbishwa.
Mbali na msimamo wake, viongozi wa CCM wamekuwa wakimuelezea Emmanuela kama kiongozi mwenye utulivu, usikivu na uwezo wa kushirikiana na wananchi kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.
Pia, katika kampeni hizo, CCM imekuwa ikirejea mara kwa mara mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 30 ya uongozi wa hayati Lukuvi katika Jimbo la Ismani.
Viongozi wa Chama wanaeleza maendeleo ya miundombinu ya barabara, sekta ya afya, elimu na maji ni ushahidi wa namna CCM ilivyoendelea kusimamia maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.
MGOMBEA UBUNGE ISMANI
Kwa upande wake, Mgombea Emmanuela alisema anaingia katika uchaguzi huo akiwa na dhamira ya kuendeleza yale yaliyoanzishwa na viongozi waliomtangulia huku akiahidi kuongeza nguvu mpya kusimamia maendeleo ya wananchi.
“CCM ndiyo kinapika viongozi na mimi nimeiva. Nimepewa dhamana hii kwa sababu Chama kinaamini nina uwezo wa kuwatumikia wananchi wa Ismani,” alisema.
Alisema uzoefu alioupata ndani ya Chama na serikalini unampa uwezo wa kuelewa changamoto za wananchi na namna ya kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na serikali.
Aliwahakikishia wananchi kuwa, ana uwezo, nguvu na nia ya dhati ya kuwatumikia huku akiwaomba kujitokeza kwa wingi Julai Mosi, mwaka huu kumpigia kura yeye na wagombea wengine wa CCM kuendelea kuharakisha maendeleo katika jimbo hilo.
Kwa mujibu wa Emmanuela, ushindi wa CCM katika nafasi za ubunge na udiwani utarahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwa viongozi watakuwa wakifanya kazi kwa mshikamano mmoja katika kuwatumikia wananchi.
Katika kampeni zake, mgombea huyo amekuwa akitoa wito kwa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wafanyabiashara, wakulima, vijana na wanawake kuendelea kuiamini CCM kwa madai kuwa, ndiyo Chama kilicho karibu na wananchi kutatua changamoto zao za kila siku.
Aliwapongeza vijana wa bodaboda aliowaita “maofisa wa usafirishaji” kwa mchango wao mkubwa wa kukuza uchumi wa wananchi na kuwaunganisha watu katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Pamoja na ushindani wa kisiasa unaoendelea, viongozi wa CCM wameendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kuhakikisha Chama kinapata ushindi mkubwa utakaoendeleza kasi ya maendeleo Ismani.
Kwa upande mwingine, wachambuzi wa siasa, walieleza kuwa uchaguzi wa Ismani umegeuka kuwa, kipimo cha vyama vya siasa vinavyoweza kushawishi wananchi kupitia hoja za maendeleo, uzoefu wa viongozi na uwezo wao wa kusimamia mahitaji ya wananchi.
Mchambuzi wa Siasa, Abduly Kambaya, alisema CCM ni Chama pekee chenye ushawishi kwa wananchi kutokana na kuwa na ilani ya uchaguzi inayotekelezeka kwa vitendo.
Kwa CCM, kampeni hizo zimejikita zaidi kuonesha mwendelezo wa maendeleo, uzoefu wa uongozi na umuhimu wa kuwa na viongozi wanaofahamu mifumo ya serikali na namna ya kushughulikia changamoto za wananchi kwa karibu zaidi.
Kadri Julai Mosi inavyokaribia, mvuto wa kisiasa ndani ya Jimbo la Ismani unaendelea kuongezeka huku wananchi wakisubiri kufanya uamuzi wao kuhusu nani anayefaa kupewa jukumu la kuongoza jimbo hilo katika hatua nyingine ya maendeleo.




