Dodoma
Na SELINA MATHEW
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amesema dhahabu inayonunuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) haijauzwa na itaendelea kuhifadhiwa kama sehemu ya sera za kifedha za taifa.
Amesema akiba hiyo imechangia kuimarisha uchumi wa nchi na kuifanya Tanzania kuhimili misukosuko ya uchumi duniani.
Akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko aliyetaka kufahamu kauli ya serikali kuhusu taarifa zinazosambazwa kwamba dhahabu inayonunuliwa na Benki Kuu ya Tanzania imeuzwa, Dk. Mwigulu alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zinazohifadhi akiba kwa fedha za kigeni na dhahabu inayohifadhiwa haijauzwa.
“Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya uchumi wa dunia yaliyoshuhudiwa katika miaka ya karibuni. Serikali ikafikia uamuzi wa kuanza kununua dhahabu,” alisema.
Alisema hadi sasa Tanzania ina takribani tani 27 za dhahabu zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.9, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 45 ya akiba yote ya fedha za kigeni, huku jumla ya akiba ya taifa ikifikia zaidi ya dola bilioni sita, kiwango kinachotosheleza zaidi ya miezi minne ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Dk. Mwigulu alisema dhahabu hiyo haihifadhiwi kwa ajili ya biashara, bali ni sehemu ya zana za sera za kifedha zinazotumika kuimarisha uchumi na kuifanya shilingi ya Tanzania kuwa imara, sawa na namna ambavyo akiba ya dola za Marekani hutumika na benki kuu mbalimbali duniani.
Alisema kumekuwapo na mawazo ya kuuza sehemu ya dhahabu wakati bei ilipokuwa juu, lakini kutokana na kushuka kwa bei kufuatia migogoro ya kimataifa, Benki Kuu ya Tanzania iliona isingekuwa busara kufanya hivyo.
“Mpaka sasa hakuna dhahabu iliyouzwa. Haya ni masuala ya sera za kifedha na mifumo yake inasimamiwa kwa uwazi kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa ikiwemo IMF na Benki ya Dunia. Haiwezekani mtu binafsi akauza dhahabu ya taifa,” alisema.
HAKUNA MGOGORO WA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA KATI YA ZANZIBAR NA TANZANIA BARA
Aidha, Waziri Mkuu alisema hakuna mgogoro wowote wa utoaji wa huduma za afya kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, akisisitiza kuwa Muungano wa Tanzania umejengwa katika msingi wa undugu na ushirikiano unaowawezesha wananchi wa pande zote mbili kupata huduma bila ubaguzi.
Akijibu swali la Mbunge wa Segerea (CHAUMMA), Agnesta Lambert, aliyetaka kufahamu utaratibu wa kisera na kisheria unaotumika kuwahudumia Watanzania wa pande zote mbili katika masuala yasiyo ya Muungano hususan huduma za afya, Dk. Mwigulu alisema pamoja na kuwapo kwa masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano, sekta mbalimbali zimeendelea kushirikiana kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu bila vikwazo.
Alisema mifuko ya bima ya afya ya NHIF na ZHIF imeweka utaratibu unaowaruhusu wananchi wa pande zote kutumia bima zao katika hospitali zinazotambuliwa, hivyo Mzanzibari mwenye kadi ya ZHIF anaweza kutibiwa Tanzania Bara na Mtanzania Bara mwenye kadi ya NHIF anaweza kupata huduma Zanzibar.
Dk. Mwigulu alisema changamoto zinazojitokeza mara chache zinatokana na baadhi ya watu kutoka n je ya nchi wanaojaribu kutumia mianya mbalimbali kujinufaisha kwa huduma zinazotolewa kwa wananchi na kwamba jambo hilo linahitaji ushirikiano wa taasisi husika badala ya kulichukulia kama suala la mgawanyiko wa Muungano.
“Muungano wetu si wa karatasi pekee, umeunganisha damu na undugu. Hatuna tatizo la kimahusiano katika matumizi ya rasilimali na utoaji wa huduma, tunachotakiwa ni kuendelea kuimarisha mifumo yetu,” alisema.
ATOA MAAGIZO KWA WAKUU WA MIKOA NCHINI
Kuhusu upatikanaji wa maji, Dk. Mwigulu alisema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika ununuzi wa mitambo ya kuchimba visima kwa kila mkoa, sanjari na mitambo ya kutambua maeneo yenye maji na ile ya kuchimba mabwawa, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya uhaba wa maji nchini.
Akijibu swali la Mbunge wa Kwimba, Cosmas Mutesigwa, aliyetaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu ufanisi wa mitambo ya kuchimba visima iliyosambazwa mikoani baada ya baadhi yake kuonekana kuegeshwa huku mahitaji ya maji vijijini yakiwa makubwa, Waziri Mkuu alisema baadhi ya miradi ilichelewa kutokana na changamoto za vipuri na vifaa vya kukamilisha visima baada ya uchimbaji na kuwataka wakuu wa mikoa kusimama mitambo hiyo.
Alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alinunua mitambo ya uchimbaji wa visima, hivyo watendaji wachukue hatua na waache kufanya kazi kwa mazoea.
“Nielekeze Wakuu wa Mikoa yote pamoja na wizara, kusimamia ili mitambo ile iweze kufanya kazi iliyokusudiwa, ni kweli kuna baadhi ya maeneo ya tunaendelea endelea na ile tabia ya ‘business as usual’, sasa ili kufikia matokeo ya Dira 2050, ni lazima tufanye kazi ‘business as unusual’, tuache kufanya kazi kwa kuchukulia vitu kimazoea mazoea”, alielekeza Waziri Mkuu.
Alisema maboresho ya mfumo wa Mfuko wa Maji yatawezesha fedha kupelekwa moja kwa moja kwenye mfuko huo, kununua vifaa vya kukamilisha miradi na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alisema Serikali haitavumilia utendaji wa mazoea unaochelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi, huku akiwaagiza wakuu wa mikoa pamoja na Wizara ya Maji kuhakikisha mitambo hiyo inafanya kazi kwa ufanisi uliokusudiwa.
Waziri Mkuu pia alisema Serikali itaendelea kuimarisha ustawi wa watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha sheria, sera na miongozo iliyowekwa inatekelezwa kikamilifu ili kuwawezesha kupata fursa sawa katika sekta mbalimbali.
Dk. Mwigulu alisema Serikali imeweka utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya watu wenye ulemavu katika halmashauri na kuhakikisha asilimia 30 ya zabuni zinazotolewa zinawanufaisha makundi maalumu ikiwemo watu wenye ulemavu.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Aisha Mduya, aliyetaka kujua namna Serikali ilivyojipanga kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa katika afya, elimu, ajira na shughuli za kiuchumi pamoja na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010.
Akifafanua alisema Serikali imeendelea kusisitiza ujenzi wa miundombinu rafiki na utoaji wa fursa sawa katika sekta za afya, elimu na ajira, huku akitoa rai kwa watumishi wa umma na jamii kwa ujumla kuendelea kuwa karibu na watu wenye mahitaji maalumu.
Kadhalika, Dk. Mwigulu alisema Serikali imekamilisha mchakato wa kisheria na uhakiki wa wapiganaji waliojitolea wakati wa Vita vya Kagera mwaka 1979 na kwamba kuanzia mwaka wa fedha unaoanza sasa wataanza kulipwa mafao yao.
Akijibu swali la Mbunge wa Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika, aliyetaka kujua ni lini wapiganaji waliojitolea wakati wa Vita vya Kagera na kuahidiwa kifuta jasho baada ya ushindi huo wataanza kulipwa, Dk. Mwigulu alisema tangazo la Serikali la Juni 2025 lilitambua rasmi wapiganaji hao baada ya kufanyika marekebisho ya sheria, huku uhakiki ukiwa umebaini kuwapo kwa takribani wapiganaji 7,200 wanaostahili kulipwa.
Hivyo, alisema maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu suala hilo yamefanyiwa kazi na sasa hakuna kikwazo cha kisheria wala cha kiutawala kinachozuia kuanza kwa malipo hayo katika mwaka mpya wa fedha.




