Na ATHNATH MKIRAMWENI
WADAU wa sekta ya afya wameitaka Tanzania kuongeza uwekezaji katika huduma za kinga na kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi na uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya sasa na ya baadaye kwa kujenga mfumo wa afya wenye tija endelevu mwaka 2050.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kongamano la Tatu la Rasilimali Watu Sekta ya Afya, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya alisema pamoja na kuimarisha huduma za kinga ni muhimu mfumo wa utumishi utoe nafasi kwa wataalamu wenye elimu ya juu kuitumia taaluma yao kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Amesema mafanikio ya sekta ya afya hayatategemea tu uwekezaji katika miundombinu na vifaa, bali uwezo wa kuandaa viongozi wa baadaye watakaosimamia maendeleo ya sekta hiyo kwa ufanisi.
“Kujenga viongozi wa baadaye kunaanza na ulezi na uongozi elekezi. Vijana wanapaswa kuaminiwa, kupewa fursa za kuonyesha uwezo wao na kuwezeshwa kwa rasilimali na mifumo ya uwajibikaji wawe nguzo ya mustakabali wa sekta ya afya,” amesema Dk. Mpoki.
Amesisitiza kuwa kuwekeza katika kinga, kutumia ipasavyo wataalamu wenye elimu ya juu na kuimarisha programu elekezi kwa vijana ni mikakati muhimu itakayoiwezesha Tanzania kuwa na rasilimali watu imara na mfumo wa afya unaokidhi mahitaji ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benjamin Mkapa Foundation (BMF), Dk.Ellen Mkondya alisema sekta ya afya inapaswa kuanza kuandaa rasilimali watu watakaokidhi mahitaji ya Tanzania ya baadaye kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia, ongezeko la watu na mabadiliko ya magonjwa, badala ya kuendelea kuangalia mahitaji ya sasa pekee.
Amesema kongamano hilo linaangalia aina ya wataalamu watakaohitajika kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2050, ikiwemo wataalamu wa akili bandia (AI), uchambuzi wa takwimu, huduma kwa wazee na matumizi ya teknolojia za kidijitali pamoja na telemedicine.
Amesema kongamano hilo limeweka mkazo kwa vijana kuwa hawapaswi kuonekana kama viongozi wa baadaye bali ni viongozi wa sasa wanaohitaji kuandaliwa kupitia programu za ulezi na uongozi elekezi.
Dk. Ellen amesema zaidi ya nusu ya wananchi wa Tanzania ni vijana, hivyo ni muhimu kuwawezesha, kuwajengea uwezo wa uongozi na kuwasaidia kukabiliana na changamoto ikiwemo afya ya akili waweze kuendelea kutoa huduma bora za afya.
Pia, amesema vyuo huzalisha zaidi ya wataalamu 25,000 wa afya kila mwaka huku Serikali ikiwa mwajiri mkuu, hali inayofanya isiwezekane kuwaajiri wote kwa wakati mmoja.
Naye, Dk. Julieth Tibyesiga kutoka Hospitali ya wilaya Namtumbo ameiomba serikali kuandaa mkakati wa kitaifa unaowahusu vijana wataalamu wa afya utakaoweka mazingira bora ya maendeleo yao, motisha na fursa za ukuaji wa taaluma kujenga nguvu kazi yenye uzalendo na kujituma katika kuimarisha mfumo wa afya nchini.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani(WHO) nchini, Dk. Alex Gasasira amesema Tanzania ina uongozi imara kuanzia viongozi wa serikali hadi wataalamu wa afya, jambo linalotoa msingi mzuri wa kutekeleza mawazo mapya yanayotokana na vijana.




