NA MUSSAYUSUPH
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameyataja mambo manne yaliyoiwezesha Tanzania kupiga hatua katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto huku akisisitiza Afrika inahitaji mageuzi katika sekta ya afya ili kuhakikisha usalama wa afya ya mama na mtoto.
Dk. Samia ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) katika masuala ya afya ya mama na mtoto, amesema baada ya kupewa kijiti hicho atahakikisha Afrika inafanya mageuzi ya kidigitali na kutilia mkazo nchi wanachama kuongeza uwezeshaji kifedha wa ndani katika sekta hiyo.
Rais Dk. Samia aliyasema hayo alipohojiwa nje ya mkutano uliowakutanisha viongozi wa mataifa ya Afrika, jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, ambapo alisema nchi za Afrika zinapaswa kuweka kipaumbele eneo la afya.
“Naishukuru AU kwa jukumu hilo kuipa Tanzania. Nimelipokea kwa unyenyekevu jukumu hili kwani ni sehemu ya kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kulinda maisha ya kinamama. Tutakuwa na jukumu la kuiunganisha Afrika katika masuala ya afya.
Alisisitiza: “Tutaendelea kutilia mkazo kwa kinamama, watoto na vijana ambao ndiyo kizazi kijacho na sasa tunawekeza vya kutosha kwa ajili yao. Wategemee mfumo wa mageuzi katika sekta ya afya kwa sababu bila mageuzi katika sekta ya afya hatutaweza kufika mahali ambako tunataka kufika.”
ATAJA VIPAUMBELE
Rais Dk. Samia alisema baada ya kupewa nafasi hiyo, jitihada zake zitajikita kuleta mageuzi kupitia uwezeshaji wa ndani kifedha kwani nchi za Afrika zinapaswa kuweka kipaumbele masuala ya afya kwa manufaa ya kizazi kijacho.
“Eneo la pili ni kushirikiana na jamii katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi. Eneo lingine ni mageuzi ya kidigitali kwani tumeshafanya mageuzi katika sekta ya miundombinu, ujenzi wa hospitali, uwekezaji katika vifaa tiba muhimu.
Alisisitiza: “Lakini sasa tunapaswa kufanya mageuzi ya kidigitali kuanzia ngazi ya vijiji hadi kitaifa katika kuhakikisha tunapata taarifa muhimu.”
SIRI MAFANIKIO YA TANZANIA
Alizitaja sababu ziliizofanya Tanzania kupiga hatua katika sekta ya afya ni uwekezaji uliofanyika katika miundombinu ya afya, ushiriki wa sekta binafsi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali katika utoaji huduma za afya na urahisi katika upatikanaji rufaa kwa wajawazito kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa hadi hospitali za rufaa kupitia mfumo wa M – Mama.
Alisema mfumo huo unamwezesha mjamzito pindi anapopata uchungu kuita gari ambalo litakuwa na muuguzi ambaye naye atakuwa akitoa taarifa kuhusu afya ya mjamzito wakati akiwa njiani kwenda kupata huduma.
“Eneo lingine ni uboreshaji miundombinu ya barabara katika maeneo ya vijijini ambazo zimewezesha urahisi kusafirisha wagonjwa kwenda kupata huduma za afya. Suala lingine ni lishe kwa wajawazito na watoto.
“Pia, tumeongeza idadi ya watoa huduma za afya ngazi ya jamii hadi vijijini ambao wamewezesha hakuna mjamzito ambaye hafikiwi na huduma za afya.”




