Na MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kilichotokea Februari 19, 2026 jijini Dar es Salaam.
Kupitia salamu zake za rambirambi, CCM kimeeleza kuwa kinatambua na kuthamini mchango mkubwa wa kiongozi huyo wa kiroho katika kulihudumia Kanisa Katoliki na Taifa la Tanzania kwa ujumla.
Chama hicho kimesisitiza kuwa katika kipindi chote cha utumishi wake, Kadinali Pengo alijitokeza kama kiongozi mwenye busara, maadili mema na moyo wa kujitoa kwa ustawi wa jamii.
Katika miaka 55 ya upadre, miaka 43 ya uaskofu na miaka 28 ya hadhi ya Ukadinali, marehemu aliweka alama ya uongozi uliotawaliwa na unyenyekevu, mshikamano wa kijamii na kuhimiza amani na maadili mema katika jamii.
CCM kimeeleza kuwa katika kipindi hiki cha maombolezo, kinaungana na Kanisa Katoliki Tanzania, familia ya marehemu, waumini pamoja na Watanzania wote kuomboleza msiba huo mkubwa wa kuondokewa na kiongozi mahiri wa kiroho.
Chama hicho kimetoa pole kwa wote walioguswa na msiba huo na kuwataka Watanzania kuendeleza misingi ya maadili, upendo na mshikamano aliyoyaenzi marehemu wakati wa uhai wake.





