Na FRED ALFRED, Dodoma
TATIZO la upungufu wa nguvu za kiume ni changamoto inayowakumba wanaume wengi duniani hali ambayo imewaathiri kisaikolojia na mahusiano ya kifamilia.
Ingawa watu wengi hulichukulia tatizo hilo kama jambo la aibu, wataalamu wa afya wanasema ni tatizo la kitabibu linaloweza kutibiwa kwa njia mbalimbali, kulingana na chanzo chake.
Nchini, tatizo hilo sasa limepata ufumbuzi baada ya Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) iliyopo jijini hapa kuanzisha huduma ya upandikizaji uume ambayo imetajwa kuwa mkombozi kwa wanaume wenye changamoto ya ukosefu wa nguvu za kiume.
Akihojiwa na UHURU, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo katika hospitali hiyo, Dk. Remigius Rugakingira, alisema upandikizaji uume ni upasuaji wa kitaalamu unaohusisha kupandikiza kifaa maalumu ndani ya uume kumwezesha mwanaume kusimamisha uume kumwezesha kushiriki tendo la ndoa.
“Kuna aina mbili kuu za vifaa vinavyopandikizwa. Aina ya kwanza ni kifaa kigumu kinachoweza kuelekezwa juu au chini kulingana na matumizi.
“Aina ya pili ni kifaa kinachoweza kupulizwa, ambacho hutumia pampu ndogo iliyowekwa kwenye korodani, kisha kujaza maji ndani ya kifaa hicho na kufanya uume usimame wakati wa tendo la ndoa. Baada ya matumizi, kifaa hurudishwa katika hali yake ya kawaida.
Aliongeza: “Tunapendekeza matibabu haya kwa wanaume wenye tatizo sugu la kushindwa kusimama kwa uume ambao hawajapata mafanikio kwa kutumia dawa au njia nyingine za matibabu.”
Alieleza kuwa, wakati mwingine upandikizaji huo unaweza kufanywa kwa wagonjwa wenye matatizo ya uume yaliyosababishwa na majeraha makubwa au magonjwa yanayoathiri uwezo wa uume kusimama.
FAIDA ZA UPANDIKIZAJI UUME
Dk. Rugakingira, alisema faida kubwa ya upandikizaji uume ni kurejesha uwezo wa kushiriki tendo la ndoa na kuongeza kujiamini kwa mwanaume.
Alisema tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa, wanaume wengi wanaofanyiwa upasuaji huo, huridhishwa na matokeo yake hasa wanapopewa ushauri wa kutosha kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kufahamu upandikizaji uume siyo njia ya kuongeza ukubwa wa uume kwa madhumuni ya urembo wala hauongezi hamu ya kufanya mapenzi.
“Lengo lake kuu ni kumsaidia mwanaume mwenye tatizo la kitabibu kurejesha uwezo wa kusimama kwa uume ili kuboresha maisha yake ya ndoa na afya kwa ujumla,” alisema.
VIJANA WAJITOKEZA KWA WINGI
Dk. Rugakingira, alisema idadi ya wanaume wanaokabiliwa na changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume inaongezeka siku hadi siku.
Alisema wanaojitokeza kutafuta huduma hiyo ni vijana wenye umri wa miaka 22 hadi 23 na wanaume wenye umri wa miaka 55 hadi 56, jambo linaloonyesha kuwa tatizo hilo halichagui umri.
Alifafanua kuwa tangu Hospitali ya Benjamin Mkapa ilipoanza kutoa huduma hiyo na kuonesha mafanikio, watu wengi wamekuwa wakijitokeza kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Kwa mujibu wa Dk. Rugakingira, hadi sasa wagonjwa wawili wamekidhi vigezo vya kuingia katika hatua ya kufanyiwa upandikizaji wa uume.
“Wanaojitokeza kutafuta huduma hiyo ni vijana wenye umri wa miaka 22 hadi 23 pamoja na wanaume wenye umri wa miaka 55 hadi 56. Hii inaonesha kuwa, tatizo hilo ni kubwa katika jamii na halichagui umri,” alisema.
MATUMIZI YA DAWA ZA ASILI
Dk. Rugakingira alisema baadhi ya virutubisho vinaweza kusaidia mwili kufanya kazi vizuri, lakini baadhi ya watu wamegeuza suala hilo kuwa biashara.
Alieleza kuwa asilimia kubwa ya wanaume wanaofika hospitalini wakiwa na tatizo la kushindwa kusimama kwa uume, tayari walikuwa wametumia dawa za miti shamba na dawa zinazodaiwa kuongeza nguvu za kiume.
“Ni muhimu jamii itambue kuwa, siyo kila dawa inayodaiwa kutibu tatizo hilo ni salama au sahihi. Wananchi wanapaswa kufika katika vituo vya afya ili kupata uchunguzi na tiba stahiki,” alisema.
GHARAMA ZA UPANDIKIZAJI
Akizungumzia gharama za matibabu hayo, Dk. Rugakingira alisema sh. milioni 10 zinazotumika kwa huduma ya upandikizaji uume, siyo kiasi kikubwa cha fedha ukilinganisha na manufaa ya muda mrefu anayopata mgonjwa, kwani upasuaji huo hufanyika mara moja na husaidia kuondoa tatizo kwa kipindi kirefu.
Alisema hali hiyo ni tofauti na magonjwa sugu kama kisukari na shinikizo la damu, ambayo humlazimu mgonjwa kutumia dawa na kugharamia matibabu katika maisha yake yote.
Aliwataka wananchi wasiogope gharama za matibabu hayo, akisisitiza kuwa ni uwekezaji wa afya wa muda mrefu unaoweza kurejesha ubora wa maisha, kuimarisha ndoa na kuongeza hali ya kujiamini kwa wagonjwa wanaostahili kufanyiwa upasuaji huo.
Pia, alisisitiza kuwa uchunguzi wa kitaalamu ndiyo msingi wa kupata tiba salama na yenye mafanikio.
WANAUME 14 WAREJESHEWA MATUMAINI
Hospitali ya Benjamin Mkapa, imekuwa ikitoa huduma hiyo tangu mwaka 2023, ikiwa ni miongoni mwa huduma zaidi ya 20 za kibingwa na kibingwa bobezi zinazotolewa hospitalini hapo.
Huduma hiyo ilianzishwa baada ya kubaini kuwepo changamoto kubwa miongoni mwa wanaume wengi, hali iliyowafanya baadhi yao kutafuta suluhisho kupitia waganga wa kienyeji na dawa zinazodaiwa kutibu tatizo hilo.
Kwa mujibu wa takwimu za hospitali hiyo, wanaume 14 wamefanyiwa upandikizaji wa uume ambapo wameeleza kuanza kushiriki tendo la ndoa kwa ufanisi baada ya wiki sita tangu kufanyiwa upasuaji.
“Kinachofanyika si kupandikiza uume bandia, bali ni kupandikiza kifaa maalumu kinachosaidia kurejesha uwezo wa uume kusimama. Baada ya upasuaji, mgonjwa hurudi katika hali yake ya kawaida, na kifaa hicho hudumu kwa muda mrefu,” alieleza daktari hiyo.
KAULI YA WATAALAMU TIBA ZA ASILI
Mtaalamu wa tiba asili mkoani hapa, Boniface Kipanta, alisema changamoto ya wanaume kukosa nguvu za kiume imekuwa ikiongezeka kwa sababu mbalimbali.
Alizitaja sababu hizo ni magonjwa sugu, msongo wa mawazo, mtindo wa maisha usiozingatia afya pamoja na matumizi holela ya dawa na bidhaa zinazodaiwa kuongeza nguvu za kiume.
Alisema tiba asili inaweza kuwa na nafasi katika kuwasaidia baadhi ya wagonjwa, lakini inapaswa kutolewa na wataalamu wenye ujuzi kwa kuzingatia uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha tatizo.
Alionya kuwa matumizi ya dawa zisizojulikana au zinazouzwa bila uthibitisho wa kitaalamu yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya.
Kipanta alisema baadhi ya watu huchelewa kupatiwa matibabu kwa sababu ya kuamini taarifa zisizo sahihi au kuhofia unyanyapaa, jambo linaloongeza ukubwa wa tatizo na kufanya matibabu kuwa magumu zaidi.
Aliwataka wanaume wanaokabiliwa na changamoto hiyo kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi, kula lishe bora, kupunguza matumizi ya pombe, kuacha kuvuta sigara, kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kupata matokeo bora ya matibabu.
“Tiba asili ina nafasi yake katika kusaidia afya ya uzazi wa mwanaume, lakini ni muhimu wananchi waepuke kutumia dawa zisizojulikana. Kila mwanaume anayepata changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume anapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini chanzo cha tatizo na kupata tiba inayofaa,” alisema Kipanta.
VIONGOZI WA DINI WATOA MSIMAMO
Askofu Mkuu wa Kanisa la Karmeli Assemblies of God (KAG), Dk. Evance Chande, alisema changamoto ya wanaume kukosa nguvu za kiume imekuwa ikiongezeka katika jamii na kuathiri uimara wa ndoa pamoja na taasisi za familia.
Alisema tendo la ndoa ni miongoni mwa misingi muhimu inayowaunganisha wanandoa, hivyo mwanaume anapopoteza uwezo wa kushiriki tendo hilo kwa muda mrefu bila kutafuta suluhisho, ndoa inaweza kukumbwa na migogoro mikubwa.
Dk.Chande alisema aliwahi kupokea kesi ya aina hiyo kanisani kwake, jambo lililompa nafasi ya kushuhudia athari zinazoweza kujitokeza ndani ya familia kutokana na changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa Askofu huyo, mabadiliko ya mtindo wa maisha ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia kuongezeka kwa tatizo hilo.
Alisema baadhi ya vijana wamejenga mazoea ya kula vyakula vya haraka kama chipsi na kupuuza vyakula vya asili vyenye virutubisho muhimu kwa afya ya mwili.
Alibainisha kuwa vizazi vya zamani vilikuwa na mtindo tofauti wa maisha, vikijikita katika lishe ya asili na shughuli za kila siku zilizochangia afya njema na uwezo bora wa kujenga familia.
“Tendo la ndoa ni sehemu muhimu ya maisha ya ndoa. Mume na mke wanapoishi pamoja kama ndugu kwa sababu ya kushindwa kushiriki tendo la ndoa, hiyo ni changamoto inayohitaji kutafutiwa suluhisho. Nimewahi kupokea kesi moja ya namna hiyo kanisani kwangu,” alisema Dk. Chande.
Aliongeza kuwa mabadiliko ya mtindo wa maisha na ulaji wa vyakula visivyo sahihi vinaweza kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia tatizo hilo, hivyo wataalamu wanapaswa kuendelea kufanya tafiti ili kubaini sababu zake na namna bora ya kulikabili.
Aidha, aliwataka wanandoa wanaokabiliwa na changamoto hiyo kutafuta ushauri wa kitaalamu mapema na kuepuka kuficha tatizo, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kulinda ndoa na kuimarisha ustawi wa familia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Maimamu na Walimu wa Madrasa Tanzania (UMMATA) Mkoa wa Dodoma, Sheikh Omar Salimu Itara, alisema amekuwa akipokea kesi nyingi zinazohusu wanaume kushindwa kushiriki tendo la ndoa kutokana na changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume.
Alisema kuwa kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, hatua wanayoichukua kwa mtu mwenye changamoto hiyo ni kumpa muda wa mwaka mmoja wa uangalizi pamoja na kumtafutia matibabu.
“Endapo ndani ya mwaka huo mmoja tatizo halitapatiwa ufumbuzi kabisa, basi tunaivunja ndoa hiyo kwa sababu itakuwa imepoteza uhalali wake,” alisema Sheikh Itara.
MWANASAIKOLOJIA AELEZA
Mwanasaikolojia wa masuala ya afya ya akili, Janeth Urio, alisema suala la wanaume kukosa nguvu za kiume wakati mwingine linasababishwa na msongo wa mawazo.
“Siyo kila mwanaume mwenye tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume atakuwa na shida ya kiafya. Wakati mwingine ni suala la msongo wa mawazo hasa kutokana na changamoto za maisha. Mtu akiwa na changamoto za kimaisha ni vigumu hata kutenda tendo la ndoa kwa ufanisi,” alieleza.
Alisema ni muhimu pindi mwanaume akijikuta katika hali hiyo akapate ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya ambao baada ya uchunguzi watabaini kiini cha tatizo badala ya kuanza kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo baadaye zinaweza kumsababishia tatizo kubwa zaidi.
WANANCHI WAFUNGUKA
Katika kufanya utafiti kuhusu changamoto ya kushindwa kushiriki tendo la ndoa na namna matibabu ya kisasa yanavyoweza kusaidia, baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma walitoa maoni yao kuhusu hali hiyo.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Chamwino B, Stella Saimon, alisema changamoto ya nguvu za kiume haziathiri wanaume pekee, bali pia huathiri mahusiano ya kifamilia na ustawi wa ndoa.
Alisisitiza umuhimu wa wanandoa kuzungumza kwa uwazi kuhusu changamoto hizo na kushirikiana kutafuta ushauri wa kitaalamu badala ya kulaumiana au kuficha tatizo.
“Jamii inapaswa kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wenye matatizo ya afya ya uzazi ili kuwapa nafasi ya kutafuta matibabu bila hofu au aibu,” alisema.
Mkazi wa Kata ya Makulu, Joseph Jilatu, alisema tatizo la kushindwa kushiriki tendo la ndoa limekuwa likiwasumbua wanaume wengi.
“Lakini wengi wao huogopa kwenda hospitalini kutokana na kuhofia unyanyapaa na hivyo kuishia kutumia dawa za kienyeji ambazo mara nyingi hazijathibitishwa kitaalamu,” alisisitiza.
Alisema elimu zaidi inapaswa kutolewa kwa jamii ili wanaume watambue kuwa tatizo hilo linaweza kutibiwa na kwamba kutafuta huduma za afya mapema huongeza uwezekano wa kupata matokeo mazuri.
Kwa upande wake, mkazi wa Swaswa, Benedict Mwakalindile, alisema huduma za kibingwa zinazotolewa nchini ni hatua muhimu kwa kuwa zinawapunguzia wananchi gharama za kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.
“Pamoja na gharama za matibabu kuonekana kuwa kubwa kwa baadhi ya watu, ni muhimu wananchi wakazingatia thamani ya afya na matokeo ya muda mrefu yanayoweza kupatikana kupitia huduma hiyo,” alisema.




