Na EMMANUEL MOHAMED
BAADHI ya wanasiasa na wasomi nchini, wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kudumishwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kupendekeza lianzishwe somo maalumu la muungano katika mitaala ya shule, kuwajengea vijana uelewa mpana kuhusu historia, misingi na faida zake.
Mapendekezo hayo yanatokana na kuwepo baadhi ya taarifa katika mitandao ya kijamii zenye lengo la kupotosha umma juu ya masuala ya Muungano.
Akizungumza na UHURU hili, mwanasiasa mkongwe nchini, Anna Abdallah, alisema kuna haja kuanzishwa somo maalumu la Muungano shuleni, hatua ambayo itasaidia vijana kupata maarifa sahihi kuhusu namna ulivyoanzishwa, mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo pamoja na wajibu wa kila Mtanzania katika kuulinda na kuendeleza.
“Ninafikiri tunapaswa kufundisha vizuri masuala ya Muungano kuanzia ngazi ya shule, kwani waliozaliwa baada ya muungano ni wengi ukilinganisha na sisi ambao tumeuona kwa hiyo lazima tuwafundishe kuepuka upotoshaji,” alisema.
Aliongeza: “Lazima tuwafundishe vijana wanatakiwa waelewe Muungano wetu ni wa kipekee ukilinganisha na wa nchi nyingine.”
Anna Abdallah alisema shule ni sehemu muhimu ya kujenga uelewa wa awali kwa kuwa ndiyo mahali ambako hupata maarifa yanayowaandaa kuwa raia wenye uwezo wa kuchambua kwa kina masuala mengi ya kitaifa.
“Kama tunataka vijana wawe na uelewa sahihi kuhusu Muungano, elimu hiyo inapaswa kuanza mapema, somo la Muungano litawasaidia kuelewa historia ya nchi yao na kutofautisha ukweli na taarifa zisizo sahihi,” alisema.
NGEMELA LUBINGA
Aidha, aliyekuwa Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, alisema kuna haja Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuliweka somo la Muungano katika mitaala ya elimu nchini.
“Tuiombe Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuandaa mtaala kuwafundisha vijana wetu kuanzia ngazi ya chini hadi elimu ya juu.
“Upotoshwaji wa taarifa inatokana na elimu ya Muungano kuwa haifundishwa kwa umakini na walimu wa historia na elimu ya siasa ama kwa maneno mengine elimu ya uraia,” alisema.
Lubinga alisema upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu unatokana na uelewa mdogo kuhusu Muungano kwa kundi la vijana, hivyo kuna haja somo hilo kuwekwa katika mitaala ya elimu.
“Somo hilo linaweza kuwasaidia vijana kufahamu kwa kina mazingira yaliyosababisha kuundwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, viongozi waliohusika, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha zaidi ya miaka 60 ya muungano,” aliongeza Lubinga.
JUMA ALLY KHATIB
Mwenyekiti wa ADA-TADEA, Juma Ally Khatib, alisema katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano, vijana wanakutana na taarifa nyingi kutoka vyanzo mbalimbali, ambapo kuna haja ya kuwajengea ujuzi wa kuzichambua kabla ya kuziamini au kuzisambaza.
“Elimu ya uraia inapaswa kuimarishwa kwa kujumuisha mafunzo yanayomjengea kijana uwezo wa kufikiri kwa kina, kuuliza maswali muhimu, kutafuta vyanzo vinavyoaminika na kutofautisha kati ya ukweli, maoni na taarifa za kupotosha.
Kizazi cha sasa kinatakiwa kuwa na uwezo wa kufanya uamuzi kwa kuzingatia ushahidi na taarifa sahihi, badala ya kuongozwa na hisia au taarifa zinazosambazwa bila uthibitisho,” alisema.
DK. AJALI NGUYAHAMBI
Mhadhiri na Mtafiti wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Ajali Nguyahambi, alisema kazi inayotakiwa kufanyika kwa vijana ni kupewa uwezo wa kuchuja mambo kitaalamu.
“Mbali na hilo, pia tunatakiwa kuwapa elimu ya kutosha kuhusu Muungano wenyewe wanapopewa maarifa tofauti wajue hiki ni tofauti na wanachokifahamu, jambo lingine ni kuwaelimisha umuhimu wa Muungano, nafikiri mambo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Dk. Nguyahambi alisema kuna haja elimu ya uraia kuboreshwa kutokana na kuwa ni nyenzo muhimu katika kujenga kizazi chenye uwezo wa kuchambua taarifa na kutofautisha ukweli na upotoshwaji.
“Elimu ya uraia inapaswa kwenda zaidi ya kufundisha haki na wajibu wa raia, bali pia ijikite katika kujenga fikra makini, uelewa wa masuala ya kitaifa na historia ya taifa,”alisema.
HISTORIA YA MUUNGANO
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliasisiwa Aprili 26, 1964, chini ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Mkataba wa Muungano huo ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Karume, Aprili 22, 1964 visiwani Zanzibar.
Pia, mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibar Aprili 26, mwaka 1964 na ilipofikia Aprili 27, mwaka 1964, viongozi wa nchi hizo walikutana katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam ambako walibadilishana Hati za Muungano.




