Na MWANDISHI MAALUMU, Zanzibar
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema mawasiliano serikalini yanahitaji uratibu, weledi na mwelekeo wa kimkakati kujenga imani ya wananchi kwa serikali na kulinda maslahi ya Taifa.
Amesema hayo Ikulu ya Tunguu, Zanzibar, , alipofungua semina elekezi ya mawaziri, naibu mawaziri na makatibu wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu umuhimu wa mawasiliano serikalini.
“Mawasiliano ni sehemu ya uongozi na nyenzo ya kimkakati ya kulinda maslahi ya taifa,” alisema.
Alieleza kuwa, mawasiliano yanapotumika vizuri hujenga ushirikishwaji na imani ya wananchi kwa serikali, huku taarifa sahihi zikiwawezesha kuelewa na kushiriki katika mipango ya maendeleo.
“Taarifa za serikali zinapaswa kutolewa kwa wakati, kwa lugha inayoeleweka na kwa takwimu zilizothibitishwa,” alisema.
Rais Dk. Samia alisema serikali zote mbili zimepata mafanikio katika sekta za elimu, afya, miundombinu, nishati na maeneo mengine ya maendeleo, ambayo yanapaswa kuelezwa kwa wananchi kwa ufasaha.
Kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Rais Dk. Samia alisema serikali zimeanza kutekeleza mageuzi ya uchumi na huduma zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
Alisema takribani asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira 2050 inategemea ushiriki wa sekta binafsi, hivyo mafanikio yake yanahitaji mawasiliano na ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta hiyo.
Awali, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, alisema semina hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia ya kuwajengea viongozi uwezo katika mawasiliano ya serikali na umma.
Alisema mafunzo hayo yatahusu utoaji wa taarifa kwa ufasaha na kwa wakati pamoja na matumizi sahihi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Semina hiyo ya siku mbili imewakutanisha, kwa mara ya kwanza, viongozi waandamizi wa serikali kutoka pande zote mbili za Muungano, kwa lengo la kujenga uelewa na msimamo wa pamoja kuhusu mawasiliano ya serikali na umma.



