Na MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi Mkoa wa Simiyu limefanikiwa kumpata kijana mwenye umri wa miaka 20, Gatami Maduhu Martine, Msukuma mkazi wa Kijiji cha Mwauchumu, Wilaya ya Bariadi, aliyedaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa muda wa wiki moja na kusababisha hofu kwa familia yake.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, tukio hilo liliripotiwa Septemba 25, 2026, majira ya saa 10:00 jioni, baada ya Gatami Maduhu Maltine, mwenye umri wa miaka 64, mkazi wa Mwauchumu, kutoa taarifa kuhusu kutoweka kwa mjukuu wake.
Alieleza kuwa Gatami aliondoka nyumbani Septemba 19, 2026, akidai kwenda kwenye mgodi uliopo Mwabasabi, Kata ya Gibeshi.
Jeshi hilo limeeleza kuwa Septemba 23, 2026, majira ya saa 4:00 usiku, Gatami alimpigia simu mdogo wake, Sayi Maduhu, na kumweleza kuwa alikuwa sehemu asiyoijua na kwamba alikuwa amefungiwa ndani ya nyumba kwa siku tano na watu waliodaiwa kumteka.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Gatami aliwaeleza ndugu zake kuwa watu hao walitaka kutumiwa kiasi cha Shilingi milioni tano (5,000,000) ili wamwachie.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi uliofanywa kuhusiana na tukio hilo umebaini kuwa Gatami lalijiteka mwenyewe kwa lengo la kupata fedha kutoka kwa ndugu zake.




