Na LILIAN JOEL, Arusha
UMOJA wa Mataifa (UN), umesema Tanzania imeendelea kuwa nchi yenye mazingira ya amani, hali inayofanya kuwa na msingi muhimu wa maendeleo ya sekta ya utalii na kunufaika na vivutio vilivyopo.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Susan Namondo, alisema hayo katika mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaondelea jijini Arusha.
Alisema amani ni muhimu katika kuendeleza utalii, akibainisha sekta hiyo haiwezi kuendelea bila kuwepo mazingira salama.
Susan aliyesema kwamba, amekuwa nchini kwa takribani miaka miwili, amepata fursa ya kutembelea maeneo ya utalii, zikiwemo Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda mazingira hayo ya amani.
“Kwa wazi Tanzania imekuwa mahali penye amani kubwa kwa miaka mingi. Tunatumaini hali hii itaendelea, kwa sababu utalii ni faida kubwa, siyo tu kwa nchi kiuchumi, bali kwa dunia kupata fursa ya kunufaika na hazina zilizopo hapa,” alisema.
Alisema amani ni miongoni mwa mambo yanayowezesha sekta ya utalii kuendelea kukua na kutoa manufaa ya kiuchumi kwa nchi.
Susan alisema Serikali ya Tanzania, inaweka mkazo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku ikifanya juhudi kuweka misingi ya utekelezaji wa ajenda hiyo ya maendeleo.
Alisema changamoto zinazohitaji kuendelea kupewa kipaumbele ni pamoja na kuhakikisha vijana wanapata fursa za kiuchumi, kuongeza tija katika kilimo na kuimarisha sekta za kijamii.
“Kwa ujumla, dira ni waraka muhimu wa msingi na tunaona juhudi ambazo serikali inaweka kuanza kuitekeleza,” alisema.
Alisema washirika wa maendeleo, wakiwemo Umoja wa Mataifa, wako tayari kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Tanzania.
Akizungumzia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Susan alisema hivi sasa, hali ya utekelezaji duniani bado siyo nzuri, huku takribani asilimia 36 ya malengo hayo, yakiwa katika mwelekeo wa kufikiwa.
Alisema hali hiyo imeathiriwa na matukio mbalimbali ya kimataifa, likiwemo janga la Covid-19 na vita vya Ukraine, ambayo yameathiri maendeleo ya nchi nyingi.
Hata hivyo, alisema wananchi bado wanahitaji huduma bora na fursa za kiuchumi, kuna haja ya kuongeza nguvu katika utekelezaji wa mipango iliyopo.
“Tunapaswa wote kuzingatia zaidi utekelezaji. Tuna mikakati na sera za kutosha. Sasa tunahitaji kuhakikisha utekelezaji unafanyika katika ngazi ya chini,” alisema.
Susan alisema Bunge lina nafasi muhimu katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa, likiwemo jukumu la kufuatilia matumizi ya fedha za maendeleo na kuwawajibisha wahusika kuhusu utekelezaji wa mipango.
Alisema mabunge yanapaswa kuhakikisha kuwa pale malengo na viashiria vinapowekwa, vinafuatiliwa mara kwa mara ili kujua hatua zilizochukuliwa kuyafikia.
“Wakati viashiria na malengo vinawekwa, wanapaswa kuwepo na baadaye kuuliza mara kwa mara wahusika wote muhimu wamefanya nini ili kuyafikia,” alisema.
Alisema jukumu hilo ni muhimu katika kipindi ambacho fedha za maendeleo siyo nyingi, huku akitaka mabunge kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika vizuri.
Aidha, Susan alisema Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), una umuhimu kwa kuwa, unawakutanisha wabunge kutoka nchi mbalimbali, wakiwemo wanaounga mkono serikali na upinzani.
Pia, alisema jukwaa hilo linawezesha wabunge kutoka nchi ambazo huenda hazizungumzi katika majukwaa mengine, kukutana na kujadili masuala yanayowahusu wananchi.




