• ePaper
Tuesday, October 13, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home AFYA

MA-RC WABEBESHWA BIMA AFYA KWA WOTE

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
October 13, 2026
in AFYA, Habari, Kitaifa
0
MA-RC WABEBESHWA BIMA AFYA KWA WOTE
0
SHARES
5
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

NA EMMANUEL MOHAMED

WAZIRI wa Afya, Mohammed Mchengerwa, ametoa maagizo 12 kwa wakuu wa mikoa (RCs), yanayowataka kutekeleza kikamilifu ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote.

Maagizo hayo aliyatoa katika kikao na wakuu hao wa mikoa ambacho kilichohusu ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote, jijini Dar es Saalam.

“Kabla ya uzinduzi, kila mkuu wa mkoa ahakikishe Kamati ya Mkoa ya Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote imeundwa, na anaiongoza mwenyewe.

Katibu Tawala wa Mkoa awe katibu, kamati za ulinzi na usalama, wajumbe wawe mganga mkuu wa mkoa, meneja wa NHIF (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya) wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, mratibu wa TASAF (Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini) na mwakilishi mwenye mamlaka ya kufanya uamuzi kutoka MSD (Bohari Kuu ya Dawa,” aliagiza.

Alisema kwa siku 14 za kwanza baada ya uzinduzi, wanatakiwa kufanya mapitio kila siku ana kwa ana au kwa njia ya mtandao.

“Baada ya hapo, kamati ikutane kila wiki, msigeuze vikao hivi kuwa sehemu ya kusomeana taarifa ndefu. Kila kikao kijibu; tumefikia wapi, tumekwama wapi, nani anaondoa kikwazo, na lini?” Alifafanua waziri huyo wa afya.

Alisema kiongozi akifuatilia jambo watendaji hulipa uzito na akiishia kulitaja kwenye hotuba nao hujifunza kwamba maneno yanatosha.

“Agizo la pili kila lengo liwe na eneo la mwenye kulisimamia na tarehe kabla ya uzinduzi, malengo ya mkoa yawe yamegawanywa hadi wilaya, halmashauri, kata, vijiji na mitaa.

“Kupitia utaratibu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, waweke ahadi za utendaji zinazoonesha malengo yao, hatua za kuyafikia na muda wa utekelezaji.

Alisema mpango huo uoneshe watumishi watakaotumika, gharama na namna ya kuyafikia maeneo ya mbali, na kwamba hataki malengo makubwa kwenye karatasi yasiyo na watu wala nyenzo za kuyatekeleza.

“Msihesabu majina yaliyoingizwa kwenye mfumo pekee. Hakikisheni usajili umekamilika, mwananchi amepewa uthibitisho na anaelewa lini na wapi anaweza kupata huduma.

“Lengo la taifa haliwezi kubisha hodi nyumbani kwa mwananchi. Mtendaji wa eneo lake ndiye anayeweza kufanya hivyo. Ndiyo maana kazi hii lazima ifike mahali wananchi wanapoishi.

Alisema agizo la tatu ni kuwa uzinduzi uwe mwanzo wa huduma, si mwisho wa maandalizi.

“Uzinduzi wa mkoa ufanyike katika kituo cha kutolea huduma kilicho tayari, chini ya uongozi wa mkuu wa mkoa. Kaya ziandikishwe hapo hapo, zipewe uthibitisho wa usajili na maelezo sahihi kuhusu mafao, masharti na kuanza kwa huduma.

“Agizo la nne mfuateni mwananchi msimsubiri aache maisha yake aje ofisini, mwendesha bodaboda akiacha kazi siku nzima, ameacha pia mapato ya familia yake. Mvuvi, mkulima na mfanyabiashara mdogo wana hali hiyo hiyo,” Mchengerewa alifafanua.

Alisema kila halmashauri iwe na ratiba inayotangazwa mapema ya uandikishaji katika masoko, vituo vya bodaboda, maeneo ya uvuvi na uchimbaji mdogo, AMCOS, SACCOS na vikundi vya wananchi.

Mchengerwa aliwaagiza kupanga huduma zinazoyafikia maeneo ya mbali na watu wenye mahitaji maalumu, NHIF iratibu watumishi na mawakala walioidhinishwa, pamoja na njia rasmi za malipo, ili mwananchi akamilishe hatua zinazowezekana kwa safari moja.

“Agizo la tano walindeni wanaostahili kulipiwa na Serikali, na fungeni mlango wa upendeleo, shirikianeni na TASAF na mamlaka za vijiji na mitaa kuhakiki kaya kwa vigezo vilivyoidhinishwa,” alisema.

Waziri huyo alitaja agizo la sita ni wakuu wa mikoa kutekeleza kazi hiyo bila kuwaonea wananchi kwa kufuata Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, kanuni na taratibu zake.

“Hakuna mkoa, wilaya wala halmashauri itakayobuni adhabu, ukamataji, vizuizi vya barabarani au masharti ya kumnyima mwananchi huduma nyingine za umma bila msingi wa kisheria,” alisema.

Agizo la saba linawataka viongozi hao kukagua utayari wa kila kituo na kujiridhisha kabla ya uzinduzi.

“Thibitisheni uwepo wa dawati lenye mtumishi, mfumo wa uhakiki unaofanya kazi, dawa na vifaa muhimu, pamoja na utaratibu wa rufaa na wa kuendelea kutoa huduma mfumo wa kielektroniki unapopata hitilafu,” alisema.

Agizo la nane, waziri huyo aliwataka wakuu wa mikoa hao kuagiza dawa kwa wakati na fedha za huduma zirudi katika huduma.

“Wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe mahitaji ya dawa yanakadiriwa kwa usahihi, maagizo yanapelekwa MSD kwa wakati na upatikanaji unafuatiliwa, msisubiri dawa iishe ndipo muanze kutafuta suluhu.

“Kila halmashauri ijue dawa muhimu zinazokaribia kuisha, hatua iliyochukuliwa na lini zinatarajiwa kupatikana, marejesho ya bima yatumiwe kwa dawa, vifaa na uendeshaji wa huduma kwa mujibu wa taratibu. Yasihamishiwe kwenye shughuli nyingine za halmashauri,” alionya Mchengerewa.

Alisema fedha inayopatikana kwa kumhudumia mgonjwa irudi kuboresha huduma ya mgonjwa.

“La tisa mlindeni mwanachama anapohitaji huduma, si wakati wa kumwandikisha tu, mwanachama mwenye uanachama halali apewe huduma anazostahili kwa mujibu wa kifurushi na masharti yake.

“Asirudishwe bila sababu halali, asidaiwe malipo yasiyoidhinishwa, wala asibebeshwe gharama kwa sababu kituo hakijatimiza wajibu wake, dawa iliyomo kwenye kifurushi inapokosekana, kituo kishirikiane na NHIF kupata suluhu kwa utaratibu unaotumika,” alisema. 

Waziri Mchengerwa katika agizo la 10 aliwataka wakuu wa mikoa kutoa ujumbe mmoja sahihi na unaoeleweka na watumie taarifa na nyenzo zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya na NHIF.

“La 11, kila lalamiko lipate mwenye kulishughulikia na mwisho wake ujulikane, kila halmashauri iwe na dawati na namba ya malalamiko inayofanya kazi. Kila lalamiko liandikishwe, lipewe kumbukumbu na mhusika anayelifuatilia.

“Malalamiko ya kunyimwa huduma ya dharura yashughulikiwe mara moja. Mengine yatatuliwe ndani ya siku saba, yanayohitaji uamuzi wa NHIF au wizara yawasilishwe bila kucheleweshwa na mlalamikaji aelezwe hatua iliyofikiwa,” alisema.

Agizo la 12, waziri aliwataka wakuu wa mikoa kutoa taarifa ya ukweli na kwamba kila tatizo liambatane na hatua zilizochukuliwa kulitatua.

“Kwa siku kumi na nne za kwanza, taarifa ifike kila siku jioni, baada ya hapo taarifa ya wiki ifike kila Jumatatu asubuhi, itakuwa taarifa moja inayowasilishwa kwa wakati mmoja kwa wizara ya afya kupitia katibu mkuu, na kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia katibu mkuu,” aliagiza.

VITUO 7,989 KUTOA HUDUMA

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI, Dk. Jafar Seif, alisema vituo vya kutolea huduma za afya ni 7,989 zikiwemo zahanati 6,693 na vituo vya afya 1001.

“Hospitali za halmashauri 183 pamoja na hospitali 12 zenye hadhi ya hospitali ya wilaya zinaendelea na utoaji wa huduma bora za afya ngazi za afya ya msingi.

“Ujenzi wa majengo 87 yautoaji wa huduma za dharura na majengo 30 ya wagonjwa mahututi umekamilika na yanaendelea kutoa huduma hadi sasa; mitambo 21 ya kuzalisha hewa tiba imenunuliwa na imesimikwa kwenye hospitali 129,” alisema.

 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Grace Magembe,  alisema kwa sasa serikali inaingia kwenye utekelezaji mzima wa bima ya afya kwa wote.

“Tulianza majaribio kwa kaya zisizokuwa na uwezo,  sasa tunakwenda kusajili kaya zisizo kuwa na uwezo na zenye uwezo, tumeona leo tuwakutanishe wakuu wa mikoa kutokana na kuwa mzigo utaongezeka.

“Kwa sababu tunakwenda zaidi kwenye kile ambacho tumekianza, pia  tunahitaji kuwaonyesha Watanzania kuwa serikali tupo tayari, na ni kweli tupo tayari,  tumejifunza baadhi ya mambo,” alisema.

Dk. Magembe alisema huduma ya Bima ya Afya kwa Wote itatekelezwa pia kwenye vituo vya afya binafsi.  

ASILIMIA USAJILI WAPANDA

Mkurugenzi Msaidizi Sera, Utafiti, Ubunifu katika wizara ya afya, Dk.Tumaini Macha, alisema waliokuwa wakipata huduma ya afya kwa kutumia bima ya afya ni asilimia tisa ya idadi ya watu nchini.

“Baadaye tulipoanza kupitia sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na baada ya kusitisha kuendelea kusajili kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) asilimia hiyo ilishuka hadi fukia asilimia nane.

“Lakini baada ya kuanza utekelezaji wa awamu ya kwanza, hali ya wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya iliongezeka kutoka asilimia 8 hadi asiliami 11.2,” alisema.

Alisema hali hiyo ilikuwa ikimaanisha kuwa bima ya afya kupitia mfuko wa serikali (NHIF) ilifanikiwa kusajili asilimia 10.7 katika mfumo wa bima ya afya.

“Tumeona katika kipindi kifupi kumekuwepo na ongezeko la watu wanaojisajiri kwenye mfumo wa huduma za bima ya afya, tunaamini tukishirikiana vizuri kwa kutoa elimu ya umuhimu wa bima ya afya ndani ya mwaka huu, tutafikia asilimia 20,” alisema

Previous Post

RAIS DK. SAMIA AMPA TANO JIHAN DIMACK

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

ULEGA AJIBU MAPIGO KUHUSU MTANDAO WA BARABARA NCHINI

ULEGA AJIBU MAPIGO KUHUSU MTANDAO WA BARABARA NCHINI

6 months ago
WATANZANIA 37,647,235 KUPIGA KURA LEO

WATANZANIA 37,647,235 KUPIGA KURA LEO

12 months ago

Popular News

  • MA-RC WABEBESHWA BIMA AFYA KWA WOTE

    MA-RC WABEBESHWA BIMA AFYA KWA WOTE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. SAMIA AMPA TANO JIHAN DIMACK

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • HATIMAYE IMELIPA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TANZANIA NJIA NYEUPE MISS GRAND 2026

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SIMBA, YANGA ZAPIGWA ‘STOP’

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Not enough quota to unlock this post
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?