Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amempongeza mnyange, Jihan Dimack kwa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania na kutwaa taji la Miss Grand International 2026.
Rais Dk. Samia alitoa pongezi hizo jana baada ya Jihan kutangazwa mshindi katika fainali za shindano hilo zilizofanyika Bangkok, Thailand ambapo walishiriki warembo 79 kutoka nchi mbalimbali.
“Ninakupongeza kwa dhati mwanangu, Jihan Dimack kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania na kutwaa taji la Miss Grand International 2026.
“Ushindi huu ni fahari kwa Taifa letu na kielelezo cha uwezo wa Watanzania kufikia mafanikio makubwa tunapoungana na kushirikiana.
“Pia ni chachu ya vijana, hususan wasichana, kujiamini, kuthubutu na kusimamia ndoto na vipaji vyao,” alisema Rais Dk. Samia.
Jihan Dimack aliandika historia kubwa jana, baada ya kushinda taji kuu la Miss Grand International 2026 katika shindano lililofanyika nchini humo na amekuwa mrembo wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na bara zima la Afrika kwa ujumla kubeba taji hilo tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 2013.
Fainali za MGM 2026, zilishirikisha warembo 79, kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo Jihan, Miss Tanzania 2016, aliwania taji huku tayari akiwa na mataji madogo matatu ya awali, aliyotwaa siku nne zilizopita, baada ya kuwabwaga wapinzani wenzake 78.
Ushindi wa tuzo hizo, umemuweka Jihan katika nafasi nzuri baada ya kuchuana vikali na Miss Grand Equador, Shyare Andrade.
Pamoja na Jihan, baadhi ya warembo wengine waliokuwa wanawania taji hilo ni Sara Shehu (Albania), Amest Aretunian (Armenia|), Cat Jane Sherpherd (Australia), Anonna Fatima (Bangladesh), Emily Baesen (Ubelgiji), Kaithlain Da Rocha (Bolvia|), Paula Ansuacao (Brazil) na Patricia Seward (Canada).
Wengine ni Ignacia Micheleson (Chile), Liu Mengmeng (China), Hana Dedkova (Jamhuri ya Czech), Keith Familia (Jamhuri ya Domonica), Shyare Andrade (Equador), Menna Elbatran (Misri), Valeria Amaya (El Salvado) na Axelle Valin (Ufaransa).
Pia, walikuwepo Adelaide Twum (Ghana), Estaphenie Charles (Haiti), Yolanda Liu (Hongkong), Lakshita Thiragalaj (India), Dilza Salsabila (Indonesia), Tanin Alemi (Iran), Angelica Marzial (Italia), Somone Gardner (Jamaica), Sara Chiba (Japan) na Alba Fazlija (Kosovo).



