Na MWANDISHI WETU
WAKATI Simba ikihitaji kupunguza idadi ya pointi ilizoachwa na kinara Yanga, kikosi cha Singida Black Stars kitaingia katika mtanange wa leo, kuvunja mwiko wa kutoshinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi katika Ligi Kuu Bara.
Singida Black Stars itachuana na Simba leo saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Airtel uliopo mjini Singida.
Katika pambano hilo, Simba itahitaji alama tatu kusogea zaidi katika mbio za kuwania ubingwa dhidi ya kinara Yanga wakati Singida ikiwa na kibarua cha kuvunja mwiko wa kutoifunga Simba katika mechi mbili msimu uliopita.
Katika mitanange hiyo miwili msimu uliopita, Simba ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 ugenini kabla ya kushinda 1-0 nyumbani katika ligi hiyo.
Kwa mujibu wa msimamo wa ligi hiyo, Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 24 baada ya kushuka dimbani mara 11, imeshinda mechi saba, imetoka sare mara tatu na kufungwa moja, ikiachwa alama nane na kinara Yanga iliyocheza mechi 12.
Wekundu hao wa Msimbazi wamefunga mabao 18 na kuruhusu mabao manne.
Kwa upande wa Singida Black Stars ipo nafasi ya tisa ikiwa na alama 19 baada ya kucheza mechi 12, ikishinda tano, sare nne na kufungwa tatu, ikipachika mabao 11 na kuruhusu mabao 11.
Kocha wa Singida Black Stars, David Ouma alisema kikosi chao kipo fiti na kinahitaji alama tatu katika mechi hiyo.
“Matarajio yetu ni kutumia vyema uwanja wetu wa nyumbani, tunajua ubora wa mpinzani wetu, lakini lengo letu ni kupata ushindi, tutahakikisha tunacheza kwa ubora zaidi,”
Kocha wa Simba, Steve Barker, alikiri ubora wa Singida Black Stars, lakini ana imani kikosi chake kitavuna pointi tatu.
“Ni mechi nzuri sana, tumetoka kupata sare mbili, sasa tunahitaji kushinda ili kurejea katika ubora, Singida ni timu nzuri, lakini niwaahidi tu mashabiki kwamba tutafanya kila linalowezekama kupata ushindi,” alisema.
Mchezo mwingine utakaopigwa leo utakuwa kati ya Azam FC na Dodoma Jiji utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma saa 1:15 usiku.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kassim Liogope, alikiri mechi hiyo itakuwa ngumu lakini anaamini timu yake itapata ushindi.
“Tunajua tunakwenda kukutana na mshindani wa aina gani, bahati nzuri tumepata kuwaona Dodoma Jiji wakicheza, ni timu imebadilika, ninaamini tutakuwa na mechi nzuri,” alisema.
Kocha wa Dodoma Jiji, Aman Josiah alisema amekiandaa vyema kikosi chake kuwania pointi tatu na japokuwa kumkosa mchezaji Abdi Banda anayetumikia adhabu ya kukosa mechi tatu, itakiathiri kikosi hicho.




