Na MWANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, anastahili kupewa ridhaa ya kuongoza nchi kwa kuwa, amefanikiwa kulivusha salama taifa katika kipindi kigumu aliposhika hatamu ya uongozi.
Wasira aliyasema hayo katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu zilizofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Akimtambulisha mgombea urais kupitia CCM, Dk. Samia, Wasira, alielezea kuwa, kiongozi huyo, alipokea madaraka nchi ikiwa inakabiliwa na majanga matatu.
Aliyataja majanga hayo ni Uviko-19, kuporomoka uchumi kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia nne na janga la nchi kuondokewa na Rais Hayati Dk. John Magufuli, akiwa madarakani.
“Pamoja na majanga hayo, Dk. Samia, aliivusha nchi salama na kuchangia kuimarika umoja wa Watanzania na nchi kuendelea kuwa na amani.
“Alitumia muda wake kukutana na makundi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa na Jukwaa la Wahariri (TEF) na kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizoelezwa na makundi hayo,” alibainisha.
Wasira alisema Dk. Samia, alitekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ukiwemo mradi wa uzalishaji umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).
Alitaja mradi mwingine ni ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ambao unandelea.
Vilevile, alisema Dk. Samia amejenga shule, vituo vya kutolea huduma za afya na kutolea mfano Dar es Salaam pekee shule 224 za sekondari zimejengwa ndani ya miaka minne.




