Na NJUMAI NGOTA,
Mwanza
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema nafasi za urais, ubunge na udiwani zinahitaji watu wenye utayari, uwezo, dhamira, malengo na kusudio la kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa mkoani hapa na Katibu wa Idara ya Organaizesheni ya CCM, Issa Haji Gavu, alipozungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM zilizofanyika viwanja vya Furahisha, wilayani Nyamanga.
Mgombea Mwenza wa Urais kupitia CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, alizindua kampeni za uchaguzi mkoani humo.
Gavu amesema Chama kinaheshimu nafasi ya kiongozi ya kukiwakilisha.
“Nafasi ya kiongozi wa kuiwakilisha jamii yetu, tunaamini nafasi za uongozi iwe udiwani, ubunge na urais ni nafasi ambazo zinahitaji watu wenye utayari, uwezo, dhamira, malengo na wenye kusudio la kusukuma mbele gurudumu la maendeleo,”amesema.
Amesema yapo mambo ambayo yanabahatishwa, kwa jambo la uongozi wa taifa, majimbo na kata siyo ya fahari, hivyo wanahitaji viongozi wa kulitoa taifa lilipokuwepo jana, leo na kesho.
Gavu alisema hakuna kiongozi wa chama kingine chochote mwenye kujua dhamira hiyo, zaidi ya viongozi wanaotokana na CCM.
Amewaomba wananchi vyama vingine vitakapokuja wavipe nafasi ya kuvisikiliza, wapime na kutazama dhamira zao.
“CCM imejiandaa kwa sera, Ilani na kwa kutambua yapo mafanikio tuliyofanikiwa, zipo changamoto tunazokabiliana nazo na ipo mipango ya kuachana na changamoto hizo.
“Tutakapokuja kwenu, hatuji kulalamika, tutakuja kuwaeleza tumetoka wapi, tupo wapi na tunakwenda wapi, hiyo ni dhamira ya Chama,”amesema.