Na NJUMAI NGOTA,
Simiyu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, iwapo kitapata ridhaa ya kuiongoza nchi, kitaanzisha mitaa ya viwanda.
Ahadi hiyo, ni miongoni mwa zile 100, alizotoa Mgombea Urais, Dk. Samia Suluhu Hassan, Agosti 28, mwaka huu wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilizofanyika Viwanja vya Tanganyika Perckers, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa CCM, lengo la kuanzishwa mitaa ya viwanda ni kuimarisha uzalishaji wa ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuongeza ajira kwa vijana.
Kauli hiyo, imetolewa na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, alipowahutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkula, wilayani Busega, Mkoa wa Simiyu.
Balozi Dk. Nchimbi, amesema kuanzishwa kwa mitaa ya viwanda, kuna dhamira ya kuhakikisha nchi inajitegemea kiuchumi na kuwa na heshima kubwa duniani, kutokana na mageuzi ya viwanda ambavyo vitazalisha bidhaa mbalimbali.
Balozi Dk. Nchimbi, amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kila kijana anapata ajira kupitia viwanda hivyo.
Amesema kutokana na viwanda hivyo, kila kaya itanufaika kwa viwanda, hiyo ndiyo dira ya Mgombea Urais wa Chama, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Balozi Dk. Nchimbi, amesema katika kipindi kijacho cha miaka mitano, serikali itajikita zaidi kuimarisha huduma za kijamii na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi. Pia, sekta ya afya, itaendelea kupewa kipaumbele kwa kujenga vituo vipya vya afya vinne na zahanati mpya nne wilayani Busega.
ELIMU
Balozi Dk. Nchimbi, amesema shule za sekondari tano na mbili za msingi, zitajengwa huku madarasa mapya 76 yakiongezwa kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Kuhusu sekta ya maji, Dk. Nchimbi, amesema watahakikisha huduma zinapatikana vijijini na unafikia asilimia 90.
Akizungumzia kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, Balozi Nchimbi amesema katika siku 100 za kwanza, serikali ijayo mambo mbalimbali yatachukuliwa, kusaidia matibabu ya magonjwa likiwemo shinikizo la damu na sukari.
Amesema sh. bilioni 200, zimetengwa kusaidia biashara ndogo na kurasimisha wajasiriamali wadogo wapate mikopo na kukuza mitaji yao.
Amesema mafanikio mengi, yamepatikana katika maendeleo wilayani humo ni kujengwa hospitali ya wilaya, vituo vinne vya afya, zahanati saba, shule mpya tisa za sekondari na ongezeko la madarasa kutoka 1,043 hadi 1,342.
SEKTA YA MAJI
Amesema miradi 15 yenye thamani ya sh. bilioni 12, imetekelezwa ikiwa ni pamoja na mradi wa Lamadi-Mkula ambao umefanyika, asilimia 72 ya wananchi, wanapata maji safi na salama.
KILIMO
Balozi Dk. Nchimbi, amesema ruzuku ya mbolea na mbegu bora, imeongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Amesema zao la alizeti, limeongezeka kutoka tani 1.2 hadi 5.5 na uzalishaji wa mpunga kufikia kilo 14,000 kutoka kilo 3,900 kwa ekari.
MBUNGE WA ZAMANI
Naye, Mbunge wa zamani wa Busega, Raphael Chegeni, amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa miaka mitano iliyopita ni ushahidi, Chama hicho ndicho kinawaletea wananchi maendeleo.
Mbunge huyo wa zamani, amesema Chama kimetekeleza Ilani kwa vitendo na wameona matunda ya uongozi wa Rais Dk. Samia, hivyo wana kila sababu ya kumpa kura za kishindo wakiwemo wabunge na madiwani.