Na MUSSA YUSUPH,
Songwe
KATIKA kuboresha upatikanaji umeme mkoani Songwe, mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameahidi kujenga njia ya umeme yenye msongo wa kilovoti 730 itakayokwenda kuimarisha upatikanaji nishati hiyo.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Tunduma mkoani Songwe, Dk. Samia amesema umeme huo pia utauzwa nchini Zambia.
“Serikali imejipanga kutekeleza mradi wa umeme kutoka Iringa – Njombe hadi Tunduma yenye msongo wa kilovoti 730, kati ya hizo kilovoti 400 zitatumika Tunduma na Rukwa huku kilovoti 330 zitakwenda kuuzwa nchini Zambia.
Ameeleza: “Tumeshakamilisha mazungumzo, tumeanza mchakato kujenga njia hii ili umeme ufike kwa uhakika. Hii inakwenda sambamba na uhamasishaji matumizi ya nishati safi kwa sababu umeme pamoja na gesi ni nishati safi,” alieleza.
Dk. Samia ameongeza: “Nataka kuwathibitishia na kuwaahidi, nitaendelea kufanya makubwa katika sekta ya elimu, afya, maji na umeme. Tunakwenda kutoa huduma kwa wananchi, tutaendelea kuongeza shule, elimu bila ada, mikopo kwa wanafunzi wa vyuo na VETA, kujenga vyuo vya VETA kuwawezesha vijana wapate ujuzi na kujiajiri.
Akizungumzia miradi ya maji, amesema serikali yake itahakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama kama ilivyoelekezwa katika ilani ya uchaguzi.
“Tutaendelea kujenga vituo vya afya na zahanati, tunakwenda kumaliza miradi ya maji lengo kuhakikisha kila Mtanzania apate maji safi na salama kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.
Baadhi ya maeneo tumefikia lakini baadhi ya maeneo miradi inaendelea. Umeme tumemaliza vijiji vyote, tupo nusu ya vitongoji na tunakwenda kuunga umeme kila mwananchi afaidike,” amebainisha.