PARIS, Ufaransa
NAHODHA wa Ufaransa, Kylian Mbappe amesema kufikia idadi ya mabao yaliyofungwa na mkongwe Henry katika timu hiyo ya taifa ni jambo lisilo la kawaida.
Mbappe amefikia mabao 51 yaliyofungwa na Henry katika timu hiyo baada ya juzi kufunga bao moja katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Ukraine katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia.
Mchezaji huyo hivi sasa anahitaji mabao sita pekee kumfikia Olivier Giroud ambaye ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Ufaransa, akiwa na mabao 57.
“Hongera sana kwa Titi (Henry), lakini sasa nataka kumpita yeye. Ni heshima kubwa kuwa sawa na mchezaji kama Henry, kila mmoja anajua Henry ana maana gani kwetu watu wa Ufaransa. Nina heshima kubwa sana kwake na ninamkubali,” alisema.
Henry alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichoshinda Kombe la Dunia mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka 20, huku Mbappe akishinda taji hilo mwaka 2018 akiwa na miaka 19.
“Rekodi inazidi kukaribia, lakini sio kitu ninachokifikiria. Sijui ni kwa sababu nafikiria ninaweza kuivunja au kwa sababu nafikiri kuna mambo mengi ya muhimu zaidi,” alisema.