Na NASRA KITANA
ALIYEKUWA nyota wa Simba na Yanga, Clatous Chama ameweka wazi kuwa amefurahia kujiunga na Singida Black Stars kwani ni timu kubwa hivi sasa na amejipanga kuisaidia kufikia malengo yake.
Chama aliyasema hayo baada ya mchezo wao dhidi ya Polisi ya Kenya katika mashindano ya Kagame yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Chama alisema atahakikisha anashirikiana vyema na wachezaji wezake ili kufanya vizuri.
Nyota huyo alisema kuwa anajua timu inahitaji nini hivyo yeye kama mchezaji atapambana kwa jasho na damu ili kufikia malengo na kusonga mbele.
“Nimefurahi kujiunga na Singida kwani ni timu kubwa na yenye wachezaji wengi bora hivyo nitapambana kwa jasho na damu kuonyesha kiwango kikubwa kufikia malengo,” alisema.
Chama alisema mashindano hayo ni muhimu kwa timu kwani inayatumia kama maandalizi mazuri kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alisema ligi ya msimu ujao itakuwa bora na yenye ushindani mkubwa kwani kila timu imejipanga vyema kufanya vizuri.