Na LATIFA GANZEL,
Morogoro
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, ameelekeza mambo matatu kwa viongozi wa Chama, kufanikisha ushindi wa kishindo kwa Mgombea Urais, Dk. Samia Suluhu Hassan, wagombea ubunge na udiwani.
Ameyataja mambo hayo ni kuvunja makundi, kueleza mambo mazuri na makubwa yaliyofanyika katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka minne.
Pia, kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura na kuwashawishi kuwapigia kura wagombea waliosimamishwa na CCM.
Wasira, alieleza hayo mjini Morogoro, alipozungumza na viongozi wa CCM wakiwemo mabalozi na wenyeviti wa mashina katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.
“Kwa hiyo ndugu zangu, baada ya kuwaeleza hayo, nataka niwakumbushe kuvunja makundi na kutangaza kazi zilizofanywa katika miaka minne ya kazi ya mgombea urais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Ili watu wakapige kura, lazima sisi viongozi tuwahamasishe kwenda kupiga kura, maana kuna wengine wakiwemo wanachama wetu, wanasema si amepita Aboud, situmemaliza? Anafikiri kura ya maoni inaweka mbunge.
“Kura ya maoni haijaweka mbunge, ndiyo maana Aboud tunamwita mbunge mteule, tena wa ndani ya CCM kwa sababu wa nje watakuja kuipinga CCM,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Sasa sisi kazi zetu ni kuhakikisha watu wanajitokeza na tunawashawishi kwa nini waipigie kura CCM, kazi nyingine ni kuwaambia watoke waende wakapige kura.”
Wasira alisema wajumbe wa mashina, ndiyo wenye Chama chao, kwa kuwa, Chama inaanzia chini na kwamba, mabalozi wote mwaka huu wamepewa usafiri.
“Kile ni kitendea kazi cha kutoka nyumba hadi nyumba, kuwaambia wananchi leo ni siku ya kupiga kura, tokeni nyote mkapige kura.
“Katika mfumo wetu, zamani ukikosa mpinzani unapita bila kupingwa, ila sasa kwa mfano, tuna mgombea wetu na wapinzani hawakujitokeza.
“Kule kunataka nguvu zaidi kwa sababu, watu watafikiri tayari, kumbe yule mgombea ili ashinde, lazima kura za ndiYo ziwe nyingi kuliko hapana, vilevile mgombea wa urais, anahitaji kura nyingi kila mahali, sasa atazipata wapi kama watu hawajitokezi kupiga kura?.
“Ndiyo maana, pamoja na kuona mkutano mkubwa wa ajabu wa mgombea urais mkoani Morogoro, mimi nimekuja kuwaambia haya, asanteni kwa mkutano mkubwa, waambieni watu wajitokeze kwenda kupiga kura.
“Wahimizeni wote, hata ambao hawataki kutupigia watoke wakapige kura, kimahesabu tutawazidi tu na wenyewe wanajua hilo,”alisema.
Alisema ushindi kwa CCM ni uhakika kutokana na wingi wa wanachama na wafuasi wake.
“Kwa mfano, Morogoro tuna wanachama 100,000, wapigakura wapo 200,000 hapo tayari tupo asilimia 50 ya wapigakura, maana hivi vyama vingine vinavyogombea, havina hata wanachama.
“Wito wangu kwa viongozi wa CCM hususan wenyeviti wa mashina na ninyi wenyeviti wa kata na jumuiya zote, kuwaambia wananchi kwanza, watupigie kura na sababu mnazo, pili wajitokeze wakapige kura,” alisema.