NJUMAI NGOTA na
LILIAN JOEL, Longido
MGOMBEA Mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika sekta za kilimo, ufugaji na utalii ni ushahidi wa kutosha wa dhamira ya dhati ya serikali, kuwaletea wananchi maendeleo.
Dk. Nchimbi, alisema hayo, alipohutubia mamia ya wananchi wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha, katika mkutano wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Alisema pamoja na changamoto za janga la Uviko-19 lililopunguza utalii kwa zaidi ya asilimia 80 kutokana na jitihada za Dk. Samia, ziliwezesha sekta hiyo kuimarika, hivi sasa Tanzania inapokea zaidi ya watalii milioni 4.9 kwa mwaka.
“Rais Samia, hakukata tamaa. Aliamua kupambana kwa nguvu kubwa kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu ya ‘The Royal Tour,’ leo matokeo tunayashuhudia.
“Watalii wameongezeka, biashara zimeongezeka, mapato ya taifa yameongezeka,” alisema.
UFUGAJI
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana miaka minne iliyopita katika sekta ya ufugaji, Dk. Nchimbi, alisema serikali imejenga majosho mapya 16 ya kuogeshea mifugo na zaidi ya lita 874 za dawa, zimetolewa kwa wafugaji wa Longido.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, serikali imetoa dozi 550,880 za chanjo kwa mifugo, kuzuia magonjwa na kuongeza tija katika uzalishaji.
MAJI
Kuhusu miundombinu ya maji, alieleza miradi tisa ya maji, imekamilika kwa gharama ya zaidi ya sh. bilioni tisa, huku miradi mingine 11 ikiendelea kutekelezwa.
ELIMU
Alisema kuna ongezeko la shule za msingi kutoka 49 hadi 59, sekondari 10 hadi 16 katika kipindi cha miaka mitano.
Hata hivyo, aliwahimiza wakazi wa wilaya hiyo, kuwapeleka watoto shule.
“Wamasai lazima wasome. Tunahitaji Wamasai wasomi kama ilivyokuwa enzi za Sokoine (Hayati Edward). Elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli,” alisema.
AFYA
Alisema katika kipindi cha miaka hiyo, zahanati zimeongezeka kutoka 23 hadi 30, vituo vya afya kutoka vinne hadi saba, hali inayoboresha upatikanaji huduma za afya kwa wakazi wa Longido.
UMEME
Dk. Nchimbi, alisema kati ya vitongoji 112 vya Longido, 34 vimepata nishati hiyo na kazi ya kufikisha katika vitongoji vilivyosalia, inaendelea.
“Tuna imani kubwa na Rais wetu. Ana nia, ana uwezo, ana dhamira ya kweli ya kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati wa juu kupitia maendeleo ya watu,” alisema.
Alisema Dk. Samia, ameendelea kuonesha dhamira ya kweli ya kuwaletea Watanzania maendeleo shirikishi na endelevu huku moja ya maeneo aliyoyapa kipaumbele ni kuboresha mazingira ya wafugaji nchini.
Alieleza kuwa, serikali chini ya Rais Dk. Samia, imejikita kuhakikisha sekta ya mifugo, inapata msukumo mpya kwa kuboresha huduma za afya ya mifugo, maeneo ya malisho na kutatua migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima.
Mbali na sekta ya mifugo, serikali imefanya kazi kubwa katika nyanja nyingine muhimu, ukiwemo uchimbaji madini, nishati ya umeme, afya, elimu, maji safi na salama, miundombinu ya barabara na miradi ambayo imefungua fursa za kiuchumi kwa mamilioni ya Watanzania vijijini na mijini.
Alisema kutokana sifa kubwa zaidi aliyonayo Dk. Samia ni uwezo wake wa kusikiliza matatizo ya wananchi wa kawaida na kuyafanyia kazi kwa vitendo.
“Hatuna Rais mbishi, hatuna Rais muongo. Tunaye Rais msikivu, mnyenyekevu, anayeguswa na shida za wananchi wake.
“Ndiyo maana, makabila yote nchini, kuanzia Kaskazini hadi Kusini, Mashariki hadi Magharibi, watu wanapopata shida, Rais wetu ama huenda mwenyewe, au hutuma wawakilishi wake waaminifu kuwasikiliza wananchi,” alisema.
MIAKA MITANO IJAYO
Balozi Dk. Nchimbi, alisema Chama kama kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo, kitaendelea kuboresha sekta hizo kwa kiwango kikubwa zaidi.
Pia, alisema katika miaka hiyo, wameahidi kujenga zahanati tano na vituo vya afya vinne, shule za msingi 26, kuongeza madarasa 88, kuimarisha miundombinu ya barabara na kuongeza maofisa mifugo.
Aidha, alisema wataweka mpango wa matumizi bora ya ardhi, utakaohakikisha kila kundi la wafugaji, wakulima na wafanyabiashara, wanapata maeneo maalumu ya shughuli zao.
NAMELOCK SOKOINE
Naye, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Namelock Sokoine, alisema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia, imeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika Jimbo la Longido kwa kuleta umeme wa Gridi ya Taifa katika vijiji vyote.
Alisema Dk. Samia, amewatua ndoo kichwani wanawake wa jimbo hilo, kwa kuleta miradi mikubwa ya maji ambayo imewezesha wanawake kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo tofauti na awali.
“Ninajua Wilaya ya Longido ni ngome ya CCM, niwaombe sana Oktoba 29, mwaka huu, tujitokeze kwa wingi kwenda kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM kwa maendeleo zaidi,” alisema.
DK. KIRUSWA
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Longido, Dk. Steven Kiruswa, alisema wilaya hiyo, imepata miradi mikubwa ya maendeleo, katika sekta ya elimu, wamepata zaidi ya sh. bilioni 4.
“Tunamshukuru Dk. Samia kwa kurejesha ardhi za wafugaji katika jimbo letu, japo kuna changamoto ndogo katika baadhi ya maeneo, hasa mashamba ya NAFCO,”alisema.
FREDY LOWASA
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli, Fredy Lowassa, alisema Dk. Samia, alipokea nchi katika kipindi kigumu cha janga la Uviko 19, ila aliendeleza miradi mikubwa ya kimkakati iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Dk. John Magufuli, ameikamilisha kwa asilimia 100 ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake.
MGOMBEA JIMBO LA NGORONGORO
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ngorongoro, Yaniki Ndoinyo, alisema Serikali ya Awamu ya Sita, imetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kwamba, shukrani yao, ni kuhakikisha wanaongoza kwa kura za Dk. Samia.