• ePaper
Wednesday, October 15, 2025
Subscribe
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
No Result
View All Result
Home Habari

DK. SAMIA AAHIDI WAKULIMA DAWA YA KUPULIZIA MIKOROSHO BILA MALIPO

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
September 26, 2025
in Habari, Kitaifa, Siasa, Uchaguzi
0
DK. SAMIA AAHIDI WAKULIMA DAWA YA KUPULIZIA MIKOROSHO BILA MALIPO

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan

0
SHARES
1
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na MUSSA YUSUPH,

Lindi

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema CCM hakitoi ahadi kutoka ndotoni, bali kinaahidi kisha kinatekeleza kwa vitendo.

Amesisitiza vyama vya upinzani vimekuwa vikitoa maigizo kwa kuahidi masuala yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo tayari Chama kupitia serikali zake imeshayatekeleza.

Pia, amesema serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mazungumzo kuhusu mradi ya gesi ya LNG na kuwahakikishia Watanzania maslahi ya taifa yamezingatiwa.

Akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika mkoani Lindi, Dk. Samia amesema hakuna Chama chenye uwezo wa kulinda na kuinua uchumi wa Tanzania zaidi ya CCM.

“Nataka niwaambie hakuna chama kitakachoweza kwa sasa kulinda na kuinua utu wa Mtanzania kama Chama Cha Mapinduzi. Hiyo ndiyo CCM, hatusemi kutoka ndotoni. Tukisema tunatekeleza.

“Na ndiyo maana tumekuja na hii kauli mbiu ya Kazi na Utu. Maana yake tupeni ridhaa yenu tuendeshe nchi hii tena kwa miaka mitano ijayo,”alisema.

Dk. Samia alisema katika kuinua utu wa Mtanzania ni kumpatia maji safi na salama, elimu, huduma za afya, umeme, kilimo kwani hiyo ndiyo tafsiri ya kulinda na kuukuza utu wa mtu.

“Wengine wanapitia ilani yetu wanadokoa dokoa. Wanasema tutatoa elimu bure kwani CCM haijatoa? Kuna fungu la mkopo ukienda chuo kikuu tunakwambia kopa hapa kijana kasome, ukipata kazi ukijiajiri utarudisha polepole.

“Mwingine anawaambia nitaleta maji, alikuwa wapi asilete siku zote?. CCM tumeshaleta maji. Kwa hiyo ahadi zao ni za kuigiza tu. Niwaombe sana wananchi tarehe 29 mwezi wa 10 nendeni mkachague Chama Cha Mapinduzi,” alieleza huku akishangiliwa na maelfu waliojitokeza katika mkutano wake uliofanyika Jimbo la Mchinga.

Alisema endapo CCM ikipewa ridhaa kuendesha serikali, itakwenda kukamilisha miradi iliyoanzishwa na ile iliyoahidiwa kupitia Ilani ya uchaguzi.

Alieleza upande wa maji, serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya mradi na awamu ya pili itakwenda kunufaisha vijiji vingine 10 vya jimbo hilo ambavyo havijapata maji.

Pia, alisema lengo la serikali ni kuona wananchi wa Mchinga wananufaika kupitia huduma za maji safi na salama.

Alibainisha akipewa ridhaa ya kuongoza serikali, visima vitachimbwa katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo kwa lengo la kuongeza kasi ya upatikanaji maji.

Kwa upande wa kilimo, aliwahakikishia serikali yake itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo.

“Tutaleta dawa ya kupulizia mikorosho bure, dawa za kuua wadudu, lakini dawa za kukabiliana na magonjwa ya mazao bure mikorosho ilimwe na izaliwe kwa wingi.

“Tunafanya hivyo lengo likiwa kujenga uwezo wa mkulima, tungemtaka mkulima afanye kila kitu mwenyewe, mazao ambayo mkulima ameyapata yasingepatikana na mashamba yasingepewa huduma inayostahili.

“Tunatoa ruzuku mkulima apate kuhudumia mashamba vizuri, korosho izaliwe, fedha iingie nyingi aweze kusimama mwenyewe,” alisema.

Pia, alisema serikali inaendelea kutafuta masoko yenye uhakika ambapo mfumo wa stakabadhi ghalani umetoa matokeo mazuri kwa wakulima.

Dk. Samia alieleza mfumo huo ulikuwa mgumu kukubalika ila umeleta matokeo mazuri kwa wakulima.

“Nataka niwahakikishie kwamba, kinacholetwa na serikali yenu mjue kina manufaa. Kikubalieni na mkifanyie kazi.

“Pia, tunatoa huduma za kitaalamu, huduma za ugani kuwawezesha maofisa ugani waweze kufuatilia maendeleo ya kilimo chetu,” alisisitiza.

Kadhalika, alisema serikali imetoa fedha kutekeleza miradi miwili ya umwagiliaji katika maeneo ya Lutamba na Kilangala.

Dk. Samia alisema hatua hiyo, itawawezesha wakulima katika maeneo hayo kuzalisha mazao yao mara mbili kwa mwaka.

Alisisitiza kwa sasa nchini hakuna mazao ya biashara na chakula, kwani hata mazao ya chakula nayo yamekuwa mazao ya kibiashara.

Pia, alisema serikali itaendelea kusimamia sekta ya kilimo kwa sababu Tanzania inazalisha mazao kwa wingi, hivyo muhimu kuwepo upatikanaji masoko yenye uhakika.

Alitoa ahadi kwa wananchi wa jimbo hilo serikali itajenga soko litakalohudumia mazao mbalimbali zikiwemo mbogamboga.

Alisema lengo ni ujenzi wa skimu za umwagiliaji utakapokamilika, wakulima watafundishwa walime mazao ya mbogamboga ambayo yanauzwa nje ya nchi.

Kwa upande wa mifugo katika maeneo ya Kitomanga na Mipingo, alieleza ruzuku ya chanjo kwa mifugo itatolewa bure.

“Katika ruzuku ya chanjo siyo Kitomanga na Mipingo peke yake. Maeneo yote yenye ng’ombe tumesema tutatoa ruzuku ya chanjo. Kama chanjo inalipiwa sh. 20,000 mfugaji atalipa sh. 10,000. Kama ni sh. 30,000 mfugaji atatoa 15,000 na serikali itamalizia.

“Kwa upande wa kuku, chanjo zote ni bure. Twende tukachanje mifugo yetu, kwani madhumuni ya kuchanja ni muda mrefu tulikuwa tukihangaika kutafuta soko.

“Tanzania hatukuwepo katika orodha ya nchi zinazochanja mifugo kwa hiyo afya ya mifugo yetu haikuwa ikitambulika. Tumetoa ruzuku ya chanjo mifugo yote ya Tanzania itambulike na tuingie katika soko la kimataifa,”alisema.

Alisema mbali na chanjo, serikali itakwenda kujenga majosho na machinjio bora kwa mifugo, nyama iwe yenye viwango vya kutambulika duniani.

Kwa upande wa uvuvi, alisema serikali ilitoa mikopo ya boti za kisasa za uvuvi zenye thamani ya sh. milioni 712 huku awamu ijayo, serikali itaendelea kutoa boti na vifaa vya uvuvi.

Pia, alibainisha katika maeneo ya Mkoa wa Lindi huduma zote za afya zinapatikana zikiwemo za kibingwa baada ya kuwepo hospitali kubwa ya rufaa.

Kuhusu elimu alisema endapo akipewa ridhaa ya kuliongoza taifa, serikali yake itajikita zaidi kujenga nyumba za walimu.

“Mchinga ni eneo lililochaguliwa kuwa na shule maalumu ya mchepuo wa sayansi kwa wasichana. Changamoto ndogo walizokuwa nazo tumeziondoa kwa hiyo matumaini yangu wataendelea kusoma vizuri,” alieleza.

Aliongeza serikali imeanzisha shule ya ufundi stadi Dk. Jakaya Kikwete iliyopo Kata ya Nangalo na ujenzi wake umefikia asilimia 70.

Alibainisha ujenzi huo utakamilika kuwezesha vijana wapate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Akizungumzia umeme, alisema vitongoji vilivyosalia kufikishiwa huduma hiyo, wakandarasi wanaendelea na kazi ikiwa ni utekelezaji ajenda ya nishati safi.

Alifafanua vijiji na vitongoji vyote vitakapopata umeme, matumizi ya kuni yatapungua.

“Tutatumia gesi au umeme kufanya mapishi yetu na tuiache misitu ipumue kidogo hali yake irejee ndani ya nchi yetu,” alieleza.

Alisema serikali inatambua mahitaji ya miundombinu ikiwemo ukarabati wa barabara na kuahidi uboreshaji wa barabara zilizoainishwa katika ilani ya uchaguzi.

Alitaja barabara hizo ni Milola-Kiwawa na nyingine ambazo zitajengwa kwa kiwango cha changarawe kuwezesha zipitike muda wote.

“Tutajenga stendi ya malori hapa Mchinga ambayo itapunguza msongamano na kuongeza fursa za biashara ndani ya eneo hilo. Aidha, mkitupa ridhaa kwa sasa tunatambua kuna uvamizi wa wanyamapori.

“Hususan maeneo ya Mipingo, Milola, Nanganga, Mtama na Kiwawa. Tunafanya jitihada za kuongeza askari wanyamapori lakini tumeamua kununua ndege nyuki kubwa ambazo kazi yake kufanya doria kufukuza wanyamapori wanaotoka katika maeneo yao,” alifafanua.

Dk. Samia alisisitiza serikali itaweka doria za kutosha wanyama hao wasiende kuharibu mazao ya wananchi.

Akiwa katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Lindi Mjini, alisema kazi kubwa ya maendeleo imefanyika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kuhusu mradi wa gesi wenye thamani ya dola bilioni 40, alisema lazima serikali iwe na uhakika wa kile ambacho itanufaika kupitia mradi huo.

Alisema serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mazungumzo kuhusu manufaa ya mradi huo kwa upande wa Tanzania.

Alisema kwa upande wa maji safi na salama umefikia wastani wa asilimia 87 nchini huku akiahidi awamu ya pili ya serikali yake itakwenda kutekeleza miradi mingi zaidi kuondoa changamoto hiyo kwa wananchi.

MAMA SALMA KIKWETE

Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Mchinga, Salma Kikwete, alisema wananchi wa jimbo hilo shukrani yao kwa Dk. Samia wataionesha katika sanduku la kura Oktoba 29, mwaka huu.

Alieleza jimbo hilo lenye wakazi zaidi ya 70,000 katika kipindi cha miaka mitano, kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi hao imefanyika.

Alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa ni mradi wa maji kutoka Ng’apa hadi Mchinga wenye gharama zaidi ya sh. bilioni 12 ambao unanufaisha wananchi wa vijiji vya Mchinga moja, Mchinga mbili na Ruvu.

Kwa upande wa barabara, alisema madaraja yakiwemo Mangoma, Lamilola na Lamatima yamejengwa kurahisisha wananchi kuvuka nyakati zote.

Alipongeza serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na kimbunga Hidaya.

Previous Post

RC MAKALLA ATAKA MPANGO MKAKATI WA UTALII UKIJUMUISHA FURSA NA MAANDALIZI YA AFCON 2027

Next Post

DK. SAMIA AMEONESHA UMAHIRI KATIKA UONGOZI – DK. NCHIMBI

Next Post
DK. SAMIA AMEONESHA UMAHIRI KATIKA UONGOZI – DK. NCHIMBI

DK. SAMIA AMEONESHA UMAHIRI KATIKA UONGOZI - DK. NCHIMBI

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

DK. SAMIA KUFANYA MKUTANO MKUBWA WA KAMPENI ZA CCM GOMBANI YA KALE

DK. SAMIA KUFANYA MKUTANO MKUBWA WA KAMPENI ZA CCM GOMBANI YA KALE

4 weeks ago
DK. BASHIRU AELEZEA UJASIRI WA DK. SAMIA

DK. BASHIRU AELEZEA UJASIRI WA DK. SAMIA

1 month ago

Popular News

  • SIMBA NI MWENDO WA MABAO LIGI KUU

    SIMBA NI MWENDO WA MABAO LIGI KUU

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • JESCA: DK. SAMIA NI KIONGOZI JASIRI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MAFANIKIO YA WATANZANIA YAKO KATIKA MATENDO – DK. MIGIRO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DK. SAMIA AAHIDI UCHUMI JUMUISHI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DK. MWINYI AAHIDI KUJENGA HOSPITALI MAALUMU YA SARATANI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
error: Content is protected !!
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2025 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.