Na SULEIMAN JONGO,
Mkinga
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewaonya baadhi ya wagombea udiwani walioanza harakati za kusaka uenyekiti wa halmashauri na umeya, kabla ya uchaguzi.
Amesema wanachotakiwa kufanya wanachama wa CCM wote kwa sasa ni kuhakikisha wanasaka kura za kishindo kwa Chama hususan za mgombea urais, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Wasira alisema hayo alipozungumza na viongozi na wanachama wa CCM katika kikao cha ndani kilichofanyika wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga.
Kikao hicho ni mfululizo wa vikao anavyoviendesha kwa kukutana na viongozi na wana-CCM kumwombea kura Dk. Samia, wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na Chama kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
“Kwa madiwani ninawaomba sana siyo hapa Mkinga, hapa sijaambiwa huko nilikotoka madiwani wameanza kutafuta mwenyekiti wa halmashauri na huku wao wenyewe hawajachaguliwa, sasa wewe utajuaje kama utachaguliwa wewe uanze kutafuta mwenyekiti wa halmashauri.
“Acheni mambo ya kutafuta mwenyekiti wa halmashauri kwanza tuchaguane halafu mambo ya mwenyekiti wa halmashauri yatakuja baadaye,” aliagiza.
Alisema hata nafasi ya umeya hutazamwa kupitia vikao vya juu na kwamba, katika mchakato wake iwapo atabainika diwani alianza mapema Chama hakitasita kumwengua katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo.
“Wameanza, ninawaambia hapana, hata umeya tunatazama katika kamati, nitasema nilikwenda Mkinga (ni mfano) nikawaambia hawakunisikiliza na huyu ndiye alikuwa anaongoza kampeni, tunamfuta tunaweka yule ambaye alikuwa ametulia.
“Siwatishi nawaambia maneno ya kweli na maneno ya kweli nayo yana ncha kali yanaweza kuonekana kama kitisho,” alisema.
Wasira alisema uchaguzi umewadia hivyo kila mwana CCM apambane kukitafutia Chama ushindi kiendelee kushikilia dola kwa manufaa ya Watanzania.
Alisema ana imani na wananchi wa Mkinga na Tanga kwa ujumla, hivyo hana shaka watampigia kura nyingi Dk. Samia kwa kuwa amewafanyia mambo makubwa huku Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025-2030 ikiwa imesheheni mengine mengi mazuri ambayo yatatekelezwa kwa miaka mitano ijayo
“Sasa uchaguzi upo tayari na mimi nina imani na watu wa Mkinga maana mmekuja hapa kwa wingi ni ushahidi kwamba CCM ina watu wake tena wengi.
“Nasimama hapa kwa niaba ya Dk. Samia Suluhu Hassan kuwaomba wananchi wa Mkinga na Mkoa wa Tanga kwa ujumla kumuunga mkono na kumpigia kura za kishindo,” alisema.
Wasira anahitimisha ziara yake mkoani humo leo, ambapo anakwenda mkoani Kilimanjaro kumnadi mgombea urais Dk. Samia.