Na MUSSA YUSUPH,
Korogwe
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza kufanya mabadiliko makubwa, pindi atakapopewa ridhaa ya kuliongoza taifa, yatakayogusa mashamba na viwanda vilivyobinafsishwa.
Viwanda na mashamba ambayo yataguswa ni yale ya chai na mkonge, ambayo yamebinafsishwa na wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza.
Katika kuthibitisha hilo, Dk. Samia ametoa maagizo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria, kupitia upya mikataba ya ubinafsishaji maeneo hayo na ile itakayobainika kukiukwa itavunjwa.
Amesema lengo la hatua hiyo ni kuiwezesha serikali na vyama vya ushirika, kuyaendeleza mashamba na viwanda hivyo, viongeze tija ya uzalishaji mazao kwa wakulima.
Dk. Samia, ametoa maagizo hayo katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika mjini Korogwe mkoani Tanga.
“Katika miaka mitano ijayo, tutahakikisha viwanda vilivyobinafsishwa, havifanyi kazi vinapatiwa wawekezaji wengine na kukabidhiwa kwa ushirika chini ya usimamizi wa serikali.
“Nataka niwaambie kwamba, kwa hapa Korogwe kuna mashamba ambayo yapo, hayaendelezwi, lakini watu wanayaangalia.
“Nimeelekeza Wizara ya Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wayafanyie kazi waangalie mikataba na wawekezaji namna gani tunaweza kuvunja mashamba yarudi serikalini, tufanye maamuzi mengine,” alieleza.
Ameongeza kuwa: “Kwa upande wa mashamba ya mkonge na hapa tuzungumzie mashamba ya Sisalana ambayo uchakataji mkonge umepungua.
“Kwa hiyo, tulichokifanya ni kuwataka NSSF na Wizara ya Kilimo, wafanye tathmini ya mashamba na kiwanda lengo letu kuongeza uwezo wa kuchakata kisha kufunga mitambo mipya.”
Dk. Samia, amesema mitambo hiyo, itaendeshwa chini ya Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) na kusimamiwa chini ya Bodi ya Mkonge Tanzania.
Kuhusu kiwanda cha chai, alieleza kuwa serikali inakwenda kufunga mitambo mipya ambayo itatumika kuchakata zao la chai.
Amesema mara baada ya kufungwa mashine za kisasa, kiwanda hicho kitaendeshwa chini ya ushirika wa chai Korogwe kupitia usimamizi wa Bodi ya Chai Tanzania.
“Hayo ndiyo ambayo tumejipanga kwa wanakorogwe, nataka niwaambie kwamba, kiwanda cha Tangold chenyewe tutakitupia macho vizuri kuangalia mwekezaji mwingine ambaye anaweza kukiendesha vizuri.
“Kama siyo mwekezaji mwingine, serikali itakichukua chini ya ushirika na kiwanda kile kitafunguliwa kiendeshwe chini ya chama cha ushirika,”alisema.
UJENZI WA MIUNDOMBINU
Dk. Samia, alisema anafahamu wananchi wa Korogwe wana kiu kubwa ya miundombinu ya barabara.
Alisema serikali yake pindi ikipewa ridhaa ya kuliongoza taifa, itazidi kuifungua Korogwe kwa lami.
Alizitaja barabara zitakazoanza ni Soni – Bumbuli – Dindira – Korogwe yenye urefu wa kilometa 74 na barabara ya Old Korogwe – Kwa mndolwa – Magoma – Mashewa – Bombo Mtoni – Mabokweni (kilometa 128) ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
“Tutaendelea kukamilisha utekelezaji wa barabara ya Manundu. Pia, Korogwe kuna mradi mkubwa wa kitaifa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Chongoleani.
“Kwa hiyo hapa (Korogwe) tunakwenda kujitahidi mradi ukamilike tukijua kwamba, Korogwe ni kituo muhimu kwani kuna ajira zitapatikana kupitia mradi huo.
Dk. Samia alisema serikali imezingatia pendekezo la kuanzishwa bandari kavu katika eneo la Old Korogwe kuondoa msongamano wa magari katika Bandari ya Tanga.
Alisema shughuli za uchukuzi zimeongezeka kufuatia maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga.
AKIWA SAME
Akiwa wilayani Same mkoani Kilimanjaro, Dk. Samia alisema fedha nyingi zimetolewa katika wilaya hiyo kwa shughuli za maendeleo.
Vilevile, alieleza kukamilika awamu ya kwanza ya mradi wa Same – Korogwe ambao umeanza kutoa huduma.
“Tunajipanga kwenda na awamu ya pili ambayo tutamalizia kata zilizobaki upande wa Same na kuingia Korogwe,” alisisitiza.
Kuhusu barabara, alisema serikali ilianza ujenzi wa barabara ya Mkomazi – Same yenye urefu wa kilometa 101 ambapo imagawanywa vipande viwili.
“Niwahakikishie tunakwenda kukamilisha barabara hii muhimu kwa usafirishaji mazao ya kilimo.
“Natambua Tarafa ya Mamba kunapolimwa Tangawizi wakati wa mvua ni shida kuteremsha Tangawizi kwenda maeneo mengine kwa hiyo tunakwenda kuzijenga barabara za milimani kwa kutumia zege na lami,” aliongeza.
KATIBU MKUU CCM
Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Asha- Rose Migiro, alisema makubwa yamefanyika katika Mkoa wa Kilimanjaro na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29 mwaka huu kumpigia kura Dk. Samia.
“Tujue kwamba, siku hiyo tunapigia kura maendeleo, tunapigia kura uboreshaji miundombinu, tunapigia kura jitihada ambazo zimefanywa na CCM chini ya Uenyekiti wa Dk. Samia katika kuboresha afya, maji, mazingira bora ya biashara.
“Hayo ndiyo yatakuwa katika boksi la kura Oktoba 29 mwaka huu. Tujitokeze kwa wingi kuhakikisha tunakipa nguvu CCM, tunampa nguvu mgombea wetu Dk. Samia, wabunge na madiwani ili waendeleze kazi nzuri waliyoianza,” alisisitiza.