Na AMINA KASHEBA
ZIKIWA zimebaki siku 13 kuelekea pambano la ‘Boxing On Boxing Day’ mpinzani wa ngumi za kulipwa, Hassan Mwakinyo ametangazwa ni Stanley Eribo kutoka Nigeria.
Mwakinyo atapanda ulingoni kuzichapa na Eribo, katika pambano la raundi 10, lisilo la ubingwa litakalofanyika Desemba 26, mwaka huu katika Ukumbi wa Warehouse, Dar es Salaam.
Akizungumza na UHURU jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Peak Time, Meja Selemani Semunyu ambao ndiyo waandaji wa pambano hilo alisema Mwakinyo atatoana jasho na Mnigeria huyo katika mtanange huo.
“Kila kitu kinaendelea vizuri hivi sasa na mabondia wanaendeleza kufanya mazoezi katika gym zao, Watanzania wengi walikuwa wanahitaji kufahamu mpinzani wa Mwakinyo, ambaye tunamtangaza rasmi ni Eribo,” alisema.
Meja Semunyu aliongeza kuwa mwaka huu, kutakuwa na mapambano mengi zaidi kuhakikisha mabondia mbalimbali wanatoa burudani kwa mashabiki wao tofauti na ilivyokuwa awali.
“Kuna mapambano mengi ambayo kila atayekuja hapo atafurahi kwa sababu maandalizi ni mazuri mno, kila kitu kinaendelea kama kilivyopangwa,” alisema.
Kocha wa Mwakinyo, Kanda Kabongo alisema kwao wako tayari na pambano hilo, hivyo bondia wake anaendelea kufanya mazoezi kuhakikisha anamchakaza mpinzani wake katika raundi za awali.
“Bondia wangu yupo fiti na ninaendelea kumpatia mazoezi ya kutosha kuhakikisha anampiga mpinzani katika raundi za awali.
“Tunatambua pambano litakuwa na upinzani mkubwa kutokana na rekodi za mpinzani, hivyo lazima tufanye maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunaubakisha ushindi nyumbani.
“Watanzania na mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kupata burudani na kumpa sapoti ya kutosha bondia wao,” alisema.
Baadhi ya mabondia wengine ambao watakaopanda ulingoni siku hiyo ni Hamadi Furahisha akizichapa dhidi ya Mmalawi Hanock Phiri, Ally Ngwando na Mussa Makuka, Issa Simba atapepetana na Wilson Phiri kutoka Malawi, huku kwa upande wa wanawake, Hidaya Zahoro atapanda ulingoni na Leila Macho, Debora Mwenda akirushiana makonde na Mmalawi Mariam Dick.




