Na Adv. Ramadhani A. Maleta
- UTANGULIZI
Katika kuhakikisha haki za abiria wanaotumia usafiri wa anga zinalindwa na viwango vya fidia vinaboreshwa, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, hivi karibuni imetunga kanuni au sheria ndogo mpya ya kusimamia taratibu za kisheria za kushughulikia madai ya fidia kwa wahanga wa usafiri wa anga hususan pale inapotokea ajali ya ndege inayosababisha vifo au majeraha ya kimwili kwa abiria.
Kanuni hizi kimsingi ndiyo sheria inayopaswa kutumika hapa nchini katika kushughulikia kesi za madai au migogoro yote inayotokana na safari za ndege zinazofanyika ndani ya mipaka ya Tanzania, ambazo kitaalam zinajulikana kama domestic flights Operations.
Madai au migogoro inayosimamiawa na kanuni au sheria hiyo mpya ni pamoja na yale yanayohusiana na malipo ya fidia kutokana na vifo au majeraha kwa abiria yanayosababishwa na ajali za ndege.
Pia kanuni au sheria hii pia inashughulikia madai ya fidia kwa abiria wanapopata madhara mengine ya kibiashara, kiuchumi na kisaikolojia wakiwa safarini, ikiwemo kupotelewa au kuharibikiwa na mizigo, kuachwa na ndege, abiria kucheleweshwa au kufutwa kwa safari za ndege walizopangiwa na wakati mwingine abiria kukataliwa kusafiri katika ndege aliyopangiwa wakati ana tiketi halali.
Makala hii inaelezea kwa ufupi baadhi ya mambo muhimu yaliyomo katika sheria hiyo mpya ya mwaka 2024.
2.0 KANUNI MPYA ZA FIDIA ZA MWAKA 2024
Kama nilivyogusia katika utangulizi hapo juu, kuanzia mwaka 2024, Tanzania imepata kanuni au sheria ndogo mpya za kusimamia madai na viwango vya malipo ya fidia kwa abiria wanaotumia usafiri wa anga pindi inapotokea ajali ya ndege na kusababisha vifo au majeraha kwa abiria husika.
Kanuni au Sheria hiyo pia inajumuisha haki ya fidia kwa abiria wanaopata madhara mengine, ikiwemo kupata hasara za kibiashara, kiuchumi na kisaikolojia wanapokuwa wanatumia usafiri wa anga kama zilivyoainishwa kwenye utangulizi.
Kanuni au sheria hiyo mpya inajulikana kwa kiingereza kama The Civil Aviation (Carriage by Air) Regulations ya mwaka 2024, ambayo ipo kupitia Tangazo la Serikali (G.N. Na 4 la Mwaka 2024). Sheria hii ndogo ijulikanayo kitaalamu kama Subsidiary Legislation, imetungwa na Waziri wa Uchukuzi ambaye ndiye mwenye dhamana ya masuala ya Usafiri wa Anga hapa nchini, kwa mamlaka aliyopewa na kifungu cha 4 cha Sheria ya Usafiri wa Anga ijulikanayo kama The Civil Aviation Act, (Cap 80, R.E. 2024 ).
Ifahamike pia kwamba, kanuni au sheria hii mpya ya mwaka 2024 inaifuta na kuchukua nafasi ya kanuni au sheria iliyokuwepo awali ambayo ilijulikana kama The Civil Aviation (Carriage by Air) Regulations, ya mwaka 2008 ambayo pia ilikuwa sheria ndogo iliyotungwa na Waziri wa Uchukuzi.
Pia ifahamike kwamba kanuni au sheria hii mpya ya mwaka 2024 kama ilivyokuwa kwa kanuni au sheria iliyopita ya mwaka 2008, inatumika hapa nchini kwa kusimamia madai ya fidia yanayotokana na safari za ndege zinazofanya shughuli zake ndani ya mipaka ya Tanzania (domestic flights), kwa mfano ndege zinazotoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine pasipo kutoka nje ya mipaka ya nchi.
Hii maana yake ni kwamba, kwa madai ya fidia yanayohusiana na ndege zinazofanya safari za kimataifa (international flights) kwa kuvuka mipaka ya Tanzania, kanuni au sheria hii ya mwaka 2024 haitumiki pindi madai au migogoro ya fidia kwa abiria wanaotumia ndege kama hizo za kimataifa yanapojitokeza. Badala yake, kuna sheria nyingine tofauti inayotumika kushughulikia madai yanayotokana na ndege kama hizo zinazofanya safari za kimataifa ijulikanayo kama Mkataba wa Kimataifa wa Montreal wa mwaka 1999, maarufu kama The Montreal Convention of 1999.
Ifahamike kwamba, mkataba huu wa mwaka 1999 ndiyo sheria ya kimataifa ambayo inampa haki raia wa nchi yoyote wakiwemo Watanzania kudai fidia dhidi ya shirikika la ndege la nchi yoyote linapopata ajali popote duniani wakati likifanya safari za kimataifa na mtu huyo kupata ajali inayopelekea kifo au majeraha akiwa ni mmoja wa abiria katika ndege husika.
Kwa bahati nzuri, ili kumrahisishia abiria kama huyo kuepukana na gharama na mambo mengine yanayoweza kumfanya ashindwe kumudu kuendesha kesi kama hiyo katika mahakama za nchi za nje, Mkataba huo wa mwaka 1999 kama sheria ya kimataifa, unampa haki abiria kama huyo chini ya kifungu cha 33 kufungua kesi dhidi ya shirika la ndege husika katika mahakama ya nchi ambayo abiria husika amekuwa akiishi, pasipo kujali uraia wa abiria huyo. Pia haijalishi kama ni wapi ajali husika ilitokea na shirika la ndege husika ni la nchi gani.
3.0 KIWANGO CHA FIDIA KWA VIFO NA MAJERAHA
Kwa mujibu wa kifungu cha aircraft cha 18(1) cha Kanuni au Sheria hii mpya ya mwaka 2024, abiria atastahili kulipwa fidia pale mambo yafuatayo yatakapothibitika: (i) kwamba ajali husika ya ndege imetokea, (ii) kwamba ajali hiyo imesababisha vifo au majeraha kwa abiria; na (iii) kwamba abiria husika walikufa au kupata majeraha ya kimwili (bodily injuries) wakiwa ndani ya ndege husika (on board the aircraft) au wakiwa katika mchakato wa kupanda au kushuka katika ndege husika (in the process of embarking or disembarking). Pindi mambo hayo matatu yatakapothibitika, mwenye ndege hatakuwa na chaguo au utetezi wowote zaidi ya kuwajibika (strictly liable) chini ya kifungu cha 29 (1) kulipa fidia inayofikia fedha za kitanzania sawa na Special Drawing Rights (SDR) 100,000 kwa kila abiria aliyekufa au kujeruhiwa katika ajali hiyo. SDR ni fedha ya kimataifa ambayo thamani na kiwango chake kinapangwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) SDR kama hizo 100,000 zinafikia Dola za Kimarekani 120,000.
Hii maana yake ni kwamba kiwango cha fidia tajwa hapo juu kitalazimika kulipwa na mwenye ndege inapothibitika tu kwamba ajali ya ndege imetokea na kusababisha vifo au majeraha kwa abiria. Hii haijalishi kama ajali husika ilisababishwa na makosa au uzembe wa wenye ndege au hapana, kwani kigezo pekee kinachomwajibisha mwenye ndege kulipa fidia hiyo ya SDR 100,000 kila abiria ni uthibitisho wa uwepo wa ajali ya ndege na vifo au majeraha kwa abiria.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 29(2) kama abiria au ndugu wa marehemu hawataridhika na kiwango hicho kilichowekewa ukomo (limited claim) cha fidia ya SDR 100,000 na wakaamua kudai malipo zaidi ya hayo, sheria hiyo inatoa haki kwa watu kama hao kuwasilisha mahakamani madai ya kuomba malipo ya fidia ya ziada kwa kiwango chochote (unlimited claim) kadri wanavyoona inafaa. Hata hivyo, ili mtu kama huyo aweze kufanikiwa kulipwa malipo kama hayo ya fidia ya ziada, atalazimika kuithibitishia mahakama kwamba ajali husika ilisababishwa na ama kutowajibika (omission) au uzembe (negligence) wa ama mwenye ndege, watumishi wake au mawakala wake.
Kwa upande mwingine, mwenye ndege naye ana haki ya kujitetea katika hatua hii kwa kupinga kulipa malipo kama hayo ya fidia ya zaidi ya SDR 100,000 kwa kuithibitishia mahakama kwamba yeye kama mmiliki wa ndege husika pamoja na watumishi au mawakala wake, waliwajibika ipasavyo kuhakikisha usalama wa ndege na abiria wake na hawakuhusika na uzembe wa aina yoyote uliopelekea kutokea kwa ajali na vifo au majeraha husika. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 29(2)(a) cha kanuni au sheria hiyo ya waka 2024.
Mbali na utetezi kama huo, mwenye ndege anaweza pia chini ya kifungu cha 29(2)(b), kukwepa adhabu kama hiyo ya kutakiwa kulipa fidia ya ziada, kama ataithibitishia mahakama kwamba, ajali husika ilisababishwa na mtu mwingine (a third part) ambaye hana mahusiano naye na hakuwa na uwezo wa kumdhibiti. Kwa mfano ajali inaposababishwa na shambulio la kigaidi.
Lakini pia mwenye ndege atajiokoa katika kutakiwa kulipa malipo kama hayo ya fidia ya ziada, kama atajitetea kwa kuithibitishia mahakama kwamba kifo au majerha ya abiria husika vilichangiwa na uzembe wa abiria mwenyewe (contributory negligence). Kwa mfano, kama wahudumu wa ndege walitoa ilani ya hatari na kuwataka abiria wote kutulia katika viti vyao na kufunga mikanda, lakini abiria husika alikaidi maelekezo hayo kwa kutofunga mkanda na hatimaye kupata madhara, hawezi kulipwa fidia kama hiyo ya ziada, kwa vile kisheria anachukuliwa kuwa alifanya uzembe uliochangia madhara yaliyompata.
Wiki ijayo tutaendelea kuangalia sheria hiyo mpya katika vipengele vya fidia kwa upotevu na uharibufu wa mizigo ya abiria pamoja na abiria kucheleweshwa safari au kufutwa kwa safari za ndege.




