NA MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi na kutengua viongozi mbalimbali ambapo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene na Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Profesa Eliakimu Zahabu, uteuzi wao umetenguliwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka kisha kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu ilisema Patrobas Katambi ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kabla ya uteuzi huo, Katambi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, akichukua nafasi ya Simbachawene ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Pia, taarifa hiyo ilisema Profesa Palamagamba Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum). Kabla ya uteuzi huo, Profesa Kabudi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Vilevile, taarifa hiyo ilieleza kuwa Paul Makonda ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo kabla ya uteuzi huo, Makonda alikuwa Naibu waziri katika wizara hiyo.
Kadhalika, Dennis Londo ameteuliwa kuwa Naibu Waziri, Viwanda na Biashara ambapo kabla ya uteuzi huo Londo alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Ayoub Mohamed Mahmoud ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Richard Muyungi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akichukua nafasi ya Mhandisi Cyprian Luhemeja ambaye ameteuliwa kuwa balozi.
Aidha, Mhandisi Zena Ahmed Said ameteuliwa kuwa Balozi, Waziri Salum ameteuliwa kuwa Balozi, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy ameteuliwa kuwa Balozi huku Mhandisi Ally Samaje ameteuliwa kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
Mhandisi Samaje anachukua nafasi ya Dk. Mussa Daniel Budeba huku uteuzi wa Profesa Eliakimu Zahabu, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) umetenguliwa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa uapisho wa viongozi wateule utafanyika Januari 13 mwaka huu, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma kuanzia saa 8.00 mchana.




