NA ATHNATH MKIRAMWENI
CHANGAMOTO kwa mwanamke kutozaa imekuwa ni mfupa mgumu kwao, baadhi ya ndoa zimevunjika, wengine wamepata ulemavu wa kudumu kutokana na vipigo kutoka kwa waume zao.
Baadhi ya wanawake wamekumbana na matukio ya ukatili wa kijinsia na wengine wametengwa na jamii kwa kukosa uzazi.
Ukweli ni kwamba katika hali ya kawaida hakuna mwanamke asiyependa kupata mtoto, lakini kutokana na mipango ya Mungu wapo waliokosa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiafya.
Hata hivyo, wapo wanawake walipata madhira ya kutengwa, kunyanyaswa na kufanyika vitendo vya ukatili kwa kutopata mtoto, ingawa mwenye tatizo ni mwanaume.
Kutokana na mfumo dume, wanaume haamini kama wao pia ni chanzo cha mwanamke kutozaa, lakini mara nyingi ukweli huo hupindishwa kutokana na sababu mbalimbali, huku mzigo mkubwa akiangushiwa mwanamke.
Kufuatia kadhia hiyo anayopitia mwanamke Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imepata mwarobaini wa kumpunguzia mzigo wa lawama mwanamke.
Iko hivi. Hospitali ya Taifa Muhimbili imeanzisha huduma ya upandikizaji mimba ambayo imeanza kufungua ukurasa mpya wa matumaini kwa wanawake wenye changamoto ya uzazi.
Katika kuthibitisha hilo, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na mbobezi wa upasuaji bila kufungua tumbo wa Muhimbili, Dk. Vincent Tarimo, alisema kuanzishwa huduma hiyo, ni jibu sahihi kwa kilio cha muda mrefu kinachowapata wanawake au ndoa zenye changamoto ya kutopata mtoto.
Akizungumza na UHURU jijini Dar es Salaam, Dk.Tarimo alisema hospitali ilichukua uamuzi wa kuanzisha huduma hiyo, baada ya kubaini ongezeko kubwa la wagonjwa wanawake waliofika kliniki kutopata ujauzito.
Alisema katika kliniki za wagonjwa wa nje, idadi ya wanawake wenye changamoto ya uzazi imekuwa kubwa kiasi cha kuashiria tatizo la kitaifa.
Alisema kufuatia changamoto hiyo, tatizo la utasa kwa wanawake halipaswa kuachwa mikononi mwa hospitali binafsi au mgonjwa kwenda nje ya nchi kufuata matibabu, hivyo Muhimbili waliona ni vyema kuanza kutoa huduma hiyo.
UZINDUZI WA HUDUMA
Dk. Tarimo alisema huduma ya upandikizaji mimba Muhimbili ilizinduliwa Septemba 22, 2024, baada ya maandalizi ya muda mrefu ya kitaalamu, miundombinu na rasilimali watu.
Uzinduzi wa huduma hiyo uliashiria hatua mpya katika huduma za uzazi nchini, hususani kwa hospitali ya umma inayohudumia wananchi wa makundi yote.
CHANZO CHA TATIZO
Dk. Tarimo alisema tatizo la utasa linaongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na mabadiliko ya maisha ya sasa ndani ya jamii.
Daktari huyo alisema ulaji usiozingatia afya, matumizi ya vyakula vyenye kemikali, msongo wa mawazo, magonjwa ya mfumo wa uzazi na kuchelewa kuanza uzazi ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia utasa kwa mwanamke.
Aliongeza wanaume pia wamekuwa sehemu ya tatizo, ingawa kwa muda mrefu jamii imekuwa ikipeleka lawama zote kwa wanawake.
Dk. Tarimo alisema huduma ya upandikizaji mimba inawahusu wanawake wote waliofikia umri wa kupata ujauzito, endapo afya zao zinaruhusu.
Alisema sharti kuu ya kupata huduma ni kuwa na mfuko wa uzazi unaoweza kubeba mimba na mayai yanayotosheleza.
Dk. Tarimo alifafanua hakuna umri unaomzuia mwanamke kupata huduma ya upandikizaji, ingawa uwezekano wa kufanikiwa hupungua kadri umri unavyoongezeka.
Hata hivyo, Dk. Tarimo alidokeza kisayansi wanawake vijana hupata matokeo bora zaidi, ikilinganishwa na wanawake wenye umri mkubwa.
MAFANIKIO
Dk. Tarimo alisema tangu huduma ilipoanza kutolewa, wanawake 22 waliingia katika mchakato wa upandikizaji mimba.
Alifafanua kati ya wanawake 22, mimba mbili zimethibitishwa na watadumu na ujauzito kwa miezi tisa kabla ya kujifungua huku wengine wakiendelea na hatua mbalimbali za maandalizi na ufuatiliaji.
Dk. Tarimo alisema mafanikio hayo ya awali, yanaonesha kuwa huduma hiyo ina manufaa na mustakabali mzuri.
SAFARI YA MATIBABU
Dk.Tarimo alielezea uhalisi wa safari ya kitabibu akisema upandikizaji mimba siyo huduma ya haraka kama wengi wanavyofikiri, ni mchakato mrefu unaohitaji uvumilivu.
Mchakato huanza kwa kumpa mwanamke dawa za kusawazisha mzunguko wa hedhi na hatua inayofuata ni matumizi ya dawa za kuchochea uzalishaji wa mayai mengi, badala ya yai moja la kawaida.
Alisema mayai hayo hukuzwa kwa uangalizi wa karibu kwa kutumia vipimo vya kitaalamu na baada ya kufikia kiwango kinachotakiwa, hufanyika zoezi nyeti la uvunaji wa mayai kwa ratiba maalumu.
Dk. Tarimo alisema kitendo cha kuchelewa hata ndani ya muda mfupi kunaweza kuharibu mchakato mzima na kuathiri upandikizaji.
WANAUME WANAHUSIKA
“Huduma ya upandikizaji haiwahusu wanawake pekee, wanaume pia wana mchango mkubwa katika changamoto za uzazi.
“Wanaume wengi hukutwa na mbegu chache, zisizokimbia vizuri au zenye maumbo yasiyo ya kawaida
“Safari ya mbegu kufikia kuwa yai ni kama watu wengi wanaotafuta mtu mmoja katikati ya jiji kubwa, kwa sababu hiyo teknolojia ya ICSI hutumika kusaidia pale mbegu zinapokuwa dhaifu,”alifafanua daktari huyo.
NAMNA YA UPANDIKIZAJI
Alisema baada ya yai kutungwa, kijusi hukuzwa kwa siku chache, kabla ya kupandikizwa kwenye mfuko wa uzazi.
“Wakati mwingine kijusi hugandishwa kwa muda ili kumpa mwanamke nafasi ya kuandaliwa upya kiafya, idadi ya vijusi vinavyopandikizwa huamuliwa kwa tahadhari kubwa, ikizingatia umri wa mwanamke na hali yake ya afya,” alisema Dk. Tarimo.
Dk. Tarimo alisema lengo ni kuepuka hatari za mimba nyingi ambazo zinaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.
GHARAMA
Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Tarimo, gharama ya huduma ya upandikizaji mimba Muhimbili ni wastani sh. milioni 14, ikilinganishwa na gharama kubwa inayotozwa katika hospitali binafsi.
Dk. Tarimo alisema gharama hiyo inashughulikia mchakato mzima wa kitabibu wa upandikizaji kutoka kwenye uchunguzi wa mwanzo, utoaji wa dawa za kusawazisha, kuchochea mayai, uvunaji wa mayai, uchanganyaji mayai na mbegu, hadi upandikizaji wa kijusi na ufuatiliaji wa awali wa ujauzito.
“Gharama za huduma hiyo Muhimbili ni nafuu ikilinganishwa na hospitali binafsi, gharama hizo zinalenga kufidia dawa na vifaa, si kutengeneza faida.
“Gharama hii inalenga kulipia huduma na rasilimali kama dawa maalumu za kusawazisha mzunguko wa hedhi na kuchochea uzalishaji wa mayai, ambazo mara nyingi ni ghali kutokana na teknolojia ya homoni inayotumika.
“Vipimo vya kitabibu vinavyohitajika mara kwa mara, ikiwemo uchunguzi wa mzunguko wa mayai, homoni na ‘ultra sound’ za kufuatilia ukuaji wa mayai,” alisema Dk. Tarimo.
Alisema operesheni ya uvunaji wa mayai na maabara za IVF ambapo vifaa maalumu vya kisayansi na wataalamu bingwa hutumika. Pia dawa baada ya upandikizaji ambazo zinasaidia mfuko wa uzazi kujiandaa kupokea kijusi.
HOSPITALI BINAFSI
Alisema gharama ya huduma ya upandikizaji mimba Muhimbili ni nafuu ikilinganishwa na hospitali binafsi, ambapo baadhi zinafikia zaidi ya sh. milioni 20 au zaidi kwa mzunguko mmoja wa IVF.
Dk. Tarimo aliweka wazi kuwa gharama hizo katika hospitali binafsi hutokana na nyongeza za ada za huduma, vifaa binafsi na rasilimali, jambo ambalo halipaswi kuwa kikwazo kwa wagonjwa wa huduma ya umma.
“Muhimbili huduma hii ni ya serikali, hatulengi faida, gharama hii inalenga tu kufidia matumizi ya dawa, vifaa na kazi ya wataalamu,”alisema.
Dk. Tarimo alidokeza lengo la gharama ni kuhakikisha huduma hiyo inakuwa nafuu iwezekanavyo kwa wananchi wa matabaka mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
AlisemaHospitali ya Muhimbili inafanya kazi ya ushirikiano na taasisi za bima, kupata mbinu za kulifanyia kazi suala la gharama kuwa rahisi kwa wagonjwa.
“Hii inatarajiwa kusaidia wanachama wa bima kupata fidia au malipo ya baadhi ya gharama ya huduma ya upandikizaji mimba bila mzigo mkubwa wa fedha kwa mtu mmoja mmoja,” alisema.
CHANGAMOTO
Alitaja moja ya changamoto kubwa inayoongeza gharama ni upatikanaji dawa na vifaa vinavyoharibika haraka, kwa sababu vinatumika ndani ya muda mfupi.
“Hii inahitaji mipango ya kitaalamu ya ununuzi, usimamizi wa hisa na upangaji wa wagonjwa kwa makundi kuhakikisha vifaa vinatumiwa kabla ya muda wake kumalizika,” alisema.
Alisema wagonjwa na familia zinazopitia huduma hiyo, gharama ya sh. milioni 14 inaweza kuonekana kubwa, lakini kwa kulinganisha na safari za nje ya nchi au hospitali binafsi, inaonekana ni chaguo la gharama nafuu na lenye tija.
“Wengi waliowahi kulazimika kutafuta huduma nje ya nchi kwa gharama kubwa bila mafanikio, sasa wanaweza kupata huduma hiyo ndani ya nchi kwa gharama inayofaa kwa wataalamu wenye uzoefu,”alisema.
MATARAJIO
Hospitali ya Taifa Muhimbili inalenga kupanua huduma ya upandikizaji mimba na kuimarisha teknolojia ya uzazi wa kisasa.
Alisema lengo kubwa ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayelazimika kwenda nje ya nchi kutafuta huduma hiyo. Pia Muhimbili inalenga kuwa kioo cha taifa katika huduma za afya ya uzazi.
“Tunataka kuona familia nyingi zaidi zikirejesha tabasamu kupitia huduma hii,” alisema.
Vilevile, ina matarajio ya kuendelea kuboresha huduma hiyo ikiwemo kushirikiana na bima na wadau wa afya gharama ipungue bila kuathiri ubora wa huduma.
Dk. Tarimo alieleza ana imani gharama itakuwa nafuu na itafikiwa na idadi kubwa ya wananchi, hasa upatikanaji wa dawa na teknolojia mpya.
ELIMU YA AFYA
Dk. Tarimo alisema mwitikio wa jamii umeendelea kuwa mzuri, huku idadi ya wanaohitaji huduma hiyo ikiongezeka kila mwezi.
Elimu kwa jamii imekuwa muhimu kuondoa dhana potofu upandikizaji mimba ni kinyume na maumbile au una madhara.
Daktari huyo aliwahakikishia Watanzania kuwa huduma hiyo ni salama na inafanyika kwa kuzingatia miongozo ya kitabibu ya kimataifa.
WITO KWA JAMII
Dk. Tarimo alitoa wito kwa Watanzania kuondoa dhana potofu kuhusu huduma ya upandikizaji mimba.
Alisisitiza kuwa huduma hiyo ni ya kitabibu na haina madhara kwa mama au mtoto.
Dk. Tarimo alisema ni muhimu jamii kuelewa upandikizaji mimba ni suluhisho la kisasa, linalolenga kusaidia wananchi kupata watoto bila hatari.
Aidha, aliwahimiza wanaume na wanawake walioko katika umri wa kupata watoto, ambao wana mbegu na mayai bora kwenda hospitali kupata huduma hiyo, huku akisisitiza kuhesabu umri au ubora wa kizazi ni sehemu ya kuhakikisha mafanikio ya mchakato.
Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha Watanzania hawalazimiki kwenda nje ya nchi kutafuta huduma hiyo.
WANAUME KUTOA MBEGU
Dk. Tarimo aliwahimiza wanaume kutoa mbegu zinapokidhi vigezo vya kitabibu kusaidia wenza zao kupata ujauzito.
Alisisitiza ushirikiano wa kila mmoja ni muhimu kufanikisha mchakato wa upandikizaji mimba, kwa kuwa lengo ni kuona Mtanzania anayehitaji huduma hiyo anaipata nchini.
USHUHUDA WA WANANCHI
Kwa upande wake Flora Urio (siyo jina lake halisi) alisema yupo ndani ya ndoa miaka 15 na amepima vipimo vingi vikimwonesha hana tatizo la uzazi, lakini hajazaa.
“Ninapongeza uwepo huduma ya upandikizaji mimba hapa nchini, italeta suluhu kwa sisi wenye changamoto za uzazi, namwomba Mungu anijalie kipato niende kupata huduma hii, kwa kweli natamani sana kushika mimba,” alisema.
Alisema amekuwa akipitia manyanyaso mengi kutoka kwa familia ya mume wake, kutokana na hali yake, lakini anaonesha tumaini kuwa atafikia huduma ya upandikizaji akipata fedha.
Sarafina John (siyo jina lake halisi) alipongeza serikali kuanzisha huduma hiyo, lakini aliiomba ipunguze gharama iwe nafuu ili kila Mtanzania mwenye changamoto amudu.
Mzazi huyo alisema ana matumaini siku moja atapokea muujiza wake wa mtoto kupitia huduma ya upandikizaji ambayo itakuwa mwisho wa machozi yake.




