Na NASRA KITANA
IKIWA imesalia siku moja ili kushuka dimbani katika mchezo wake dhidi ya Esperance De Tunis ya Tunisia, wachezaji wa Simba wametoa msimamo kuwa watahakikisha wanashinda ili kuwapa furaha mashabiki wao.
Simba ipo nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wake wa tatu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa katika Uwanja wa Stade Olympique Hammadi mechi zote zikichezwa saa 1:00 usiku.
Wekundu hao wa msimbazi, wapo kundi D ikiwa inaburuza mkia huku Esperance ikiwa na pointi mbili baada ya kupata sare katika mechi mbili za awali na kushika nafasi ya tatu.
Wakizungumza jana kutoka nchini Tunisia kwa nyakati tofauti, nyota wa timu hiyo, Shomari Kapombe alisema wanajua wanatakiwa kushinda ili kuwapa furaha mashabiki wao baada ya hivi karibuni kupata matokeo ambayo si mazuri.
“Hatujapata ushindi katika mechi zetu mbili, lakini tutahakikisha tunapambana ili kushinda katika mchezo huu dhidi ya Esperance na kupata mwanga wa kusonga mbele,”alisema.
Mlinzi huyo alifafanua kuwa wanajua mchezo huo utakuwa mgumu wenye ushindani mkubwa lakini hawatakubali kupoteza.
“Tutajitoa kwa hali na mali ili kupata ushindi, lengo tusonge mbele huku tukiwapa furaha mashabiki wetu,” alisema
Kapombe aliongeza kwamba watatumia uzoefu waliokuwa nao katika mashindano ya kimataifa ili kupata ushindi na kujizolea pointi tatu muhimu.
“Utakuwa mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa lakini tutapambana kufa au kupona ili kupata ushindi, lengo letu ni kupata pointi tatu,” alisema Kapombe.
David Kameta ‘Duchu’ alisema kuwa wachezaji wote wamejipanga kupambana kwa jasho na damu ili kupata ushindi.
Alisema kwamba wanawaheshimu wapinzani wao na wataingia katika mchezo huo, wakicheza kwa nidhamu kubwa ili kushinda.
“Tunaenda katika mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa, hatutakubali kupoteza tutapambana kwa jasho na damu ili kupata matokeo mazuri,” alisema Duchu.
Hata hivyo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally alisema kuwa timu yao imefika salama Tunisia na tayari wameanza maandalizi kwa ajili ya mchezo huo muhimu.
“Timu imefika salama Tunisia na mwalimu ameshaanza programu ya mazoezi kwa ajili ya mchezo huo muhimu, wachezaji wote wana morari ya kutosha kuhakikisha wanapata ushindi na kurejea na pointi tatu nyumbani,” alisema Ahmed.
Baada ya mchezo huo, Simba itarejea nyumbani kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Esperance utakaochezwa Februari Mosi, mwaka huu jijini Dar es Salaam.




