NA EMMANUEL MOHAMED
SHIRIKA la Masoko ya Kariakoo, limeanza kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipofungua Soko Kuu Jipya la Kariakoo Februari 8, mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Meneja Mkuu wa shirika hilo, Ashraph Abdulkarim, alipozungumza na Uhuru.
Abdulkarim amesema katika kutekeleza maelekezo hayo tayari uongozi umewasilisha maombi ya fedha kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kujenga kituo hicho cha kulelea watoto.
“Miongoni mwa maelekezo ambayo Rais Dk. Samia aliyatoa ni kutenga eneo hilo ambalo tushirikiane na sekta binafsi katika kutoa huduma hiyo na hii inatokana na kuwa, katika soko letu tumejenga eneo la kunyonyeshea watoto, hivyo akataka twende mbali zaidi tuwe na eneo maalumu la kulelea watoto,”amesema.
Meneja Mkuu huyo amesema maelekezo mengine ambayo yameanza kufanyiwa kazi ni kuhakikisha bidhaa zinazoingia sokoni hapo zinazingatia viwango vyenye ubora ambapo tayari uongozi wa soko imewapatia ofisi ndani ya soko hilo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA).
“Rais Dk.Samia alitutaka tuhakikishe bidhaa zinazoingizwa na kuuzwa hapa zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa kulinda afya ya watumiaji na hadhi ya soko letu, hivyo tayari tumewapa ofisi tulilifanyia kazi agizo hilo,”alisema.
Alitaja maelekezo mengine ambayo uongozi wa soko umeyafanyia kazi ni matumizi ya mifumo ya kidijitali ambayo itawasaidia wafanyabiashara kujulikana ambapo wameanza kutumia mfumo wa TAUSI.
“Tumetengeneza kanzidata ambapo wafanyabiashara wote wameingizwa katika mfumo wa TAUSI na wafanyabiashara 1,520 wameshasajiliwa na wengine ambao wanataka kuomba kufanya biashara sokoni hapa wanapaswa kutumia mfumo huo,”alisema
Alisema agizo lingine ambalo wamelifanyia kazi ni kuhakikisha uwepo wa usalama wa bidhaa za wafanyabiashara ambapo tayari wamewapatia ofisi ndani ya soko hilo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
“Rais Dk.Samia alitutaka tuhakikishe kuwa bidhaa za wafanyabiashara zinakuwa katika hali ya usalama, tumeamua kuwapatia ofisi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili janga lolote la moto likitokea lidhibitiwe kwa haraka,”alisema
“Kuhusu agizo la Rais Dk.Samia la tozo za wafanyabiashara tutakaa nao kujadiliana kuona namna gani ya kuweka kiwango nafuu,”alisema
Februari 8, mwaka huu, Rais Dk.Samia alizindua soko hilo na kutoa maagizo kwa uongozi wa Soko Kuu la Kariakoo , kulifanya soko hilo liaminike ndani na nje.
Miongoni mwa maagizo hayo ni kutenga eneo maalumu la kulelea watoto kwa kinamama wafanyabiashara, kuhakikisha bidhaa zinazoingia sokoni hapo zinazingatia viwango vyenye ubora, matumizi ya mifumo ya kidijitali, uwepo wa usalama wa bidhaa za wafanyabiashara.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema katika soko hilo zaidi ya wafanyabiashara 1,500 wanatarajiwa kufanya biashara.




