>>> UWEKEZAJI, MIUNDOMBINU, MASHIRIKA YA UMMA YALETA MAGEUZI
Na Hamis Shimye na Hanifa Ramadhani
SIKU 100 za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi zimeendelea kuonyesha uongozi safi na wenye malengo kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na maendeleo makubwa yaliyopatikana kwa kasi kubwa.
Serikali ya awamu ya nane imedhamiria kuongeza kasi ya uwekezaji, kuboresha mashirika ya umma na ujenzi wa miundombinu kwa kuweka nguvu zaidi kwa kuwavutia wawekezaji kuwekeza kwa wingi zaidi visiwani Zanzibar.
UWEKEZAJI
Siku 100 zimekuwa Dk. Mwinyi imekuwa na mafanikio katika sekta ya uwekezaji ambapo serikali imeanza mikakati ya kuwa na miradi 150 ya uwekezaji kila mwaka katika kipindi chote cha miaka mitano.
Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif, alisema hatua hiyo inalenga kufikisha miradi isiyopungua 750 ifikapo mwisho wa kipindi cha uongozi wa Dk. Mwinyi kuhitimisha miaka 10 ya uongozi wake.
Alisema ongezeko la miradi nchini limechangiwa na mabadiliko ya sera na miongozo iliyowekwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambapo mwaka 2024/2025 pekee miradi 137 iliwekezwa Zanzibar kwa mtaji wa zaidi ya dola milioni 700.
“Kiwango hiki kwa mwaka mmoja ni kikubwa, katika miaka mitano iliyopita tulikaribia miradi 600, hii inaonesha dhamira ya serikali kuvutia wawekezaji zaidi,” alisema.
Alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa mageuzi aliyoyafanya katika wizara hiyo, kupitia ZIPA na miradi ya PPP, hatua iliyowezesha taasisi kuweka vipaumbele na malengo yanayotekelezeka.
Akizungumzia kipaumbele kwa miradi mikubwa na yenye tija alisema serikali imeweka mkazo katika miradi hiyo ambayo inaleta ajira na kuongeza mapato ya nchi.
Alisema sehemu kubwa ya miradi hiyo ipo katika sekta ya utalii kutokana na mvuto wa visiwa vya Zanzibar.
Alitoa mfano wa kisiwa cha Bawe, kilichowekezwa kwa zaidi ya dola milioni 30 na malazi yanayofikia hadi dola 300 kwa siku, alisema hiyo ndio aina ya miradi inayolenga watalii wa hali ya juu.
MAENEO HURU YA KIUWEKEZAJI
Akizungumzia dhana waliyokuja nayo sasa ya maeneo huru ya kiuchumi alisema serikali imetenga maeneo maalum ya Fumba kwa ajili ya uwekezaji wa masuala ya kidijitali.
Alisema pia kuna mikakati ya kuhakikisha kwamba miradi hasa ya ujenzi wa nyumba za biashara nayo inapata msukumo.
“Ukiangalia hisabu ambazo tunazo zinaonesha kwamba ukimaliza utalii inayofuata ni real state mali isiyohamishika kwani karibu asilimia 18 ya miradi inayokuja ZIPA ni hiyo,” alisema
Alisema miradi hiyo pia inapewa msukumo kwani ni ya kitajiri na pesa zao watazitumia hapa na itatoa ajira ndani yake.
Waziri Sharif alibainisha kuwa sekta ya viwanda vya kati pia imepewa msukumo, ikiwemo usarifu wa mwani, karafuu, nyama, mazao ya baharini, tungule na viwanda vya vifaa vya kielektroniki.
“Zanzibar ina bidhaa nyingi ambazo zinaweza kusarifiwa ikiwemo tungule, viungo na vyakula vyengine ambavyo vinaweza kusarifiwa na hata mazao ya baharini,” alisema.
Alifahamisha kuwa pia serikali inalenga kukuza uchumi wa buluu kupitia ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, itakayokuwa na bandari tano ikiwemo ya makontena, mafuta na gesi, na utengenezaji wa meli.
“Bandari hii itaziwezesha meli kubwa kushusha bidhaa zao Zanzibar na kusafirisha nchi nyengine za kiafrika,” alibainisha.
Alieleza kuwa tayari mwekezaji mmoja amepatikana Micheweni kwa ajili ya mradi wa gati maalum la uvuvi na kiwanda cha usarifu.
Kwa upande wa miradi ya PPP na vivutio kwa wawekezaji alisema serikali inafungua milango kwa wawekezaji kuja kushirikiana katika eneo hilo lengo ni kuona kipauimbele ni miradi inayotoka katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo.
“Bado tuna miradi ambayo tunataka kushirikiana nao ikiwemo uwanja wa ndege Kigunda, Uwanja wa ndege wa Kitataifa wa Abeid Amani Karume ambapo lengo la serikali ni kutengeneza taminal 1V hivyo watajenga wao kwa mujibu wa makubaliano,” alisema.
Aidha, serikali imeongeza vivutio vya kodi na visivyo vya kodi, ambapo mwekezaji mwenye mtaji kuanzia dola milioni 50 visiwani Unguja au milioni 10 Pemba anapewa hadhi ya mradi mkakati.
“Zanzibar ni mahali salama na rafiki kwa uwekezaji, tumeondoa vikwazo vingi, ikiwemo vibali vya muda mfupi, hii ni kuonesha kuwa serikali ipo tayari kushirikiana na sekta binafsi,” alisema.
Alisisitiza kuwa licha ya changamoto za dunia kama vita Ulaya na Mashariki ya Kati, Afrika sasa inaonekana kuwa kitovu kipya cha uwekezaji, na Zanzibar inanufaika kutokana na amani iliyopo.
Aliwataka wawekezaji wa ndani na nje kutazama fursa za uwekezaji, kwani serikali ipo tayari kushirikiana nao, imeshaondoa vikwazo vingi ikiwemo upatikanaji wa vibali vya muda mfupi kwa ajili ya uwekezaji.
Alisema pia inawakabirisha wawekezaji wanaokuja na miradi yao na akiwa na mtaji wa dola milioni 50 kwa Unguja na Pemba dola milioni 10 na kupewa hadhi ya kuwa miradi ya kimkakati.
Aliahidi kuwa Wizara itaendelea kusimamia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030, maagizo ya Rais aliyatoa katika hotuba zake kwani maeneo hayo ndio yanayotakiwa kufanyiwa kazi na kuhakikisha wanayatekeza vizuri ili azma ya serikali inafikiwa na wananchi wanaendelea kupata maendeleo.
Mbali na hayo, Shariff alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi kwa dhamira yake njema ya kuifanyia mabadiliko wizara hiyo ili kuhakikisha uwekeza unaongezeka Zanzibar.
Alisema, kupitia taasisi ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na miradi ya serikali kupitia dhana ya PPP, kila taasisi ni lazima ije na mpango ambao utaonesha kwa kipindi kifupi utekelezaji ambao una mafanikio makubwa.
UJENZI NA UCHUKUZI
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohammed alisema siku 100 zimekuwa na msingi bora wa utekelezaji wa miradi mbali mbali ya kimkakati ambayo itazidi kuvifungua visiwa vya Zanzibar kiuchumi.
Alisema, sekta ya usafirishaji ni sekta muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi na ndiyo maana serikali imedhamiria kuimarisha sekta hiyo kwa kujenga miundombinu ya barabara, madaraja ya juu (fly over), kujenga, kuimarisha na kutanua viwanja vya ndege, kujenga bandari mpya na kuimarisha zilizopo.
“Kukamilika kwa miradi hiyo mikubwa itachochea uchumi wa Zanzibar na wananchi pia watanufaika, ajira zitapatikana maisha yataimarika na haiba ya mji wa Zanzibar utaimarika sana,” alisema
Alisema,Wizara ya Ujenzi katika kipindi cha awamu ya pili ya uongozi wa serikali ya awamu ya nane imejipanga kwenda na kasi ya Dk. Mwinyi na kuhakikisha kuwa inatekeleza kikamilifu vipaumbele vya Wizara hiyo na serikali kwa ujumla.
Alibainisha kuwa, Wizara yake imejipanga vizuri na inaandaa mkakati wa utekelezaji wa miradi yote na kuhakikisha kuwa miradi inakamilika kwa wakati sahihi na wenye kutoa mwelekeo thabiti wa kiuchumi.
“Kwa hivyo huo mpango mzima utakapokamilika utaonyesha dira nzima ya utekelezaji wa miradi yote hiyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo, na hilo linawezekana,”alisema
Alisema, katika kipindi hiki cha awamu ya pili ya serikali ya awamu ya nane, vipaumbele vya Wizara vimejikita katika maeneo manne ikiwa ni pamoja ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwakia 2025/2030, mpango wa maendeleo wa Zanzibar, ahadi za Dk. Mwinyi alizozitoa wakati wa kampeni na dira ya maendeleo.
KUIMARISHA HUDUMA ZA USAFIRI NA USAFIRISHAJI
Alisema, kipaumbele cha kwanza cha Wizara hiyo ni kuendelea kuimarisha kuduma za usafiri na usafirishaji kwa kuimarisha miundombinu ya barabara
Alibainisha kuwa, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo barabara na viwanja vya ndege ina umuhimu mkubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha huduma na kuchochea uwekezaji.
Alisema, katika kipindi hiki, Serikali itaendeleza ujenzi wa miundombinu ya usafiri kwa kujenga barabara ya Tunguu-Makunduchi (km 48), Fumba – Kisauni (km 12), Mkoani – Chake (km 43.5) na barabara za Utalii Nungwi (km 12) pamoja na kuweka taa za barabarani katika maeneo yote hayo ikiwemo barabara za ndani.
Pia alisema, wataendeleza ujenzi wa barabara za mjini km 100.9, vijijini km 275 na barabra mpya za mjini km 333.7, pia watakamilisha ujenzi wa daraja na barabara ya Unguja Ukuu – Uzi na kujenga daraja litakalopita baharini la kuunganisha kijiji cha Chwaka na Charawe kuunganisha barabara baina ya mkoa wa Kusini na mkoa wa Kaskazini Unguja.
“Sasa hivi kuna Km. 100.9 tunazimalizia pamoja na fly over mbili, sasa katika utekelezaji wa ilani hii mpya kuwa karibu Km 333 barabara za mjini, na humo ndani mtakuwemo pia na madaraja ya juu katika maeneo yale ambayo tunahisi yatasaidia kupunguza msongamano wa magari,” alisema
KUIMARISHA BANDARI
Alisema, bandari ni sekta muhimu sana katika kukuza uchumi wa Zanzibar na ndiyo maana imekuwa ni kipaumbele cha Wizara hiyo kuhakikisha kuwa inaimarisha bandari sambamba na kujenga bandari nyengine mpya.
Alisema, sasa hivi biashara imekuwa Zanzibar na sababu mbali mbali kama vile kuongezeka kwa utalii, kuongezeka kwa uwekezaji na sababu mbali mbali nyengine zimepelekea biashara kukua sana.
Alisema, zaidi ya asilimia 90 ya bidhaa zinazoingia Zanzibar zinapita bandarini, na kusema kuwa bandari kubwa ya Malindi imeshazidiwa na ndiyo maana serikali imeweka mkazo wa kuhakikisha kuwa kwa kushirikiana na sekta binafsi wanapanua bandari ya Fumba ili meli ziwe zinakuja moja kw amoja katika bandari ya Fumba.
Pia alisema kwa kushirikiana na sekta binafsi bandari ya Mkoani Pemba pia itapanuliwa ili sasa meli kutoka nje ziweze kuingia moja kwa moja kwa ajili ya kuhudumia kisiwa cha Pemba na kupunguza gharama za bidhaa hizo.
KUIMARISHA HUDUMA ZA USAFIRI WA ANGA
Dk. Khalid alifahamisha kuwa, katika kipindi hiki wana lengo la kuongeza idadi ya abiria wanaotumia viwanja vyetu vya ndege kutoka million 2,140,986 kwa mwaka hadi kufikia abiria million 2,824,011 kwa mwaka ili kuongeza kipato na ajira.
Alisema, ili kufikia azma hiyo, wataendelea kuimarisha miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa ujenzi wa majengo na ukarabati wa baadhi ya majengo ya zamani, kujenga vituo viwili vya mafuta ya ndege na karakana ya kufanyia matengenezo ya ndege na kuongeza eneo la maegesho ya ndege kwa mita za mraba 106,000.
Aidha, alisema wataendeleza ujenzi wa njia ya kurukia ndege katika kiwanja cha ndege cha Pemba na kujenga jengo jipya la abiria sambamba na mpango wa kuujenga uwanja wa ndege wa Kigunda.
KUIMARISHA HUDUMA ZA USAFIRI WA BAHARINI
Alisema, katika kuimarisha usafiri wa baharini serikali inajenga boti za mwendo kasi mbili ambapo zitakuwa zikifanya kazi ya kusafirisha abiria baina ya Dar es saalam-Unguja-Pemba- Tanga na Mombasa.
Aidha alisema, hivi karibuni serikali inatarajia kuanzia usafiri wa MV Mapinduzi II ambayo ishamalizika matengenezo yake na muda wowote itaanza kazi lengo ni kuboresha huduma kwa wananchi.
MASHIRIKA YA UMMA
Akizungumza na Uhuru , kuhusiana na siku 100 za rais wa Zanzibar, Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammed Ibrahim Sanya alisema kupitia maelekezo bora na yenye kutoa dira na matokeo ya haraka kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, neema kubwa imekuja.
Alisema kuna mafanikio makubwa kwa mashirika ya umma Zanzibar kutokana na mikakati bora yenye dira, mwelekeo wa serikali ni kuhakikisha mashirika yanaleta mapinduzi kwa umma kama sasa ambapo mafanikio yamekuwa ni mengi.
MIKAKATI YA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR KWA MASHIRIKA YA UMMA
Alisema mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Mashirika ya Umma Zanzibar kwa miaka mitatu kutoka mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2026/2027 yametekeleza mageuzi ya kiutawala na kiutendaji yanayolenga kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma.
Alisema malengo ya kufanya hayo ni kuendeleza utoaji wa huduma kwa wananchi, uimarishaji wa uwekezaji wa kibiashara, kukuza ufanisi, uongezekaji wa mapato uwajibikaji, uwazi na matumizi bora ya rasilimali za umma.
“Katika kufikia mageuzi hayo, Serikali imepanga mikakati mbali mbali katika maeneo mengi ikiwemo Kuimarisha usimamizi wa Mashirika ya Umma na mali za Serikali. Ofisi ya Msajili wa Hazina inatarajia kukusanya gawio la jumla ya shilingi bilioni 71 kufikia mwaka wa fedha 2026/2027 kutoka shilingi bilioni 13 mwaka wa fedha 2022/2024,”
Aliendelee; “Pamoja na kukusanya shilingi bilioni 2 kama uwiano wa mapato yatokanayo na Mashirika ya Umma zisizotengeneza faida, na shilingi bilioni 8.3 kutoka shilingi bilioni 1.4 zinazotokana na mauzo ya mali chakavu na ukodishaji wa bohari na majengo.”
Aidha, alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Ofisi imepangiwa kianzio kipya cha ukusanyaji wa Mashamba ya Serikali ambapo jumla ya shilingi bilioni 0.21 zimekadiriwa kukusanywa.
Pia, alisema wanatarajia kuongezeka kwa idadi ya sera na miongozo itakayotolewa kutoka sita (6) hadi kumi na saba (17), na kuimarika kwa taarifa za kifedha kutoka kumi na nane (18) hadi ishirini na tano (25).
“Ongezeko la mapato hayo linasababishwa na kuimarishwa kwa ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa Mashirika ya Uwekezaji wa Umma na Taasisi za Umma, kuongezeka kwa idadi ya Mashirika ya Uwekezaji wa Umma, utekelezaji wa shughuli za ufuatiliaji, tathmini, uhakiki na tathmini ya mali za umma, tathmini ya matumizi ya mali za umma, pamoja na kuimarisha usimamizi wa kifedha kutoka Taasisi za Uwekezaji wa Umma.” alisema
Pia, alisema wanatarajia kuanzisha jumla ya miongozo sita (6) ya kiutendaji, kuongeza ujuzi wa watendaji katika masuala mtambuka hadi kufikia watendaji arobaini (40), na kuongeza asilimia ya wafanyakazi watakaopimwa katika hatua za kuimarisha utendaji.
“Ongezeko hili litatokana na kupatikana kwa mafunzo ya kitaalamu kwa wafanyakazi, kuanzishwa kwa kanuni na miongozo ya kiutendaji, uhamasishaji wa masuala mtambuka, pamoja na kutoa mafunzo ya kikazi na kuwaambatisha watendaji katika mafunzo ya kivitendo.” alisema
Kufanya ufuatiliaji, tathmini, ukaguzi wa ndani na uchambuzi: Katika hatua za kuimarisha ufuatiliaji, tathmini, ukaguzi na uchambuzi wa taarifa za Mashirika ya Uwekezaji wa Umma na Usimamizi wa Mali za Umma, Ofisi inapaswa kuhakikisha kuwa inaongeza ubora wa kazi zinazotekelezwa.
Hivyo, alisema mikakati imeweka msingi wa mageuzi ya kina kwa mashirika ya umma, ikilenga kuongeza mapato, kuboresha utendaji, kuimarisha uwajibikaji, kupunguza mianya ya rushwa na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika ipasavyo.




