NA SELINA MATHEW
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ameshusha maagizo manane kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini, akiwataka kuongeza uwajibikaji na kuandaa jedwali maalumu la namna wanavyotatua kero za wananchi kila mwezi.
Alisisitiza kila kiongozi katika nafasi yake anapaswa kuweka utaratibu wa kujali changamoto za wananchi, hivyo lazima viongozi watende haki.
Maagizo hayo aliyatoa katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, jana.
Katika agizo la kwanza, Dk. Mwigulu alisema hataki kuona wanafunzi wakibeba vidumu vya maji kwenda shuleni, wakati serikali imewekeza katika miundombinu ya maji.
“Tuna mitambo ya kuchimba maji na bajeti inaandaliwa. Sitaki kuona wanafunzi wanabeba vidumu vya maji, zahanati au shule ya msingi kukosa maji,” alisema.
Alisema serikali ina mpango wa kuchimba mabwawa kila wilaya ili kukomesha changamoto ya upatikanaji maji, hivyo aliwataka viongozi kuacha mazoea ya kukubali matatizo kama jambo la kawaida.
Agizo la pili, Dk. Mwigulu aliwataka viongozi ndani ya miezi sita baada ya kupitishwa bajeti mpya (2026/2027) wahakikishe hakuna shule ya msingi au sekondari itakayokuwa na upungufu wa matundu ya vyoo.
“Nimepita maeneo na kuona watoto wakipanga foleni kwenda kujisaidia wakati fedha za ujenzi zipo. Hili halikubaliki,” alisisitiza.
Akitoa agizo la tatu, Waziri Mkuu alikemea ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo, akieleza wapo baadhi ya watumishi wa umma wanalipana posho au kuwalipa wakandarasi bila mikataba halali kwa lengo la kugawana fedha.
“Kila mtu aheshimu fedha za miradi ya maendeleo. Kuanzia sasa, miradi na fedha zake zisiwe siri kwa sababu hiyo ni njia ya kutengeneza kichaka cha kuiba,” alisema.
Kuhusu agizo la nne, aliagiza kila fedha inapopelekwa katika halmashauri, nakala ya taarifa ipelekwe kwa mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, mbunge na madiwani kwa kuwa fedha hizo ni kodi za wananchi.
Pia, Dk. Mwigulu katika agizo lake la tano, aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuwasilisha taarifa ya kina kuhusu waliohusika, waliopokea na waliorejesha fedha walizofanya ubadhirifu katika ujenzi wa majengo wilayani Kiteto.
“Nipate taarifa ya mmoja mmoja na ushiriki wake kabla sijamaliza ziara yangu. Hatuwezi kuchezea fedha za umma namna hiyo,” alisisitiza.
Katika agizo la sita, aliwataka viongozi kuacha uzembe, rushwa na wizi, akionya hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa bila kujali nafasi za wahusika.
JEDWALI UTATUZI KERO ZA WANANCHI
Akizungumzia makusanyo ya ndani, Dk. Mwigulu, aliagiza apewe taarifa namna makusanyo ya ndani, hususan fedha za minada.
Alisema hakuna ustaarabu katika suala la mali ya umma, hivyo kila mtumishi wa umma anapaswa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za umma.
Alibainisha serikali imefika hadi ngazi za chini, lakini baadhi ya viongozi hawawajibiki ipasavyo kutatua migogoro ya wananchi, badala yake kujihusisha na majungu.
“Nataka jedwali la kila mwezi linaloonyesha namna kero za wananchi zinavyotatuliwa. Haiwezekani wananchi wafanye kazi za serikali wakati watumishi wa umma wapo,” alisema.
MIGOGORO WAKULIMA NA WAFUGAJI
Akitoa agizo la nane, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kutumia busara na undugu kutatua migogoro kati ya wafugaji na wakulima.
“Hakuna namna tunavyoweza kutenga shughuli za kilimo na ufugaji. Tuepuke kuleta uhasama kati ya pande hizi mbili. Heshimuni shughuli za wenzenu na zingatieni undugu,” alisisitiza.
Alionya serikali haina mzaha na mambo yanayoweza kuvuruga amani ya nchi na yeyote atakayevunja sheria kwa makusudi atachukuliwa hatua kali kulinda mshikamano na maendeleo ya taifa.
AMPONGEZA RAIS DK. SAMIA
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika mkoa huo na maeneo mengine nchini, kupitia utekelezaji miradi ya kimkakati.
“Tumpongeze Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya katika mkoa huu kupitia miradi ya maendeleo. Huu ni mkoa wangu wa nne kutembelea na nimeona mambo makubwa yamefanyika. Haya ni matokeo ya dhamira ya dhati ya kutatua kero za Watanzania,” alisema.
Alisema ndani ya miaka minne, serikali imejenga majengo 143 ya utawala, hospitali za wilaya 119, vituo vya afya 649 na zahanati 2,700. Aidha, vifaa vya uchunguzi wa kibingwa vimesambazwa katika hospitali zote za kanda na rufaa kuboresha huduma za afya.
Katika sekta ya maji, alisema awali kulikuwa na mitambo mitatu ya kuchimba visima vya maji nchi nzima, lakini kila mkoa una mitambo yake.
“Kwa sasa mitambo ipo ya kutosha. Ikitokea uchimbaji visima unasuasua huo utakuwa uzembe wa wasimamizi kwa sababu Rais Dk. Samia ametimiza wajibu wake,” alisisitiza.
Aliongeza katika Sekta ya Elimu, serikali imejenga madarasa 79,000, shule za msingi 27,000, shule za sekondari 1,300 na shule maalumu za wasichana katika kila mko na kuimarisha mafunzo ya amali.
KAULI YA NAIBU SPIKA
Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, alisema Bunge litaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali, kuhakikisha inatimiza wajibu wa kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi.
“Bunge lina wajibu kuisimamia na kuishauri serikali. Tutaendelea kushirikiana kuhakikisha ahadi na mipango inayopitishwa inatekelezwa kwa manufaa ya wananchi,” alisema.
Sillo alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha changamoto zinazoibuliwa na wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, alisema mkoa huo umenufaika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu.
Alisema miradi hiyo imechangia kuboresha huduma za kijamii, kuinua ustawi wa wananchi ingawa kuna changamoto zinazohitaji usimamizi wa karibu.
“Tuna changamoto ya migogoro ya ardhi inayosababishwa na uvunjifu wa sheria. Hata hivyo, tumeendelea kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo kwa kufuata maagizo ya viongozi wa juu, akiwemo Rais. Dk. Samia Suluhu Hassan,” alisema.
KAULI YA MBUNGE
Naye, Mbunge wa Kiteto, Edward Ole Lekaita, alisema pamoja na jitihada za serikali kuleta maendeleo, jimbo hilo linakabiliwa na changamoto zinazohitaji ufumbuzi haraka.
Alitaja baadhi ya changamoto hizo ni migogoro ya ardhi, kukatika umeme mara kwa mara na wanyamapori wakali kuingia katika maeneo ya wananchi.
“Tunaiomba serikali iangalie kwa kina masuala haya wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa amani na utulivu,” alisema.
Aliomba serikali kuchimba mabwawa katika eneo hilo kuwawezesha wananchi kuendesha kilimo cha uhakika kwa kuwa Kiteto ni eneo kame lenye changamoto ya upatikanaji maji.
Mbunge huyo alisema ujenzi wa mabwawa na miradi ya umwagiliaji utasaidia kuongeza uzalishaji mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua kipato cha wananchi.




