Dar es Salaam
NA ATHNATH MKIRAMWENI
SERIKALI imetangaza mafanikio ya sekta ya uchukuzi yaliyopatikana ndani ya siku 100, tangu Rais Dk. Samia Suluihu Hassan alipoapishwa kuongoza nchi kwa kipindi cha pili Awamu ya Sita.
Mafanikio hayo yamewezesha kuongeza mchango wa sekta hiyo kwa kuongeza Pato la Taifa kutoka asilimia 7.1 mwaka 2021 hadi asilimia 7.5 mwaka 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya serikali kufanya uwekezaji mkubwa kwa sekta hiyo.
Amesema serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imewekeza zaidi ya sh. trilioni 1.1 kuboresha na kupanua viwanja vya ndege nchini, kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria, ndege, mizigo na kuimarisha usalama.
Msigwa ameeleza miradi mikubwa inaendelea kutekelezwa katika viwanja vya ndege vya Arusha, Moshi, Mwanza, Serengeti, Kyabajwa (Kagera), Msalato, Shinyanga, Tabora, Kigoma na Sumbawanga, ambapo baadhi vimekamilika na vingine vikiwa katika hatua za mwisho.
Amesema uboreshaji huo umewezesha kuvutia mashirika saba ya ndege ya kimataifa mapya, ambayo ni Airlink, Zambia Airways, Saudia, Air France, Skyward Express, South African Airways na Xerin Air yaliyoanza safari zake nchini.
Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, amesema takwimu zinaonesha idadi ya abiria imeongezeka kutoka milioni 5.15 mwaka 2023/2024 hadi milioni 5.25 mwaka 2024/2025, huku mizigo ikiongezeka kwa asilimia 8.8.
Kuhusu Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Msigwa alisema serikali imeendelea kuliimarisha kwa kununua ndege mpya, ikiwemo Boeing 787-8 Dreamliner iliyowasili Agosti mwaka 2024 na kufanya shirika hilo kuwa na ndege 16.
Alisema uwekezaji huo umeiwezesha ATCL kupanua wigo wa safari kutoka vituo 23 mwaka 2020/2021 hadi vituo 33 mwaka 2025/2026, ikirejesha na kuanzisha safari katika miji ya Afrika na nje ya bara hilo.
“Katika kipindi cha mwaka 2024/2025, ATCL ilisafirisha abiria 1,178,025 na kukusanya dola milioni 157.69 sawa na ongezeko la asilimia 87.88, ikilinganishwa na mwaka uliotangulia huku ikichangia sh. bilioni 52.35 kama kodi na tozo mbalimbali.
SEKTA YA RELI
Msigwa alisema serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), imeendelea na ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilometa 1,219, ambapo hadi Desemba mwaka jana utandazaji wa reli ulikuwa umefikia kilometa 747 sawa na asilimia 61.
Alisema treni ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma imepunguza muda wa safari uliokuwa unatumiwa na abiria wa mabasi kati ya saa 10 na 12 hadi saa tatu hadi nne kwa treni na tayari zaidi ya abiria milioni 4.6 wamesafirishwa tangu kuanza kwa huduma hiyo.
Pia, alisema zaidi ya ajira 207,000 zimezalishwa kupitia mradi huo zikiwemo za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hatua inayochochea ukuaji uchumi na kipato cha wananchi.
“Serikali imeendelea kuboresha reli ya zamani (MGR) kwa kuongeza uwezo wa miundombinu, kununua mabehewa na vichwa vipya vya treni ili kuongeza ufanisi katika usafirishaji mizigo na abiria,” alisema.
Kuhusu reli ya TAZARA, Msigwa alisema Serikali za Tanzania na Zambia zimesaini mkataba wa ufufuaji na uboreshaji reli wake kwa kushirikiana na kampuni ya China ya CCECC, huku utekelezaji rasmi ukitarajiwa kuanza Juni mwaka huu.
MAFANIKIO BANDARI
Msigwa alisema serikali imekamilisha maandalizi ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga magati 10 mapya na matenki 15 ya kuhifadhi mafuta, hatua itakayoongeza uwezo wa bandari kuhudumia hadi tani milioni 50 kwa mwaka.
Alisema maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo yameanza, mradi unaotarajiwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji baharini katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Msigwa alieleza mapato ya forodha yameongezeka hadi kufikia sh. trilioni 8.2 katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari mwaka jana.
Kuhusu usafiri wa majini, alisema serikali imekamilisha ujenzi wa meli ya MV New Mwanza katika Ziwa Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo.
Msigwa alisema mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya serikali kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kama kichocheo cha biashara, uwekezaji, ajira na ustawi wa wananchi.
MELI KUKAMATWA
Akizungumzia suala la meli iliyokamatwa nchini El Salvador yenye bendera ya Tanzania inayodaiwa kubeba dawa za kulevya za tani 6.6, Msigwa alisema ni kweli serikali imepokea taarifa za kukamatwa kwa meli hiyo.
Alieleza kuwa baada ya kupitia takwimu imebainika kuwa ilisajiliwa Zanzibar kupitia wakala kwa mujibu wa taratibu za kimataifa za usajili wa meli chini ya Shirika la Kimataifa la Usafirishaji Baharini (IMO).
Alisema meli hiyo ilisajiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini ilikuwa inafanya kazi nje ya nchi na wakati wa kukamatwa hakukuwa na Mtanzania.
“Kutokana na tukio hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichukua hatua za haraka mara tu ilipopata taarifa Februari 17 mwaka huu ambapo kufikia Februari 18 mwaka huu, ilifuta rasmi usajili wa meli hiyo iliyotajwa kwa jina la FMS Eagos,” alisisitiza.
Alisema mbali na kufuta usajili, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imewatafuta wamiliki wa meli hiyo ili kupata maelezo ya kina kuhusu kilichotokea, pia imeitoza kampuni husika faini ya dola za Marekani 20,000 kwa mujibu wa taratibu za IMO.
Pia, alisema mawasiliano yanaendelea kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ili kuondoa utambuzi wowote wa kimataifa wa meli hiyo chini ya usajili wa Tanzania.




