Na ABDUL DUNIA, Zanzibar
WAKATI Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves akiahidi kuboresha zaidi aina ya uchezaji ili kukaribia ubingwa, Kocha wa Simba, Steve Barker anaamini timu yake ina nafasi ya kuwapiku wapinzani wake katika mbio za taji hilo msimu huu.
Makocha hao walitoa kauli hizo juzi muda mchache baada ya kutoka suluhu katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.
Baada ya matokeo hayo, sasa Yanga inaendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 11, JKT Tanzania ipo nafasi ya pili kwa alama 28, imecheza mechi 17 huku Simba ikifuatua kwa alama 24 imeshuka dimbani mara 11.
Ili Simba kuipiku Yanga inapaswa kwanza kufuta utofauti wa alama tano dhidi yake katika mechi 19 zilizosalia.
Akizungumza juzi, Kocha wa Simba, Barker alisema ikiwa kikosi chake kitaendelea kuonyesha kiwango kama kilichoonyesha dhidi ya Yanga anaamini bado watakuwa na nafasi kubwa ya kutwaa taji.
“Bado kuna mechi nyingi za kucheza, kweli wametuzidi alama tano lakini bado kuna mechi lakini pia Yanga inaweza kufanya makosa.
Kama tutaendelea kucheza kama tulivyocheza leo(juzi) na kuepuka kufanya makosa basi bado tuna nafasi kubwa tukawa mabingwa,” alisema.
Pia, Barker aliongeza kuwatimu yake ilikuwa bora kiwanjani hasa kipindi cha kwanza, kwa kutengeneza nyingi walikosa kufunga mabao.
Naye Kocha wa Yanga, Pedro alisema ataendelea kukiboresha kikosi chake kimbinu kuzikabili kila timu wanazokutana nazo.
“Tutazidi kujipanga kuhakikisha tunacheza vyema zaidi katika aina hii ya mechi. Lengo ni kuendelea kupata matokeo mazuri,” alisema.
Pia, Pedro alisema katika mchezo wa juzi, Simba ilianza vyema lakini baadaye kikosi chake kilirejea katika staili yake na kucheza soka safi.
Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo ikifanya hivyo kuanzia 2021/2022, 2022/2023, 2023/2024 na 2024/2025.
Mara ya mwisho Simba kubeba taji hilo ulikuwa msimu wa 2020/2021 na tangu hapo haijatwaa taji lolote kubwa.




