Na SUPERIUS ERNEST
MWANAMKE wa kwanza kuteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji mstaafu Julie Catherine Manning, amefariki dunia.
Jaji Julie alikuwa miongoni mwa wanafunzi 18 wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akiwa mwanamke wa kwanza katika kitivo cha sheria ambapo alihitimu mwaka 1963.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, kufuatia kifo cha jaji mstaafu huyo kilichotokea Upanga, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu na kutiwa saini na Shaaban Kissu, taifa limepoteza kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha misingi ya haki, usawa na uadilifu nchini.
Taarifa hiyo ilisema Jaji Julie atakumbukwa kama kinara aliyefungua milango kwa wanawake wengi kushiriki katika taaluma ya sheria na uongozi. Jaji Julie alikuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa jaji katika mahakama kuu kwa nchi za Afrika Mashariki.
“Tutamkumbuka kwa weledi na uadilifu katika utumishi wake. Ameacha urithi wa mfano bora kwa vizazi vijavyo,” ilieleza taarifa hiyo.
Rais Dk. Samia alitoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, na watumishi wa kada ya sheria nchini, huku akiwaasa Watanzania kumuenzi jaji huyo kwa kuendelea kudumisha misingi ya haki, usawa na utawala wa sheria.
Alifariki dunia katika Hospitali ya Hitech Sai Healthcare ya jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akitibiwa.
WAZIRI HOMERA
Naye, Waziri wa Katiba na Sheria, Juma Homera, alitoa pole kwa familia na wananchi kwa ujumla kutokana na kifo hicho.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dk. Homera aliandika: “Pumzika kwa amani jaji mstaafu na Waziri wa Sheria mstaafu.”
JAJI WARIOBA, MULAMULA
Akizungumzia msiba huo, Jaji mstaafu Joseph Warioba, alisema kiongozi huyo alikuwa imara katika kutekeleza majukumu yake mbalimbali yakiwemo ya uwaziri na aliwasimamia vyema wakati huo yeye akiwa mwanasheria mkuu wa serikali.
“Nimepokea taarifa za msiba wa kiongozi huyu kwa masikitiko makubwa na nilikuwa msibani, tumepoteza kiongozi mahiri aliyetekeleza majukumu yake kwa weledi,” alisema Warioba.
Alisema alisoma na Jaji Julie Chuo Kikuu cha Dar es Salaam japo yeye alikuwa amemtangulia kwa kujiunga masomoni mwaka 1961, Jaji Warioba akiingia 1963.
Alieleza mwaka 1973 aliteuliwa kuwa jaji akiwa kitengo cha sheria mahakama kuu, 1965 yeye na mama Chiwale, walikuwa wanawake wa kwanza kuteuliwa baraza la mawaziri, huku Jaji Warioba akiteuliwa mwanasheria mkuu wa serikali.
Alisema katika uongozi wao, walikuwa ni vijana wenye umri chini ya miaka 35, ambapo kipindi hicho kilikuwa kigumu ikiwemo kupanda bei ya mafuta, kuvunjika Jumuiya ya Afrika Mashariki na vita ya Kagera.
“Kazi ilikuwa ngumu, lakini alitusimamia vyema, japokuwa watu walikuwa hawaamini kama wanawake wana uwezo, lakini yeye (Julie) na Chiwale walifanya kazi njema wakaaminika,” aliongeza Jaji Warioba.
Naye, Balozi Liberatha Mulamula alisema amepokea taarifa ya msiba huo kwa masikitiko makubwa, kwani jaji huyo mstaafu ni miongoni mwa wanawake waliofanya vyema katika uongozi na kuwa chachu kwa wanawake wengi kupenda uongozi.
Alisema alimfahamu kutokana na uongozi wake mahiri na kumwombea mapumziko mema kwa Mungu.
Mwanasiasa mkongwe Anna Abdallah, alisema amepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa, kwani ni miongoni mwa viongozi wanawake wa kwanza waliowapa hamasa kubwa siyo katika uongozi tu hadi kielimu.
Alisema jaji huyo atakumbukwa kwa historia kubwa, ni miongoni mwa watanzania wachache wa kwanza kusoma taaluma ya sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye kuteuliwa jaji wa mahakama kuu akiwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo.
WASIFU WAKE
Jaji Julie Manning aliteuliwa jaji wa mahakama kuu mwaka 1973 hadi 1975 na baadaye kuwa Waziri wa Sheria kuanzia mwaka 1975 hadi 1983, akiaminiwa na Rais Julius Nyerere.
Alikuwa miongoni mwa wanafunzi 18 wa kwanza wa UDSM, huku akiwa mwanamke wa kwanza katika kitivo cha sheria ambapo alihitimu mwaka 1963.
Aliajiriwa ofisi ya mwanasheria mkuu kwa nafasi ya mwandishi wa sheria na kupelekwa Uingereza chini ya sekretarieti kujiendeleza katika ujuzi wa kazi hiyo.
Jaji huyo alizaliwa Januari 24, 1939 mkoani Morogoro.




