Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema serikali imejipanga upya kuyatangaza na kuyainua madini ya Tanzanite kimataifa kupitia mkakati wa kurejesha hadhi ya jiwe hilo adimu duniani.
Akizungumza katika mkutano na wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini ya vito katika eneo tengefu la ukuta wa Magufuli, Mirerani mkoani Manyara, Waziri Mavunde, alisema hatua hiyo, inalenga kurejesha hadhi na uhitaji wa Tanzanite kuimarisha thamani na soko lake duniani.
Katika Mkutano huo, ambao ulihusisha hafla ya kukabidhi leseni kwa wanufaika 423, Mavunde alisema serikali imedhamiria kurejesha minada ya madini ya vito kama njia ya kuongeza uwazi, ushindani na thamani ya madini ya vito nchini.
Akifafanua zaidi, alisema serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa Tanzanite Exchange Centre (TEC), jengo ambalo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 98 likiwa la ghorofa mbili, hivyo alimtaka mkandarasi kuongeza kasi kituo hicho kianze kufanya kazi na kutumika kama kitovu cha kimataifa cha biashara ya Tanzanite.
“Tunataka wageni wanaokuja kununua Tanzanite wapate huduma zote muhimu katika eneo moja, kuanzia huduma za kibenki, hoteli, hadi miundombinu rafiki ya biashara,” alieleza.
Pia, Waziri Mavunde alisisitiza kuwa, dhamira ya serikali, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona Mirerani, Arusha na maeneo mengine nchini, yanakuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito barani Afrika.
“Rais Samia anataka kuona mfumo wa biashara ya madini ya vito kama ilivyo Hong Kong na Dubai ikihama na kuja hapa Simanjiro,” alisema.
Alieleza mikakati ya kutatua changamoto za wachimbaji wadogo, Waziri Mavunde, alisema serikali inafanya mazungumzo na Wizara ya Fedha, kuwezesha upatikanaji wa mitaji kupitia mifuko ya dhamana kuwawezesha vijana, wanawake na wachimbaji wadogo kuimarisha shughuli zao.
Aidha, alisema serikali imenunua mitambo 15 ya uchorongaji kuwasaidia wachimbaji hao kuongeza uzalishaji.
Katika taarifa ya mapato ya serikali, Mavunde alisema sekta ya madini, imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi, ambapo mwaka jana kwa mara ya kwanza, iliingiza katika mfuko mkuu wa serikali sh. trilioni moja.
Aidha, kwa mwaka huu wa fedha, sekta hiyo imepangiwa kukusanya sh. trilioni 1.2, hadi sasa zaidi ya sh. bilioni 500, tayari zimekusanywa.
Waziri Mavunde, alisema bado kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana Tanzanite nje ya eneo la ukuta wa Mirerani na kwamba, serikali inaendelea kufanya utafiti wa kina kubainisha maeneo mapya yenye rasilimali hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA), Jeremiah Kituyo, aliahidi kuendelea kushirikiana na serikali kudhibiti utoroshaji wa madini hayo akisema chama hicho, kitaendelea kutoa taarifa kuimarisha usimamizi wake.




